Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataja vipaumbele vya Serikali

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 13, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.) KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2021/2022
UTANGULIZI

Shukrani

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo ndani ya Bunge lako tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti zilizochambua Bajeti ya Mfuko wa Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2020/2021 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2021/2022. Aidha, naliomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na hotuba hii, ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa fadhila zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo kwa ajili ya kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2020/2021 na mwelekeo wake kwa mwaka 2021/2022 tukiwa na siha njema.

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa huu ni Mkutano wa Tatu wa Bunge la 12. Aidha, ni Mkutano wa Kwanza wa Bunge la Bajeti tangu kuzinduliwa kwa Bunge hili tarehe 13 Novemba 2020. Mkutano huu, unafanyika wakati ambao Tanzania imepitia majuma kadhaa ya huzuni, majonzi makubwa na maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Salamu za Pole

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie tena fursa hii adhimu kutoa pole kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge lako tukufu, wanafamilia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kumpoteza kiongozi wetu mpendwa. Aidha, naishukuru Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mazishi kwa kujitoa kwao usiku na mchana kufanikisha taratibu zote muhimu za maziko sambamba na kuhakikisha kuwa kiongozi wetu anapewa heshima zote za mwisho hadi alipolazwa kwenye nyumba yake ya milele.

Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Rais Samia Sululu Hassan kutoa wito kwa Watanzania wenzangu kuwa tuendelee kushikamana, kushirikiana, kupendana na kuchapa kazi. Aidha, kwa upande wetu Waheshimiwa Wabunge, Viongozi na Watendaji wote, nasi hatuna budi kuendeleza ushirikiano, kuchapa kazi na kuwatumikia ipasavyo Watanzania kwa kulinda na kutetea maslahi mapana ya nchi yetu. Hii ndio njia sahihi ya kumuenzi mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sote tutakumbuka kuwa msiba wa kiongozi wa nchi ulikuja wakati ambao Taifa lilikuwa bado halijasahau tukio la tarehe 17 Februari, 2021 wakati Taifa lilipopokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo.

Mheshimiwa Spika, Maalim Seif atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa chama chake, watu wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla, hususan kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, tuliondokewa pia na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John William Herbert Kijazi. Mheshimiwa Balozi Kijazi atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka wakati akiitumikia Serikali kwenye nyadhifa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana tarehe 12 Aprili, 2021 nchi yetu imeadhimisha kumbukizi ya miaka 37 ya kifo cha hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufariki dunia tarehe 12 Aprili, 1984. Watanzania tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi jemedari huyo, kwa uzalendo, uhodari na uchapakazi wake wakati wote wa uhai wake.

Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa Taifa limepoteza watu muhimu waliotoa mchango mkubwa katika uongozi, maendeleo, ustawi wa Taifa letu sambamba na kuimarisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa. Hivyo, tuendelee kuenzi na kujifunza mambo mazuri yaliyoachwa na viongozi hao, huku tukimuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina!

Mheshimiwa Spika, mkutano huu wa tatu wa Bunge la 12 ni wa Bajeti ya Serikali, nami naanzisha kusoma Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2021/2022. Kabla sijaendelea na hotuba yangu hii naomba uruhusu tusimame walau kwa dakika moja kwa lengo la kuwaombea marehemu wetu ili Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani.

Salamu za Pongezi

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushika nafasi ya kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa Rais wetu nguvu, ulinzi, afya na kila lililo la heri katika kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nampongeza pia, Mheshimiwa Philip Isidor Mpango, kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitishwa kwa asilimia 100 na Waheshimiwa Wabunge. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif Kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, natambua kuwa Mkutano huu wa bajeti ni wa kwanza kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa msingi huo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuitumie vyema fursa hii kutoa michango itakayosaidia Serikali kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango na Bajeti ya Mwaka 2021/2022. Serikali kwa upande wake, itaendelea kuheshimu, kuthamini na kuifanyia kazi michango ya Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kushughulikia kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, kipekee, napenda kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuendelea kuonesha umahiri na uwezo mkubwa katika kusimamia shughuli za Bunge. Hivyo basi, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu hususan wale walioingia katika Bunge hili kwa mara ya kwanza ili tutumie vizuri uzoefu wenu katika kujifunza namna bora ya kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Nampongeza kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nawashukuru pia Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako tukufu kwa ushauri walioutoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maoni na ushauri wao utazingatiwa vilivyo wakati wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano mlionipatia wakati nikitekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa na hivyo, kuwezesha Serikali kutekeleza kazi zake kwa tija na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, nawashukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Geofrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Masasi Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji); Mheshimiwa William Tate Ole Nasha Mbunge wa Ngorongoro na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji); Mheshimiwa Paschal Patrobas Katambi, Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) na Mheshimiwa Ummy Hamis Nderiananga, Mbunge wa Viti Maalum na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu).

Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru sana Bwana Tixon Tuyangine Nzunda, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakurugenzi na Wakuu wa vitengo, Wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia wakati nikitekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru waliokuwa Makatibu Wakuu, Bibi Dorothy Aidan Mwaluko na Bw. Andrew Wilson Massawe kwa kazi nzuri waliyoifanya wakati wote wakiwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia natoa pongezi kwa Profesa Godius Kahyarara kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Profesa Jamal Adam Katundu na Bwana Kaspar Kaspar Mmuya kwa kuteuliwa kuwa Naibu Makatibu Wakuu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Hongereni sana!

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea nchi yetu maendeleo. Mchango wao umekuwa muhimu na kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.

Mheshimiwa Spika, makadirio ya bajeti ninayowasilisha leo ni sehemu ya utekelezaji wa yale yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Makadirio hayo, yamezingatia ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni na katika uzinduzi wa Bunge hili tarehe 13 Novemba, 2020. Vilevile, makadirio hayo ya mapato na matumizi yamezingatia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo, matumizi ya fedha za umma sambamba na uwajibikaji. Serikali itatumia rasilimali chache zilizopo katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza tija ili kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi na maendeleo ya watu. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hayo, ningependa kuwahakikishia wananchi na Bunge lako tukufu kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ile ya kimkakati na inayolenga kuboresha huduma pamoja na kuboresha maisha ya wananchi. Serikali itahakikisha ahadi alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Rais wetu, hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli zinatekelezwa sambamba na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2020/2021

Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Juni 2021, tutahitimisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021). Aidha, kuanzia Julai mosi 2021, Serikali itaanza kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, Mpango huo ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025. Dira hiyo, ina lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati na hali bora ya maisha ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo, hatunabudi kujipongeza kwa nchi yetu kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda tuliojiwekea. Kuingia katika uchumi wa kati ni kiashirio cha kuongezeka kwa uwezo wa Taifa kugharamia huduma muhimu kwa wananchi sambamba na uwezo wa wananchi kugharamia mahitaji yao. Natoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ili kulinda na kuendeleza mafanikio tuliyoyapata.

Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021, Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi trilioni 34.88. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 22.10 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.78 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021 umekuwa wa mafanikio makubwa. Hivyo basi, naomba japo kwa uchache nilieleze Bunge lako tukufu na Watanzania wote baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo ni pamoja na Serikali kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imekuwa na mwendelezo kutokana na kuhitaji muda wa zaidi ya miezi 12. Baadhi ya miradi hiyo ni kama ifuatavyo:-

Mosi: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90.34 na kipande cha Morogoro - Makutupora (km 422) asilimia 57.57. Aidha, tayari Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora - Tabora (km 294) na Tabora - Isaka (km 133) na hapo baadaye kujenga njia ya Tabora - Kaliua - Kigoma (km 411) na Kaliua - Mpanda (km 207). Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 jumla ya shilingi bilioni 596.8 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu.


Pili: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115): Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 45 hadi Machi 2021 ambapo shilingi trilioni 2.1 zimetumika na ajira zaidi ya 7,000 zimezalishwa.



Tatu: Usambazaji wa Umeme Vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini na Makao Makuu ya Wilaya (REA - III): Hadi Februari 2021, jumla ya vijiji 10,294 kati ya vijiji 12,317 sawa na asilimia 83.3 vilikuwa vimeunganishwa umeme ambapo shilingi bilioni 323.7 zimetumika. Kwa sasa tumebaki na vijiji 1,974. Usambazaji wa umeme katika maeneo hayo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha hali ya biashara za wananchi na hivyo kujiongezea kipato. Lengo la Serikali ni kukamilisha usambazaji umeme katika vijiji vyote hadi visiwani na kwenye vitongoji.

Nne: Kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwenye maziwa makuu: Katika Ziwa Victoria tumejenga chelezo na meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu inajengwa. Aidha, tumekarabati meli za New Butiama Hapa Kazi Tu, New Victoria Hapa Kazi Tu, MV. Clarias na ML. Wimbi.

Ziwa Tanganyika: Kukamilika kwa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo pamoja na kuendelea na ukarabati wa meli ya MV Liemba na ukarabati wa meli ya MT Sangara.

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja na kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa meli mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200.

Tano: Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kukamilika kwa barabara ya juu ya Kijazi (Dar es Salaam) ambayo imezinduliwa, kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza) ambao umefikia asilimia 14.5; na daraja la Tanzanite (Dar es Salaam) ambao umefikia asilimia 71.3.

Sita: Miradi ya Maji: kuwezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji ambapo wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama imefikia asilimia 86 kwa mijini na asilimia 72.3 vijijini. Hadi Machi 2021, shilingi bilioni 241.3 zimetumika na kazi ya usambazaji maji vijijini inaendelea.

Saba: Elimu: Hadi kufikia Januari 2021, shilingi bilioni 178 zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu muhimu katika shule za msingi, sekondari na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Uimarishaji wa miundombinu ya elimu utasaidia kuongeza ubora wa elimu inayotolewa na hivyo kuongeza idadi ya wahitimu wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri; na

Nane: Afya: Hadi kufikia Januari 2021, shilingi bilioni 69.4 zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya inayohusisha hospitali za rufaa za kanda, mikoa na hospitali za halmashauri. Vilevile, tumejenga vituo vya afya na zahanati kote nchini. Hatua hiyo imesaidia kuboresha huduma za afya zinazotolewa na kuwezesha wananchi wengi kupata huduma ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 pia ulikumbwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kupungua kwa shughuli za kibiashara na uzalishaji duniani kulikosababishwa na athari za COVID-19 na uharibifu wa miundombinu ya barabara kutokana na mafuriko.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua za tahadhari dhidi ya majanga, kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko na kuimarisha ukaguzi wake pamoja na kuimarisha utekelezaji na usimamizi wa sera za uchumi jumla na bajeti.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 mwelekeo wa kazi za Serikali utajikita katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/2022 ambao ni wa kwanza katika hatua za utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (2021/2022 - 2025/2026). Vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2021/2022 vimejikita katika masuala makuu matano ya Mpango wa Tatu. Masuala hayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2021/2022, pia, utajumuisha ukamilishaji wa miradi ya kipaumbele na ya kimkakati ambayo utekelezaji wake haukukamilika katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021).

Mheshimiwa Spika, katika kufikia malengo hayo, Serikali itajikita katika kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kuimarisha utulivu wa uchumi jumla; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuimarisha uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje na kuendeleza miundombinu na huduma katika maeneo ya reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini, usafiri wa anga, TEHAMA, nishati, ujenzi wa bandari na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuihakikishia sekta binafsi kuwa kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa kiuchumi na kijamii, Serikali kupitia Mpango wa Mwaka 2021/2022 itaendelea kuhakikisha kuwa sekta binafsi inashamiri kwa kuainisha fursa zilizopo, kuweka vipaumbele vitakavyowezesha maendeleo ya sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji. Nitoe rai kwamba sekta binafsi ilete mpango mahsusi kuhusu namna ambavyo itaunga mkono mipango na mikakati ya Serikali ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira milioni nane katika kipindi cha miaka mitano.

HALI YA UCHUMI

Hali ya Uchumi wa Dunia

Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi wa dunia ilidorora katika mwaka 2020 ikilinganishwa na mwaka 2019. Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Januari 2021 inaonesha kuwa uchumi wa dunia ulikadiriwa kushuka kwa asilimia 3.5 katika mwaka 2020 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.8 mwaka 2019. Kudorora huko, kumetokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba dunia katika kipindi hicho zikiwemo janga la ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19), mgogoro wa kibiashara baina ya mataifa yenye uchumi mkubwa duniani na hatua zisizo rafiki zilizochukuliwa na baadhi ya nchi katika kujikinga na maradhi hayo.

Hali ya Uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa inaonesha kuwa uchumi wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ulikadiriwa kushuka kwa asilimia 2.6 mwaka 2020 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.2 mwaka 2019. Sababu za kudorora kwa hali hiyo ya uchumi ni kama zilizobainishwa katika hali ya uchumi wa dunia.

Hali ya Uchumi wa Taifa

Mheshimiwa Spika, licha ya changamoto ambazo baadhi nimezieleza hapo juu, uchumi wa Tanzania umeendelea kufanya vizuri katika kipindi hicho. Katika mwaka 2020, Benki ya Dunia ilikadiria uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 2.5 kutokana na athari za janga la COVID-19 lililoikumba dunia. Hata hivyo, katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.7. Kasi hiyo, ilitokana na uamuzi wa Serikali wa kutofunga shughuli za kiuchumi (Lock down) kufuatia mlipuko wa COVID-19.

Mfumuko wa Bei

Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu katika kiwango cha chini, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.5 Januari 2021, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Katika kipindi chote cha mwaka 2020, mfumuko wa bei ulikuwa ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0 na ndani ya wigo uliowekwa kwa mujibu wa vigezo vya mtangamano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kiwango ambacho hakizidi asilimia 8.0.

Mheshimiwa Spika, kiwango hicho cha mfumuko wa bei, pia kilibaki ndani ya wigo uliowekwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa kati ya asilimia 3.0 na 7.0. Kushuka kwa mfumuko wa bei kulitokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, bei ndogo ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani na sera madhubuti za fedha na bajeti. Serikali itaendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuwa na mwenendo tulivu wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo inayotarajiwa kuleta matokeo makubwa na ya haraka katika uchumi. Msukumo mkubwa utawekwa katika maeneo ambayo yanachochea mageuzi ya viwanda, ukuaji wa ajira, maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara, tulivu na shindani.

BUNGE

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Bunge lako tukufu limetekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumu yake ya msingi ya kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Katika kipindi hicho, Bunge lilisimamia na kuratibu shughuli za Mikutano Mitatu ya Bunge ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12. Katika Mkutano wake wa Pili, Bunge lilijadili hotuba ya hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba 2020 wakati akifungua Bunge la 12.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango, kujadili na kushauri kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Ofisi ya Bunge itaendelea kuratibu shughuli za mikutano minne ya Bunge pamoja na Kamati za Kudumu za Bunge, kuratibu ushiriki wa Wabunge katika Mikutano ya Kimataifa kama SADC – Parliamentary Forum, Bunge la Afrika Mashariki, Maziwa Makuu, Inter-Parliamentary Union (IPU) na Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Aidha, itaendelea kukarabati ukumbi wa Bunge na kuboresha miundombinu mingine ya ofisi zake ili kuwezesha shughuli za Bunge kufanyika kwa ufanisi na tija.

MAHAKAMA

Uendeshaji wa Mashtaka na Utoaji Haki

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya utoaji haki na huduma zitolewazo na Mahakama kwa kukamilisha miradi ya ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi mbili katika Mikoa ya Simiyu na Njombe. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mahakama za Wilaya tatu katika Wilaya za Kasulu, Longido na Makete na Mahakama za Mwanzo sita katika maeneo ya Ngerengere, Mtae, Msanzi, Laela, Mtowisa na Kibaigwa na ujenzi wa mahakama nyingine mpya za milaya 25 katika maeneo ambayo hayana huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 127,344 ikiwa ni pamoja na mashauri 120,938 yaliyosajiliwa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2020. Moja ya mifumo iliyotumika ili kuimarisha ufanisi katika utoaji haki kwa wananchi ni utekelezaji wa mradi wa Mahakama maalum zinazotembea. Lengo la mahakama hizo ni kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi hususan walio katika sehemu zisizo na Mahakama ili kuweza kuzisikiliza kesi na kuzimaliza.

Mheshimiwa Spika, katika hatua ya majaribio, Serikali imeanzisha huduma hiyo katika Wilaya tano nchini. Wilaya hizo ni Kinondoni (Bunju), Ilala (Chanika), Temeke (Buza) na Ubungo (Kibamba) kwa mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ilemela (SAUT) kwa Mkoa wa Mwanza. Jumla ya mashauri 446 yamesajiliwa kwenye Mahakama hizo na mashauri 401 kusikilizwa na kuhitimishwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa Taifa wa kutenganisha mashtaka na shughuli za upelelezi kwa kusogeza huduma za mashtaka karibu na wananchi ili kurahisisha shughuli za utoaji haki. Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Serikali ilifungua jumla ya ofisi mpya sita za Taifa za Mashtaka katika mkoa wa Songwe na wilaya za Mufindi, Serengeti, Kahama, Karagwe na Kilombero. Lengo ni kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi na hivyo kupunguza muda na gharama za uendeshaji wa mashtaka.

UWEKEZAJI

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha shughuli za uwekezaji nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje. Juhudi hizo zilihusisha kuunganisha watumishi walio katika huduma za mahala pamoja kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwenye mfumo na kupewa idhini ya kuutumia kwa ajili ya kurahisisha maombi ya vibali vya uwekezaji. Lengo ni kuhakikisha kwamba vibali na leseni mbalimbali za uwekezaji na biashara kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania vinatolewa ndani ya siku 14. Hatua hiyo inalenga kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya ukuaji wa sekta binafsi. Serikali itaendelea kutoa taarifa muhimu zinazohitajika kwa wakati na kushughulikia changamoto za wawekezaji kwa kuzingatia sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali imekamilisha tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996. Tathmini hiyo imeonesha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho ikiwemo ukuaji wa uwiano wa uwekezaji kwa Pato la Taifa kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019. Aidha, tathmini hiyo imeainisha changamoto mbalimbali za kisera, kisheria na kiutendaji. Kutokana na tathmini hiyo, Serikali inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kuvutia uwekezaji. Katika mwaka 2020/2021, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 100. Miradi hii inatarajiwa kuwekeza mtaji wa dola za Marekani milioni 536.04 na kutoa ajira 9,085. Sekta ya Viwanda imeongoza kwa idadi ya miradi 64 sawa na asilimia 64 na mtaji wa uwekezaji wa dola za Marekani milioni 370.41.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itakamilisha na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ikiwemo kuendeleza miundombinu muhimu ya uwekezaji katika mikoa yote ili kuvutia uwekezaji, kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara, kuimarisha uhamasishaji wa fursa za uwekezaji na kuboresha mfumo wa upatikanaji wa taarifa za uwekezaji kwa kufanya tafiti na kuandaa Kanzidata ya Uwekezaji ili kuwa na takwimu sahihi za uwekezaji wa ndani na nje ikiwa ni pamoja na idadi ya miradi ya uwekezaji, thamani na ajira zinazozalishwa kutokana na uwekezaji huo.

SEKTA ZA UZALISHAJI

Kilimo

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo kwa lengo la kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ajira. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwawezesha wakulima kupata pembejeo, zana za kisasa, teknolojia na mbegu bora ili kuongeza tija katika kilimo. Kadhalika, Serikali inaimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ili kuhakikisha wakulima wanafaidika na mauzo ya mazao.

Hali ya Upatikanaji wa Chakula

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha katika maeneo yote nchini imeendelea kuimarika. Mipango madhubuti ya Serikali, mageuzi yanayoendelea kutekelezwa katika sekta ya kilimo pamoja na kuimarika kwa hali ya hewa ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuimarika huko. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 18.1 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 14.4. Uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 126 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua za kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula, Serikali inaimarisha miundombinu ya kuhifadhi chakula. Hivi sasa, ujenzi wa vihenge vya kisasa, katika miji ya Babati, Mpanda, Sumbawanga, Shinyanga, Dodoma, Mbozi, Makambako na Songea umefikia asilimia 87.39. Vilevile, ujenzi wa maghala na miundombinu mingine katika miji ya Songea, Makambako, Shinyanga, Babati, Mpanda na Sumbawanga umefikia asilimia 60.65. Miundombinu hiyo itakapokamilika uwezo wa kuhifadhi chakula utaongezeka kwa kiasi cha tani 501,000 kutoka tani 251,000 za sasa.

Upatikanaji wa Mbolea

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima kwa wakati sambamba na matumizi ya mbinu bora za kilimo ikiwemo teknolojia umeimarishwa. Lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji na kufanya kilimo chetu kiwe chenye tija kwa kuhimiza usambazaji wa pembejeo kwa wakati na kulingana na mahitaji ya kila mkoa.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mbolea nchini umeendelea kuimarika. Aidha, matumizi ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja umekuwa chachu ya kuimarika kwa upatikanaji na kupungua kwa bei. Hadi Februari 2021, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 631,660 sawa na asilimia 88 ya mahitaji ya tani 718,051. Serikali inaendelea kuhakikisha asilimia 12 iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati ili kukidhi mahitaji kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji wa mazao.

Uvamizi wa Nzige wa Jangwa

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa hivi karibuni baadhi ya maeneo hapa nchini yalivamiwa na nzige wa jangwa. Kufuatia uvamizi huo, Serikali imefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige yaliyoingia mwezi Januari, 2021 katika Wilaya ya Mwanga na baadaye Simanjiro. Pia, imefanikiwa kudhibiti makundi mapya yaliyoingia tarehe 15 Februari, 2021 katika Wilaya ya Longido na Monduli.

Mheshimiwa Spika, hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali ziliwezesha udhibiti wa nzige hao kabla hawajaleta madhara yoyote kwenye mazao ya wakulima wetu. Niwahakikishie Watanzania wenzangu kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mbinu zote za kupambana na wadudu hawa waharibifu wa mazao sambamba na matumizi bora ya zana za kisasa na teknolojia.

Kilimo cha Umwagiliaji

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali imeendelea kuimarisha kilimo cha umwagiliaji baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu 17 za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 8,536 kupitia Mpango wa Pili wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II) na kukamilika skimu tano ambazo ni Kigugu - Mvomero (hekta 195), Msolwa Ujamaa (hekta 40), Njage - Kilombero (hekta 75), Mvumi (hekta 249) na Kilangali Seed Farm - Kilosa (hekta 400) kupitia Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Mpunga (ERPP). Pia, imetoa mafunzo kwa wakulima na wakulima viongozi 1,000 katika uandaaji wa mipango ya matunzo na uendeshaji wa skimu pamoja na usimamizi wa rasilimali maji katika skimu 50.

Kuimarisha Ushirika

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali iliendelea kudhibiti, kusimamia na kuhamasisha ushirika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Aidha, Serikali imefanikiwa kurejesha mali za vyama vya ushirika zenye thamani ya shilingi bilioni 48.98 na kufanya mali zilizookolewa hadi kufikia Desemba 2020 kuwa na thamani ya shilingi bilioni 68.9. Mali hizo ni pamoja na majengo, viwanja, magari na mitambo ya mashine.

Mheshimiwa Spika, Serikali itasimamia na kuunganisha Wizara na Taasisi zinazoendesha ushirika kama vile AMCOS, SACCOS na vikundi vidogo vya ushirika ili uweze kuwanufaisha wanaushirika wenyewe. Kwa msimu huu wa mavuno, mazao ya wanaushirika yataendelea kuuzwa na wanaushirika wenyewe kupitia minada chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao yanayozalishwa kwa wingi. Mfumo wa TMX utatumika kutafuta masoko ya nje ya nchi lakini ni mpaka elimu ya kutosha itakapotolewa. Tuwaache wanaushirika wasimamie mauzo ya mazao yao.

Sekta Ndogo ya Mafuta ya Kula

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imekabiliwa na changamoto ya uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kutosha ya kula. Hali hiyo, imetokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya mbegu ikiwemo nazi, alizeti, pamba, chikichi na mengineyo. Kwa mfano, mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni zaidi ya tani 570,000 wakati uzalishaji wa ndani ukikadiriwa kuwa tani 210,000. Katika kukabiliana na upungufu huo Serikali imekuwa ikitumia takriban shilingi bilioni 470 kuagiza tani 360,000 za mafuta ya kula kila mwaka kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekekeza mikakati ya kufufua zao la chikichi ambalo limeonekana kuwa na ufanisi mkubwa katika uzalishaji wa mafuta ya kula. Mikakati hiyo inakwenda sambamba na kuimarisha uzalishaji kwenye mazao mengine ya mbegu ikiwemo alizeti, nazi na pamba ili kupata mafuta mengi na kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na sekta binafsi itaimarisha shughuli za utafiti hususan kwenye uzalishaji wa mbegu na miche bora sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kupata mbegu nyingi zaidi.

Mifugo

Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa Rais wa tano akizungumzia eneo la mifugo kwenye hotuba yake ya kuzindua Bunge la 12 tarehe 13 Novemba 2020, alisema kuwa “Mifugo ni Utajiri”. Hata hivyo, licha ya nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya mifugo, bado mchango wa sekta hiyo katika kuboresha maisha ya wafugaji na ukuaji wa uchumi si wa kuridhisha.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 sekta ya mifugo ilichangia Pato la Taifa kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2018/2019. Ongezeko hilo, limechangiwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mnyororo mzima wa thamani kwenye sekta ya mifugo. Hatua hizo, zinajumuisha kuimarisha biashara ya ndani kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, kuboreshwa kwa mbari au kosaafu za mifugo na hivyo, kuongeza uzalishaji wa nyama bora na maziwa mengi.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2021 uzalishaji wa nyama umeongezeka kufikia tani 738,166 kutoka tani 701,679 mwaka 2019/2020. Aidha, uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo umesaidia kuimarisha biashara ya mazao ya mifugo ndani na nje ya nchi. Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 692.36 zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.30 mwaka 2019/2020 hadi tani 2,154 zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.65 mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kumekuwepo na ongezeko la viwanda vya ngozi nchini vikiwemo, kiwanda cha ngozi cha ACE Leather, Morogoro na Kiwanda cha Kimataifa cha Ngozi (Kilimanjaro International Leather Industry Co. Ltd). Viwanda hivyo, vimechangia kuongeza thamani ya ngozi inayozalishwa nchini sambamba na kutengeneza ajira. Uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata ngozi, utaongeza uzalishaji wa ngozi kutoka futi za mraba milioni 9 hadi futi za mraba milioni 25.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuhamasisha ufugaji wa kisasa na kuhimiza uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo ili kuhakikisha Taifa linanufaika na idadi kubwa ya mifugo iliyopo nchini. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji, malisho na vyakula vya mifugo sambamba na kuboresha vyuo vya mafunzo ya mifugo.

Uvuvi

Kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua madhubuti katika kukuza sekta ya uvuvi kwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo. Hatua hizo, zinatokana na ukweli kwamba sekta ya uvuvi inao uwezo wa kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa, kupambana na umaskini na tatizo la ajira.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Serikali imeanza kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Corporation - TAFICO) ikiwa ni pamoja na taratibu za ujenzi wa meli na bandari ya uvuvi. Aidha, tayari upembuzi yakinifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa bandari na Mpango wa Biashara wa kulifufua Shirika hilo umekamilika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Serikali itakamilisha ufufuaji wa Shirika la Uvuvi Tanzania na kuendelea na taratibu za ujenzi wa bandari na meli za uvuvi. Lengo ni kuimarisha shughuli za uvuvi wa bahari kuu ili kujitosheleza kwa mahitaji ya samaki na kuwezesha mauzo ya bidhaa za uvuvi nje ya nchi na hivyo kuchangia katika kuongeza mapato yatokanayo na mauzo nje, ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira.

Utalii

Mheshimiwa Spika, utalii ni miongoni mwa sekta za kiuchumi ambazo zilikumbwa na changamoto za ukuaji mzuri katika kipindi cha mwaka 2020/2021 kutokana na janga la Homa Kali ya Mapafu lililoikumba dunia kuanzia mwishoni mwa mwaka 2019. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani katika kujikinga na janga hilo ikiwemo kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege na kuwafungia watu ndani zilichangia kutokukua vizuri kwa sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho Serikali ilichukua hatua madhubuti za kunusuru sekta ya utalii ikiwemo kuandaa miongozo na taratibu maalum za kuendesha biashara ya utalii kwa kuzingatia taarifa na maelekezo ya mashirika ya kikanda na kimataifa. Hatua hizo, ziliwezesha Tanzania kupewa utambulisho wa usalama katika safari (Safe Travels Stamp) mwezi Agosti, 2020 kutoka Shirika la World Travel and Tourism Council (WTTC). Utambulisho huo ulikuwa ni kielelezo kwamba Tanzania ni sehemu salama kwa utalii dhidi ya janga la COVID-19.

Mheshimiwa Spika, hatua hizo zilichangia kuimarika kwa sekta ya utalii kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 ambapo idadi ya watalii waliotembelea Tanzania ni 624,096 ikilinganishwa na idadi ya watalii 437,000 ambao walitarajiwa kutembelea Tanzania katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, Tanzania pia imeendelea kufahamika zaidi katika masoko makuu ya utalii duniani kama kituo muhimu cha utalii barani Afrika. Kutokana na jitihada za utangazaji, mtandao wa safaribookings.com umeendelea kuitambua Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa kivutio cha utalii kinachofaa zaidi kutembelewa miongoni mwa hifadhi 50 barani Afrika mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kuimarisha usalama wa watalii wanaoingia nchini. Aidha, Serikali itaongeza kasi zaidi ya kutangaza vivutio vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na maeneo mengine ya kihistoria ndani na nje kwa kutumia balozi zetu, tovuti na sekta ya michezo.

Madini

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha sekta ya madini ili Taifa liweze kunufaika zaidi na rasilimali hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha masoko ya madini, kuzuia utoroshaji wa madini na kufanikisha uwekezaji wa kimkakati katika madini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizo, katika mwaka 2019 sekta ya madini imekua kwa asilimia 17.7 na kuongoza kwenye mauzo ya bidhaa nje ya nchi na uingizaji wa mapato ya Serikali. Hadi kufikia Februari 2021, kiasi cha shilingi bilioni 399.33 zilikusanywa sawa na asilimia 72.91 ya lengo la shilingi bilioni 547.74 kwa mwaka.

Uendelezaji Wachimbaji Wadogo

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini, Serikali imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo, kuwajengea uwezo na kuwapatia leseni za uchimbaji wa madini. Katika mwaka 2020/2021 jumla ya leseni 4,652 za utafutaji wa madini, uchimbaji mdogo na uchimbaji wa kati, uchenjuaji na uyeyushaji wa madini na leseni za biashara ya madini zimetolewa.

Mheshimiwa Spika, moja ya matokeo mazuri ya uwezeshaji wa wachimbaji wadogo ni kupatikana kwa mawe ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Bwana Saniniu Kurian Laizer. Mawe hayo yenye uzito wa kilo 9.27, 5.103 na 6.33 na thamani ya shilingi bilioni 12.59 yalivunja rekodi ya uzito wa madini ya Tanzanite yaliyowahi kupatikana nchini.

Usimamizi wa Masoko ya Madini

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini. Masoko ya madini yameongezeka kutoka 28 hadi 39 na vituo vya ununuzi wa madini vimeongezeka kutoka 28 hadi 41 katika kipindi cha Januari 2020 hadi Februari 2021. Masoko na vituo vya ununuzi wa madini vimekuwa chachu ya kuongeza ushindani na uwazi kwenye biashara ya madini, kudhibiti utoroshaji wa madini pamoja na kuwahakikishia ulinzi na usalama wa kutosha wanunuzi na wauzaji wa madini. Hatua hiyo, imewezesha kuinua uchumi wa wachimbaji wadogo na kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kwa kuwatengea na kuwapimia maeneo maalumu ya uchimbaji, kuwapatia leseni na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rahisi na rafiki ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha na kusimamia utendaji kazi wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuliongezea Taifa mapato.

Nishati

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme, mafuta na gesi imeendelea kuwa nzuri na hivyo, kutoathiri shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika mwaka 2020/2021, Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya umeme, mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Mwalimu Julius Nyerere, Mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo pamoja na ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta kutoka Hoima - Uganda hadi Chongoleani - Tanzania.

Mheshimiwa Spika, miradi hiyo mikubwa na ya kimkakati inalenga kuliwezesha Taifa kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa gharama nafuu na uhakika kwa ajili ya kujenga uchumi shindani wa viwanda. Utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 wenye thamani ya trilioni 6.55 umefikia asilimia 45 mwezi Machi, 2021. Vilevile, ajira zaidi ya 7,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zimetolewa katika mradi huo. Aidha, mradi wa uzalishaji wa umeme wa Rusumo wa megawati 80 katika maporomoko ya maji ya Mto Kagera umefikia asilimia 75.3. Kukamilika kwa miradi hiyo, kutaihakikishia nchi yetu upatikanaji wa umeme wa uhakika, wenye kutosheleza mahitaji ya viwanda na uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme unakwenda sambamba na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme ikiwemo njia ya Msongo wa kV 400 kutoka Rufiji - Chalinze - Kinyerezi na Chalinze - Dodoma na njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kwa ajili ya treni ya mwendo kasi. Nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kwa ajili ya treni ya mwendo kasi (Dar es Salaam - Morogoro) imekamilika kwa asilimia 99.

Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Septemba 2020 Mheshimiwa Yoweri Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda alizuru Tanzania. Ziara hiyo ililenga kukamilisha taratibu za mwisho za utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania. Mradi huo, utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 unatarajiwa kutengeneza ajira zipatazo 18,000. Tarehe 11 Aprili, 2021 Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki katika utiaji saini wa Mkataba wa Utekelezaji nchini Uganda na hivyo kuashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi huo. Rai yangu kwa wananchi ni kujiandaa kuzitumia kikamilifu fursa zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) ili kuhakikisha kuwa vijiji 1,974 vilivyosalia vinapata huduma ya umeme. Kadhalika, Serikali itasimamia miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme, sambamba na utekelezaji wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania.

Viwanda, Biashara na Masoko

Mheshimiwa Spika; Serikali inaimarisha sekta ya viwanda ili kutengeneza ajira nyingi zaidi, kuongeza thamani ya mazao, kupanua wigo wa masoko na hivyo, kuongeza pato la mtu mmoja mmoja, mapato ya Serikali na fedha za kigeni. Katika mwaka 2019 sekta ya viwanda ilichangia asilimia 8.5 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 8.1 mwaka 2018 katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Katika kuongeza mchango wa sekta hii, Serikali inasimamia azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini kwa kuimarisha ulinzi wa viwanda vya ndani, kuendeleza viwanda mama, viwanda vya kimkakati sambamba na kuhakikisha matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa ujenzi wa uchumi wa viwanda umewezesha kuongezeka kwa kasi ya ujenzi wa viwanda vipya kila mwaka, upanuzi wa viwanda vilivyopo pamoja na ufufuaji wa viwanda vilivyokufa. Baadhi ya viwanda vilivyojengwa katika mwaka 2020 ni, Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd katika Mkoa wa Kilimanjaro, kiwanda cha usindikaji maziwa cha Kahama Fresh kilichopo katika Mkoa wa Shinyanga, Taifa Leather Company Ltd, Murzar Wilmar Rice Mills Ltd na Mahashree Agro-processing Tanzania Ltd vilivyopo Morogoro.

Mheshimiwa Spika, vilevile, ujenzi wa majengo ya viwanda (Industrial Sheds) kwa ajili ya wajasiriamali katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Geita, Mtwara na Ruvuma; kiwanda cha chai cha Kabambe (Njombe); kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd kinachobangua korosho (Mikindani - Mtwara); na jengo la kiwanda kipya cha kuunganisha matrekta TAMCO - Kibaha umekamilika. Ujenzi wa majengo hayo pamoja na kuimarisha uwekezaji kwa wajasiriamali, utasaidia kuimarisha shughuli za viwanda na hivyo kuongeza ajira na masoko ya bidhaa zinazozalishwa.

Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya umeongeza mahitaji ya vifaa tiba, kinga na dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika kukabiliana na ongezeko la mahitaji hayo, mwaka 2020/2021 katika kipindi kifupi Serikali ilifanikiwa kuhamasisha uwekezaji mkubwa ambapo viwanda 17 vya dawa, vifaa tiba na kinga vilianzishwa. Kuanzishwa kwa viwanda hivyo, kutawezesha kuimarika kwa huduma za afya nchini kufuatia upatikanaji wa kutosha wa bidhaa hizo, usalama wake, kuongeza ajira na kuondokana na utegemezi kutoka nje.

Masoko

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto za ukuaji wa viwanda na biashara nchini ni upatikanaji wa masoko ya uhakika. Katika mwaka 2020/2021, Serikali imefanikiwa kupata masoko ya bidhaa zetu nje kwa lengo la kukuza uchumi na pato la Taifa. Mafanikio hayo, yanajumuisha kusainiwa kwa mkataba kati ya Tanzania na China Oktoba, 2020 ili kuruhusu maharage aina ya soya kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.

Mheshimiwa Spika, mwezi Januari, 2021 Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye samaki unaojulikana kama Fish4ACP. Mradi huo, unaohusisha nchi 10 kati ya 79 za Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibeani na Pasifiki (OACPS) utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano mkoani Kigoma. Kupitia mradi huo, wavuvi wadogo watapatiwa ujuzi wa kuongeza uzalishaji na mnyororo wa thamani kwenye samaki aina ya migebuka na dagaa.

Mheshimiwa Spika, masoko mengine yaliyopatikana ni soko la minofu ya samaki aina ya sangara nchini Saudi Arabia, soko la nyama katika nchi za Kuwait, Qatar na Oman na soko la matunda aina ya karakara (passion), parachichi pamoja na nanasi katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Katika kipindi hicho, zaidi ya tani 7,000 za nyama na kontena 22 za matunda ziliuzwa katika masoko hayo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itapanua wigo wa masoko ya bidhaa zetu nje ili kutoa fursa nzuri zaidi za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara, kuwapa uhakika wa kipato na kukuza uchumi na pato la Taifa. Natoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo, Viwanda na Biashara kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kutafuta fursa zitakazowezesha bidhaa zinazozalishwa nchini kuongezwa thamani hususan mazao ya kilimo, pamoja na kuwaunganisha wakulima na wenye viwanda ili kupata masoko ya uhakika nje ya nchi.

HUDUMA ZA KIUCHUMI

Ardhi

Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa uchumi na maendeleo ya watu kumechangia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zimeibua migogoro ya matumizi ya ardhi. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/2021 Serikali imesimamia mikakati mbalimbali yenye lengo la kuondoa migogoro ya ardhi na kuhakikisha uwepo wa mipango na matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji, kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Julai, 2020 Serikali iliridhia vijiji 920 kati ya 975 vyenye migogoro kubaki katika maeneo ya mikoa na kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii. Vilevile, Serikali imeridhia vijiji 19 kati ya 55 vilivyokuwa na migogoro na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zinahusisha kufutwa kwa mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na misitu ya hifadhi 7 yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili kuruhusu wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Aidha, migogoro mingine ya ardhi ipatayo 23,783 imetatuliwa kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Kwa kuzingatia hatua ambazo Serikali imezichukua, naelekeza viongozi wote wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali na kuhakikisha kuwa hakuna migogoro mipya ya ardhi inayojitokeza katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Januari 2021 viwanja 95,329 vimetambuliwa, kupimwa na kumilikishwa kwa kutumia dhana shirikishi katika upangaji na upimaji wa ardhi. Hatua hiyo, ni utekelezaji wa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. Vilevile, ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,885.40 imetengwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itatekeleza mipango na programu za upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi katika maeneo ya wananchi pamoja na miradi ya kimkakati ya kitaifa, uimarishaji wa muindombinu ya upimaji na ramani na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo kwa pamoja itapunguza migogoro ya ardhi nchini.

Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ni hatua muhimu katika kukuza uchumi na sekta za uzalishaji. Katika mwaka 2020/2021 Serikali imejenga, kukarabati na kufanyia matengenezo barabara, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege na reli.

Barabara na Madaraja

Mheshimiwa Spika, hadi Februari, 2021 Serikali imejenga na kukarabati km. 401.60 ikilinganishwa na lengo la km. 520.47 sawa na asilimia 77.16 kwa mwaka 2020/2021. Ujenzi na ukarabati huo ulihusisha barabara kuu, za mikoa na wilaya ili kuziwezesha zipitike wakati wote. Lengo la Serikali ni kuhakikisha mikoa na wilaya zote nchini zinaunganishwa kwa barabara za lami. Aidha, kazi ya kuunganisha mikoa ya Rukwa - Katavi, Katavi - Tabora, Singida - Tabora, Tabora - Kigoma na Kigoma - Kagera inaendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha tunapunguza msongamano wa magari mkoani Dar es Salaam, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya juu ya John Kijazi, iliyozinduliwa tarehe 24 Februari, 2021. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa km. 19 ambao ujenzi wake umefikia asilimia 62.32. Vilevile, Serikali inajenga barabara za juu katika eneo la Keko, Chang’ombe na Uhasibu, Kurasini ili kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine ya ujenzi wa madaraja makubwa ambayo ni pamoja na Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2 uliofikia asilimia 25.71, Tanzanite lenye urefu wa kilomita 1.03 uliofikia asilimia 70.6 na Wami lenye urefu wa mita 513.5 uliofikia asilimia 42. Aidha, ujenzi wa madaraja mengine upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Anga

Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo utalii, kilimo na madini. Miradi inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Geita ambao umefikia asilimia 98, Songea asilimia 95 na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mtwara ambao umefikia asilimia 53.2. Aidha, maandalizi ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato utakaogharimu shilingi bilioni 759 yamekamilika. Vilevile, ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vitakavyogharimu shilingi bilioni 136.85 unaendelea.

Mheshimiwa Spika, sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri wa anga, Serikali imekamilisha malipo ya ununuzi wa ndege mpya tatu, mbili zikiwa ni Airbus A220-300 na moja ni Dash 8-Q400 De-Havilland. Ndege hizo zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/2022 na hivyo kuwezesha Serikali kuwa na jumla ya ndege 12. Nitumie fursa hii kulipongeza Shirika la Ndege Tanzania kwa kuanzisha safari za kwenda Guangzhou, China. Safari hizo, zitakuwa chachu ya kuimarisha biashara, utalii na ajira.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja, viwanja vya ndege, nyumba na majengo ya Serikali. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya vivuko katika maeneo mbalimbali nchini inayohusisha ujenzi wa maegesho ya vivuko, ukarabati na ujenzi wa vivuko vipya.

Reli

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye jumla ya urefu wa km. 1,219 unaendelea kwa awamu. Ujenzi wa kipande kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km. 300) umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.34 na ujenzi wa kipande cha Morogoro hadi Makutupora (km. 422) umekamilika kwa asilimia 57.57. Vilevile, Serikali imesaini mkataba na mkarandasi ili kukamilisha kipande cha Mwanza hadi Isaka (km. 341).

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha taratibu za manunuzi ya vichwa vya treni na mabehewa ya mizigo na ya abiria. Kuboreshwa kwa miundombinu ya reli kutarahisisha usafirishaji wa mizigo ya ndani na nchi jirani, kuboresha utendaji wa bandari ya Dar es Salaam na kuimarisha uchumi wa wananchi. Hii ni hatua kubwa kwa Taifa letu kwani kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa na treni inayoendeshwa kwa kutumia umeme.

Bandari

Mheshimiwa Spika, Serikali inaboresha bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. Uboreshaji wa gati Na. 6 na 7 katika Bandari ya Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 90 na 75 mtawalia. Kwa upande wa Bandari ya Tanga kazi ya kuchimba lango la kuingia meli lenye urefu wa km. 1.75 imekamilika na linatumika na ujenzi wa sehemu ya kugeuzia meli yenye upana wa mita 400 unaendelea. Aidha, ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300, ukarabati wa yadi ya kuhudumia shehena na ghala namba 3 katika Bandari ya Mtwara umekamilika. Miradi hiyo itawezesha Taifa kutumia kwa ufanisi fursa za kijiografia tulizonazo pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itakamilisha miradi iliyoanzishwa na kuanza utekelezaji wa miradi mipya.

Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mheshimiwa Spika, dunia hivi sasa ipo katika mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanaongozwa na sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari. Kama zilivyo nchi nyingine duniani, nasi ni lazima kuendana na mabadiliko haya. Hivyo basi, katika miaka mitano ijayo, Serikali itafikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu hususan wilayani, kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (Broadband) na kuongeza watumiaji wa internet.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali imesimamia utekelezaji wa Mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi, Mkakati wa Kitaifa wa Usalama wa Mitandao (National Cyber Security Strategy), ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kuweka miundombinu ya Mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi inaendelea na jumla ya kata 118 katika Halmashauri za Majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, na Tanga na Manispaa ya Morogoro zimefikiwa. Vilevile, Mkakati wa kukamilisha Mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi kwa maeneo yote nchini ifikapo 2025 umeandaliwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaongeza matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya kasi (Broadband) kutoka asilimia 45 ya mwaka 2020 hadi asilimia 60 kwa mwaka 2022, kuimarisha huduma za Posta ikiwemo biashara mtandao (e-Commerce) ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa na huduma ndani na nje ya nchi sambamba na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa na huduma kwa wananchi na kuendeleza ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufikisha huduma ya Mkongo kwa ngazi za Wilaya.

HUDUMA ZA JAMII

Elimu

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali imetekeleza mpango wa Elimumsingi Bila Ada pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu nchini. Hadi kufikia Februari 2021, Serikali imetumia shilingi bilioni 166.17 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo kwa ajili ya shule za msingi na sekondari. Pia, Serikali imeboresha miundombinu ya Shule za Msingi 1,372 na Sekondari 554 kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, imekarabati shule 18 za wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 142,179. Shilingi bilioni 464 zitatumika kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ukilinganisha na shilingi bilioni 450 zilizotumika kwa wanafunzi 130,883 mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kuinua kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa kuimarisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini; kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wakufunzi pamoja na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Maji

Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia vizuri sekta ya maji na kuhakikisha inatoa mchango unaostahili katika kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu. Katika mwaka 2020/2021, Serikali ilipanga kutekeleza miradi 1,346 katika maeneo ya mijini na vijijini. Hadi Februari, 2021 miradi ya maji iliyokamilika ni 422 ambayo imegharimu shilingi bilioni 913.74. Kati ya miradi hiyo, 355 ipo vijijini na 67 ipo mijini. Halikadhalika, utekelezaji wa miradi 924 iliyobaki unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, miradi mikubwa iliyokamilika ni pamoja na mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega na mradi wa kupeleka maji katika miji ya Kagongwa na Isaka. Kukamilika kwa miradi hiyo, kumewanufaisha wananchi wapatao milioni 3.52 wa mijini na vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaweka kipaumbele katika kukamilisha miradi 924 inayoendelea kutekelezwa, kuanza utekelezaji wa miradi mipya ikiwemo miradi katika miji 28, kuboresha huduma ya maji jijini Dodoma kwa kujenga bwawa la Farkwa na mradi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya kipaumbele katika kipindi hicho ni mradi wa maji na usafi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam, mradi wa maji wa Orkesumet, mradi wa maji wa mji wa Mugango - Kiabakari - Butiama, mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda miji ya Tinde na Shelui, mradi wa maji wa Same - Mwanga, mradi wa majisafi na usafi wa mazingira katika Jiji la Arusha na mradi wa maji katika Jiji la Mwanza. Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ili ilete tija katika uchumi wa Taifa.

Afya

Mheshimiwa Spika, kulinda na kuimarisha afya ya Watanzania imeendelea kuwa ni kipaumbele cha Serikali. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imejenga na kuboresha miundombinu ya afya, huduma za kibingwa, upatikanaji wa vifaa tiba, kinga, dawa na vitendanishi.

Miundombinu ya Huduma za Afya

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali maalumu umefikia hatua mbalimbali za ukamilishwaji kama ifuatavyo: Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Njombe (asilimia 80), Simiyu (asilimia 70), Mara -Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (asilimia 74), Geita (asilimia 94), Songwe (asilimia 80), Katavi (asilimia 65), Mwanza-Sekou Toure (asilimia 73), Dar es Salaam - Mwananyamala (asilimia 98), Ruvuma (asilimia 45), Tanga (asilimia 75), Kigoma - Maweni (asilimia 75), Kilimanjaro - Mawenzi (asilimia 65), na Hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino, Dodoma imekamilika.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Hospitali tatu za Rufaa za Kanda ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini - Mtwara (asilimia 90), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini - Mbeya (asilimia 72) na Kanda ya Ziwa - Burigi (awamu ya kwanza asilimia 98) unaendelea. Vilevile, Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya uchunguzi kwa njia ya maabara katika Hospitali ya magonjwa ambukizi ya Kibong’oto - Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa hospitali za Halmashauri 102, vituo vya afya 487 na ujenzi wa zahanati 1,198. Hadi Machi 2021, hospitali 57 za Halmashauri, vituo vya afya 296, na zahanati 654 zimekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mapambano Dhidi ya Magonjwa ya Mlipuko Ikiwemo Homa Kali ya Mapafu

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupambana na Magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza, mwezi Februari 2021, Serikali imeingiza nchini mitambo saba yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya oksijeni kwa siku. Mitambo hiyo itasimikwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa ya Amana, Dodoma, Geita, Manyara, Mbeya, Mtwara na Ruvuma. Sambamba na usimikaji wa mitambo hiyo, hospitali zote saba zimepatiwa mitungi 74 kila moja.

Mheshimiwa Spika, kila mtambo mmoja kwenye hospitali hizo utakuwa na uwezo wa kusambaza gesi ya oksijeni katika vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 18. Hatua hiyo, inalenga kuimarisha mfumo wa huduma za afya ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto za sasa na baadaye. Maeneo yanayolengwa ni vyumba vya kutoa huduma za dharura, huduma ya mama na mtoto, upasuaji na vyumba vya uangalizi maalum. Katika mwaka 2021/2022, Serikali itaongeza mitambo mingine ya aina hiyo 12.

Huduma za Afya za Kibingwa

Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za afya za kibingwa na kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hizo ndani ya nchi na hivyo kuokoa fedha zilizokuwa zitumike kugharamia huduma hizo nje ya nchi. Katika mwaka 2020/2021 wagonjwa 62 wamepandikizwa figo katika hospitali ya Taifa Muhimbili na wagonjwa 16 katika hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma. Aidha, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa huduma za upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua kwa wagonjwa 114. Vilevile, watu wazima 36 walifanyiwa upasuaji uliohusisha mishipa ya damu.

Hali ya Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba

Mheshimiwa Spika, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya unaoendelea kote nchini, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo hivyo umeendelea kuimarika. Hadi Machi 2021, shilingi bilioni 74.38 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15 ni za ununuzi wa chanjo.

ULINZI NA USALAMA

Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama katika nchi na mipaka yetu imeendelea kuwa shwari. Vilevile, Jeshi la Wananchi Tanzania linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mamlaka za kiraia na mataifa mengine kupambana na matishio ya kiusalama yakiwemo ugaidi, uharamia, uhamiaji haramu, biashara haramu ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.

Mheshimiwa Spika, jeshi letu limeendelea kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na mradi wa kufua umeme Rufiji (Julius Nyerere Hydropower Project) pamoja na kutoa huduma wakati wa majanga na matukio yenye kuleta athari kwa watu na mali zao.

Mheshimiwa Spika, jeshi letu linashiriki katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Darfur, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati na Lebanon. Lengo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kuimarisha amani na masilahi ya Taifa katika Nyanja za Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuliimarisha na kuliongezea uwezo JWTZ kwa kulipatia vifaa na zana bora za kisasa pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa wanajeshi ikiwemo mafunzo, maslahi, huduma bora za afya na makazi ili kuongeza uwezo wake wa kiutendaji na utayari wa kulinda mipaka ya nchi.

KAZI NA WAFANYAKAZI

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi na wafanyakazi kwa kusimamia viwango vya kazi na wafanyakazi pamoja na afya na usalama mahali pa kazi. Hadi Februari, 2021 jumla ya kaguzi 4,771 za viwango vya kazi zimefanyika sawa na asilimia 99.4 ya kaguzi 4,800 zilizopangwa kufanyika. Aidha, kaguzi 110,123 zilizohusu afya na usalama mahala pa kazi zimefanyika. Kufuatia kaguzi hizo, waajiri 1,162 walichukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi na kutoa elimu na ushauri kwa wafanyakazi, waajiri na vyama vyao. Lengo ni kuelekeza namna bora ya kutekeleza Sheria hizo; kuimarisha majadiliano ya pamoja baina ya waajiri na wafanyakazi pamoja na Serikali na pia ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maeneo ya kazi kupitia Mabaraza ya Wafanyakazi ili kuongeza uzalishaji na tija, sambamba na kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Aidha, itashughulikia maombi ya vibali vya kazi na maombi ya msamaha kwa raia wa kigeni wanaoomba kufanya kazi nchini.

HIFADHI YA JAMII

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 gharama za uendeshaji wa Mifuko ya Pensheni ziliendelea kupungua kutoka asilimia 6.8 mwaka 2019/2020 mpaka kufikia asilimia 5.4 Desemba, 2020. Sambamba na kushuka kwa gharama za uendeshaji, Mifuko ya Pensheni imeendelea kulipa mafao kwa wastaafu. Hadi kufikia Machi 2021 jumla ya wanachama 203,418 walilipwa mafao ya pensheni ya jumla ya shilingi bilioni 1,361.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais ili kuwezesha kupata kanuni za ulipaji wa mafao ambazo zitakidhi matarajio ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma na Binafsi na kuhakikisha Mifuko inakuwa endelevu. Pili, Serikali itaendelea kuisimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha Sera ya Kinga ya Jamii inakamilika. Aidha, Ofisi yangu itaendelea kutekeleza majukumu yote yaliyoainishwa katika Sheria ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha Taasisi zote za Hifadhi ya Jamii zinafuata Kanuni na Miongozo iliyopo ili kupunguza kero kwa wananchi wanaowahudumia.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha usimamizi wa mabenki, mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji katika kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi kwa kupatiwa mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri zetu. Lengo ni kuhakikisha Watanzania wengi wanajihusisha na shughuli za kiuchumi ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Serikali inaendelea na mapitio na tathmini ya mifuko ya uwezeshaji wananchi ili kuwezesha kuunganisha mifuko hiyo na hivyo kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija kubwa kwa wananchi. Katika kipindi hicho, hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa ajili ya kuwapa fursa wananchi wengi kufahamu kuhusu uwepo wa mifuko na programu hizo na fursa zinazopatikana.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza malengo hayo, mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilifanya maonesho ya wiki moja kuanzia tarehe 7 hadi 13 Februari, 2021 kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Arusha. Maonesho hayo, yamewapatia fursa Watanzania kufahamu kwa undani mifuko na programu zilizopo, majukumu yake na fursa za uwezeshaji zinazopatikana.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 mifuko na programu za uwezeshaji zimetoa mitaji ya masharti rafiki yenye thamani ya shilingi bilioni 898.12 kwa wajasiriamali 3,614,857. Mitaji hiyo, imewanufaisha wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uchumi zilizo katika sekta mbalimbali kama vile viwanda, afya, elimu, biashara, madini, uvuvi, ufugaji, kilimo na miundombinu.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari, 2021 shilingi bilioni 22.3 zimetolewa kwa vijana (asilimia 4), wanawake (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2) ikiwa ni mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Ninaendelea kusisitiza halmashauri zote nchini kuzingatia matakwa hayo ya kisheria ya kutenga fedha zinazotokana na mapato ya ndani na kuhakikisha fedha hizo zinatolewa na kutumika kama ilivyokusudiwa kwa makundi hayo.

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuwezesha wananchi kiuchumi, Serikali imetekeleza miradi ya kimkakati yenye kuhusisha masoko na vituo vya basi. Miradi hiyo, sambamba na kuimarisha mapato ya ndani ya halmashauri husika imelenga kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi hususan wanaozunguka maeneo hayo. Miongoni mwa miradi iliyokamilika ni kituo cha mabasi cha Magufuli cha Mbezi Luis, kilichopo Dar es Salaam na Soko la Chifu Kingalu lililopo Manispaa ya Morogoro.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ni soko la Kagunga (Kigoma), Muhange (Kakonko), ghala la mazao (Ruangwa) na soko la Kisutu (Dar es Salaam). Miradi mingine 33 ya namna hiyo inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na hivyo kujiongezea kipato, kuboresha huduma katika maeneo husika na kuimarisha mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2021/2022 ni kukamilisha zoezi la tathmini na kuiunganisha mifuko na programu za uwezeshaji ili kuleta ufanisi na tija iliyokusudiwa. Kadhalika, Serikali itahakikisha asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri inawafikia walengwa na kusimamia miradi ya kimkakati inayotekelezwa ili thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali ionekane.

Ukuzaji wa Fursa za Ajira na Ujuzi

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Serikali imechukua hatua za makusudi hususan utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, sambamba na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania. Hadi kufikia Februari, 2021 ajira 594,998 zimezalishwa katika sekta mbalimbali. Kati ya hizo, ajira 314,057 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ajira za Serikali. Vilevile, ajira 280,941 zimezalishwa kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 18,956 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kati ya hao, vijana 5,538 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi ambapo waanufaika 77 ni watu wenye ulemavu. Aidha, vijana 10,178 wamepewa mafunzo ya kurasimishiwa ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi wa mafunzo ambapo kati ya wanufaika hao 28 ni watu wenye ulemavu. Vilevile, vijana 3,240 wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu kazini (Internship) katika taasisi binafsi na za umma ambapo kati yao wahitimu 92 ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala ya ukuzaji ajira na kazi za staha katika Sera, Mikakati na Mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahiki pamoja na kuongeza fursa za ajira.

MASUALA MTAMBUKA

Uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba - Dodoma

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba yatakayotosheleza watumishi wote. Katika mwaka 2020/2021, Serikali imekamilisha usanifu wa majengo husika. Aidha, mradi wa ujenzi wa barabara (km. 51.2) kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikali umefikia asilimia 71.

Mapambano Dhidi ya UKIMWI

Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi za Serikali na wadau mbalimbali hali ya maambukizi ya UKIMWI imepungua. Hadi kufikia Desemba 2019, inakadiriwa kuwa Watanzania milioni 1.7 wanaishi na VVU. Aidha, takwimu zinaonesha kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi watu 77,000 mwaka 2019. Halikadhalika, vifo vimepungua kutoka 52,000 mwaka 2010 hadi kufikia vifo 27,000 mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika, kufuatia maambukizi hayo, Serikali imeimarisha huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za ARV na afua za kinga zinazotekelezwa na wadau mbalimbali nchini. Hadi Desemba, 2020 zaidi ya watu milioni 1.36 walikuwa wanapata huduma za dawa za ARV. Aidha, juhudi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kutoa afua za mabadiliko ya tabia, tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha vijana wengi ndio wanaathrika na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Hivyo, napenda kusisitiza kuwa kampeni za mawasiliano ya mabadiliko ya tabia kwa vijana ni lazima ziwe endelevu kupitia njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Pia niendelee kuitaka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania iendelee kufanya kazi na majukwaa ya wasanii ili kuwafikia vijana wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kufanya jitihada za kupunguza kasi ya maambukizi mapya na vifo vinavyotokana na UKIMWI katika jamii kwa kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali muhimu kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI. Aidha, itapunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuimarisha huduma za elimu ya UKIMWI.

Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupambana na dawa za kulevya ambapo katika kipindi cha Julai 2020 hadi Februari 2021 watuhumiwa wa dawa za kulevya 5,374 walikamatwa. Katika kipindi hicho, kilogramu 67.2 za heroin na kilogramu 1.96 za cocaine pamoja na tani 12.8 za bangi, tani 6.1 za mirungi na tani 57.6 za kemikali bashirifu zilikamatwa. Aidha, mashamba ya bangi 39 yenye jumla ya ekari 49 yaliteketezwa kote nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusogeza huduma karibu na wananchi, Serikali imefungua Ofisi mbili za Kanda za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika mikoa ya Mtwara na Mwanza. Kwa upande mwingine, Serikali imeongeza vituo vya kutolea huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka vituo sita mwaka 2019/2020 hadi kufikia vituo tisa vinavyohudumia waathirika wapatao 10,565.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini, kutoa elimu kwa umma juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kudumisha ushirikiano na nchi nyingine katika kupambana na dawa za kulevya na kuendelea na upanuzi wa tiba ya methadone katika vituo vingine vitakavyoanzishwa.

Maafa

Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha uwezo wa usimamizi wa maafa nchini ili kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga. Katika mwaka 2020/2021, Serikali imewezesha upatikanaji wa vifaa vya huduma za kibinadamu na hivyo kuongeza utayari wa kukabiliana na maafa. Sambamba na kutoa elimu kwa umma na Kamati za Usimamizi wa Maafa za mikoa, Serikali imekamilisha taratibu za kumiliki eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022 Serikali itaanza ujenzi wa kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa, kuimarisha uwezo wa usimamizi wa maafa nchini na kuchukua hatua stahiki katika kuzuia, kupunguza, kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Mazingira

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia matumizi ya rasilimali na maliasili ili kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kuwa na mazingira endelevu. Lengo ni kuhifadhi mazingira, kupambana na uharibifu wa mazingira na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali imefuatilia utekelezaji wa kanuni za udhibiti wa taka hatarishi za mwaka 2019 pamoja na kusimamia utekelezaji wa kanuni za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini za mwaka 2019. Lengo la Serikali ni kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala pamoja na vifungashio vya plastiki vinayokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imetekeleza miradi na shughuli wezeshi mbalimbali ikiwemo Mradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Tanzania; Mradi wa kusaidia kujenga uwezo wa taasisi na jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi; Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa; Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini na Mradi wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu hifadhi ya mazingira hapa nchini. Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, ajira 729 zimetengenezwa wakati shughuli wezeshi zimezalisha ajira 1,528.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Serikali itaandaa na kutekeleza mikakati, mipangokazi na miongozo mbalimbali ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini. Aidha, itaratibu, kufuatilia na kupima utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira katika ngazi zote.

UTAWALA BORA

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha masuala ya utawala bora Bunge lako tukufu kwenye Mkutano wake wa pili mwezi Februari 2021 lilipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 wa Mwaka 2021. Sheria hiyo imefanya marekebisho katika Sheria ya Tafsiri ya Sheria (Sura ya 1), Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Sura ya 11) na Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi (Sura ya 216).

Mheshimiwa Spika, mabadiliko hayo muhimu yameweka msingi kwa lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya sheria na lugha ya Mahakama, Mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki badala ya Kiingereza kama ilivyokuwa hapo awali. Mabadiliko hayo, yanazingatia ukweli kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa, lugha ambayo inaeleweka na inatumika katika shughuli zote za kijamii na maendeleo nchini.

Mheshimiwa Spika, marekebisho hayo yataboresha mfumo wa upatikanaji haki kwa wananchi ambao ndio walengwa wa sheria husika. Vilevile, Serikali inaendelea na zoezi la kutafsiri Sheria Kuu na Sheria ndogo zote ambazo ziliandikwa kwa Kiingereza kwenda kwenye lugha ya Kiswahili. Kwa upande mwingine, Serikali itayafanyia kazi maoni na ushauri wote uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2021 ili kuhakikisha tunaendelea kuboresha mfumo wa upatikanaji haki hapa nchini. Aidha, kuanzia sasa Serikali itatayarisha na kuwasilisha katika Bunge lako tukufu miswada yote ya sheria kwa lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine la utawala bora lililoimarishwa ni mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma. Serikali ilichukua hatua ya kufungua jumla ya mashauri sita kwenye Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Mahakama Kuu na kufikisha jumla ya mashauri 21 yaliyosajiliwa katika mahakama hiyo. Hadi Februari, 2021 mashauri matano yamehitimishwa na mengine 16 yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, katika mpango na bajeti ya mwaka 2021/2022, Serikali pamoja na mambo mengine imepanga kukamilisha zoezi la kutafsiri Sheria Kuu na Sheria ndogo zote kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili na kutekeleza mipango ya kitaifa ya masuala mtambuka yanayohusu vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

MUUNGANO

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) imeendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kuulinda, kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa pande zote mbili kufurahia matunda yake.

Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Julai, 2020 kilifanyika kikao cha Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Muungano. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho ni tukio la kihistoria la kusainiwa kwa makubaliano ya kuondoa hoja tano zilizopatiwa ufumbuzi kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Mheshimiwa Spika, hoja hizo tano zinajumuisha: Ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda; ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; gharama za kushusha mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar; utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ katika kushughulikia masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa faida za kusainiwa kwa hati hizo ni kuimarisha Muungano hususan ushiriki wa nchi katika Jumuiya za Kikanda pamoja na ushirikiano katika sekta ya uchukuzi. Kwa msingi huo, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wote wa Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kwa jitihada zao kubwa katika kuhakikisha muungano wetu unaendelea kuimarika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kuimarisha uratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizopo na zitakazojitokeza kwa madhumuni ya kuuenzi, kuulinda na kuudumisha muungano wetu; Kuratibu masuala ya kiuchumi na kijamii kwa kufuatilia utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo kwa pande mbili za muungano; Kutoa elimu ya muungano kwa umma kwa makundi tofauti ya kijamii; na Kuratibu masuala yasiyo ya muungano kupitia vikao vya ushirikiano vya Wizara, Idara na Taasisi za SMT na SMZ zisizo za muungano zenye majukumu yanayoshabihiana.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuheshimu misingi ya ushirikiano na mataifa mengine duniani zikiwemo Taasisi za Kimataifa na Kikanda sambamba na kusimamia, kulinda na kutetea maslahi yake ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama huko nje. Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Serikali imeendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji, watalii na kutafuta masoko ya bidhaa zetu nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi na Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kutumia ziara za viongozi wakuu wa kitaifa kutoka nje pamoja na majukwaa ya kimataifa na kikanda katika kukuza ushirikiano kwenye nyanja za biashara, uwekezaji, masoko ya bidhaa zetu, utalii na lugha ya Kiswahili ili kuchochea maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 tuliwapokea Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda na Mheshimiwa Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.

Mheshimiwa Spika, ziara za viongozi hao zimekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi na kuimarisha ujirani mwema. Kwa mfano, ziara ya Rais wa Burundi ilikuwa chachu ya kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi tarehe 3 hadi 5 Machi, 2021 mjini Kigoma. Lengo la Mkutano huo, lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya uchukuzi, biashara, nishati, utalii, ulinzi pamoja na masuala ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, ziara ya Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda mwezi Septemba 2020, iliwezesha kujenga mazingira mazuri kuelekea utiaji saini wa mkataba wa mwisho wa utekelezaji wa ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania.

Mheshimiwa Spika, akiwa nchini Tanzania mwezi Januari 2021, Mheshimiwa Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia alieleza utayari wa nchi yake kukifanya Kiswahili kuwa moja kati ya lugha zinazozungumzwa nchini humo sambamba na kushirikiana kwenye fursa ya mafunzo katika sekta ya usafiri wa anga na uwekezaji katika sekta ya viwanda vya kuzalisha bidhaa za ngozi nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jumuiya za Kikanda, Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao Agosti 2020. Jambo la kujivunia wakati wa uenyekiti wa hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni lugha ya Kiswahili kuongezwa kuwa moja ya lugha rasmi za SADC.

Mheshimiwa Spika, masuala mengine ni kuanzishwa kwa Baraza la Biashara linalolenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza mtangamano wa Kanda; kuhamasisha uendelezaji wa viwanda kwa lengo la kukuza ajira, biashara na mapato ya Nchi Wanachama pamoja na kufanikisha kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uwezeshaji Biashara na Usafirishaji katika kipindi cha COVID-19 ambao nchi zote zimeendelea kuutekeleza kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2021/2022 kwa upande wa mahusiano ya kimataifa ni kutekeleza diplomasia ya uchumi, kudumisha na kuimarisha mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine, kushiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa na Mashirika yake, Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kikanda.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Tanzania itashiriki katika juhudi za kuleta Amani na usalama kwenye Jumuiya za Kikanda ambazo nchi yetu ni mwanachama sambamba na kulinda na kutetea misingi na maslahi ya Taifa letu ndani na nje. Wakati tunatekeleza hayo, ni matarajio yetu kuwa mataifa mengine nayo yataendelea pia kuheshimu uhuru wa nchi yetu hususan katika kujiamulia mambo yetu wenyewe.

UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Pili wa Bunge lako tukufu kupitia kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, nilitoa maelekezo kwa Balozi zetu zote kuanzisha vituo vya kujifunza Kiswahili. Hatua hiyo, inakwenda sambamba na kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani na nje kwa kutoa mafunzo ya matumizi sanifu na fasaha ya Kiswahili. Hatua nyingine ni kutoa ithibati kwa vitabu vya lugha ya kiswahili vinavyokusudiwa kutumika shuleni. Vilevile, kufanya tafsiri ya nyaraka mbalimbali na kuanzisha mafunzo ya kuimarisha stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni.

Mheshimiwa Spika, licha ya kuendelea kukua kwa sekta ya sanaa, michezo na burudani bado mchango wake katika uchumi ni mdogo. Kwa mfano, tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2019 sekta ya sanaa na burudani ilichangia asilimia 0.3 kwenye pato la Taifa. Hata hivyo, sekta hii inapata hamasa kubwa, inaajiri vijana wengi kwa sasa na imekuwa miongoni mwa sekta zinazotumika kulitangaza Taifa letu nje na wakati mwingine kuvutia utalii.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto zinazoikumba sekta ya michezo, sanaa na burudani ni eneo la kiufundi na mbinu. Hili linadhihirishwa na uwepo wa walimu wengi wa kigeni hususan kutoka baadhi ya nchi jirani kwenye mchezo wa soka. Kwa mantiki hiyo, natumia fursa hii kutoa maelekezo kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuja na mkakati wa kuendeleza wataalam wetu wa michezo, sanaa na burudani kupitia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi washirika kwenye eneo la utamaduni, michezo na sanaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka mazingira bora ya kuimarisha michezo nchini kwani faida za michezo ni nyingi ikiwemo ajira kwa vijana, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kinga na tiba kwa magonjwa yasiyoambukizwa.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza. Aidha, nimetoa mwelekeo wa kazi zitakazofanyika katika mwaka 2021/2022. Maelezo ya kina ya utekelezaji wa kisekta yatawasilishwa na Mawaziri watakapokuwa wanawasilisha bajeti zao. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza kwamba Serikali itatekeleza mambo muhimu yafuatayo:-

Mosi: Kuenzi na kuendeleza jitihada, maono, juhudi za Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan katika ulinzi wa rasilimali za Taifa, nidhamu katika matumizi ya fedha za Umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kuunganisha na kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa kitaifa.

Pili: Kutekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira. Kwa kasi tuliyoanza nayo, Serikali itaendelea kuongeza nguvu zake kuendeleza na hatimaye kukamilisha miradi hiyo;

Tatu: Kuimarisha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya;

Nne: Kuimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo;

Tano: Kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii;

Sita: Kuchukua hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, dini na ukabila waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa ili tuweze kulinda mafanikio tuliyoyapata. Jitihada hizo ndizo zimetuwezesha kuingia katika nchi za uchumi wa kati.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2021/2022

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/2022, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 116,784,244,000.00 kati ya fedha hizo, shilingi 93,303,370,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 23,480,874,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, vilevile naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 128,873,377,000.00 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 121,875,906,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na shilingi 6,997,471,000.00 ni kwa ajili ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news