Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema ajira za walimu 6,000 zitatangazwa hakuna kazi ambayo itatolewa kinyume na utaratibu,anaripoti Angela Msimbira (TANGA).
Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Zingibari iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Waziri Ummy amesema kuna matapeli wameibuka mitaani wakisema kuwa nafasi 6000 hazitatangazwa hivyo watumiwe fedha ili waweze kuwapangia vituo walimu wenye mahitaji na kazi hiyo, huo ni utapeli Serikali haitozi fedha kwa ajili ya ajira na haziwezi kutolewa kinyemela ajira hizo zikikamilika zitatangazwa.
Amewataka waalimu wanaokusudia kuomba nafasi hizo kuwa na subira mpaka zitakapotangazwa na Serikali itatenda haki kwa wote watakaokuwa wameomba nafasi hizo kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.
Aidha,Waziri Ummy amesema kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe ameanza kuchunguza kama matapeli hao ni watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI au ni watu wa mitaani ambao wanadai fedha kwa watu kwa ahadi ya kutoa ajira na ikibainika hatua kali zitachukuliwa kwa mtumishi anayefanya vitendo vya utapeli huo.
Tags
Habari