Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na mabalozi watatu
wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na kupokea nakala ya hati za
utambulisho za balozi mteule wa Italia hapa nchini.
Mabalozi hao
wamekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Burundi Mhe. Gervais Abayeho, Balozi
wa Uingereza Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya,Mhe.Manfredo Fanti.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali
ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu Biashara na
Uwekezaji na Utamaduni.
“Leo nimekutana na mabalozi watatu
kutoka Burundi, Uingereza na Umoja wa Ulaya na nimejadiliana nao masuala
mbalimbali ya ushirikiano katika masuala ya uchumi, biashara na
uwekezaji na mahusiano baina yetu na nchi zao,”amesema Balozi Mulamula.
Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa “mabalozi wote watatu wameahidi
kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya nchi zetu, lakini
pia tumejadili mipango ya kimkakati kutoka kwa Umoja wa Ulaya na
Uingereza ambapo wangependa kuona inaendelezwa katika awamu hii,”
amesema Balozi Mulamula.
Nae Balozi wa Burundi nchini Tanzania
Mhe. Abayeho amesema uhusiano wa Burundi na Tanzania ni wa miaka mingi
na wamefurahia kuuona uhusiano huo ukiendelea kuboreka zaidi na
tunaamini uhusiano huo utaendelea kudumu kwa miaka mingi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfredo Fanti wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Uhusiano wa Burundi na Tanzania ni uhusiano wa muda mrefu na
tunafurahia kuona unazidi kuimarika. Mbali na masuala ya uhusiano
umependekeza utekelezwaji wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa bandari,
barabara na reli uharakishwe kwa manufaa ya nchi zote mbili,” Amesema
Balozi Abayeho.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza hapa nchini
Mhe. David Concar amesema katika kikao chake na Mhe. Waziri wamejadili
namna ya kuboresha uhusiano baina ya Uingereza na Tanzania na jinsi ya
kufanya kazi kwa pamoja katika kudumisha na kuendeleza uhusiano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni wa zaidi ya miaka 46 na umekuwa ukinufaisha pande zote mbili hivyo Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inapata manendeleo kijamii na kiuchumi.
Katika tukio jingine, Mhe. Waziri Mulamula amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi.
“Tanzania na Italia tuna uhusiano mzuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii, uwekezaji na elimu na tumejadiliana mambo aliyoagizwa na serikali yake katika kudumisha uhusiano wa Italia na Tanzania.
Kwa Upande wake Balozi Mteule, Mhe. Lombardi amesema Italia na Tanzania zina masuala mengi ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi,kijamii na utamaduni na kwamba yuko nchini kuhakikisha hayo yote yanatekelezeka kwa maslahi ya nchi zote mbili.
“Tunaamini kupitia maongezi yetu ya leo tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya Italia na Tanzania, lakini pia nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Italia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha mahusiano yake ya kidiplomasia yanakua na kuimarika,”amesema Mhe. Lombardi
Tags
Kimataifa