Waziri Mkuu asisitiza Serikali ipo imara, miradi yote itatekelezwa kwa ufanisi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo imara na miradi yote ya kimkakati inaendelea kujengwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani nayo.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo makini na inaendelea kuwatumikia Watanzania. ”Tuendelee kuchapa kazi”.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa nyumba za makazi ya waliyokuwa wakazi wa eneo la Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri mkuu).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 20, 2021 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam.

”Siri ya kuwepo mafanikio na maendeleo nchini ni utulivu na amani. Tulianza vizuri tangu Serikali ya Awamu ya kwanza, tutaendelea kuimarisha amani na utulivu.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi na vibarua wa TBA, wakati alipokagua mradi wa nyumba za makazi ya waliyokuwa wakazi wa eneo la Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo kuliko mambo mengine yasiyo na tija.

Akizungumzia kuhusu mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema amefurahi kukuta majengo yamekamilika na kwamba ameridhika na maendeleo ya ujenzi wake.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanakamilisha kazi iliyosalia haraka ili mwaka huu wananchi waanze kuishi hapo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini (TBA,) Mbunifu Majengo. Daud Kondoro, wakati alipokagua nyumba za Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia moja ya chumba, wakati alipokagua mradi wa nyumba za makazi ya waliyokuwa wakazi wa eneo hilo, Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, Bw. Daud Kondoro amesema mradi huo una jumla ya block tano na ambazo zinauwezo wa kuchukua familia 656.

Amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo za makazi pia katika eneo hilo wanajenga maduka makubwa pamoja na vizimba kwa ajili ya wajasiriamali kufanya biashara.

Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika Mei 2021. Hadi sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji wake na gharama yake ni shilingi bilioni 50.

Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota, Waziri Mkuu alikagua kituo cha Reli ya Kisasa cha Tanzanite jijini Dar es Salaam

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news