Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amekabidhi hundi kwa vikundi 37 vya Jiji la Tanga ikiwa ni mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kutoka katika mapato yake ya ndani kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2020/21,anaripoti Nteghenjwa Hosseah.
Waziri Ummy amekabidhi hundi hiyo mapema leo Aprili 26,2021 katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Waziri Ummy amesema, "Tanga mmenifurahisha kwa kutekeleza maagizo ambayo nimeyatoa siku tatu tu wakati nawasilisha Taarifa ya Ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri, nlisisitiza kuhusu utoaji wa mikopo kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemevu na nyie leo mmeanza kutekeleza hilo nawapongeza sana,"amesema Mhe. Ummy.
Ameongeza kuwa, "leo nakabidhi hundi ya shilingi mil. 300 ni furaha kwangu kuona Jiji mmetimiza wajibu wenu sasa nivitake vikundi ambavyo mmapokea fedha hizi mkazifanyie kazi na kuzirejesha kwa wakati ili wenzenu wengine waweze kunufaika na mikopo hii ya Serikali,"amesema.
Akizungumza wakati wa Makabidhiano hayo Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe.Abdulrahman Omary Shiloo amevitaka vikundi hivyo kuacha kwenda kutumia fedha hizo kwa ajili ya kununulia madera na kuvaa wenyewe ila wakazitumie kukuza vipato vya kwa kufanya biashara.
"Msimu huu mnaweza kuutumia vizuri kwa kuwa tunakaribia kwenye sikukuu mkanunue bidhaa zenu hizo za nguo, viatu na kuuza wakati huu tunapokaribia sikukuu bila shaka mtapa faida na marejesho ya mkopo kwa haraka,"amesisitiza Meya Shiloo.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Bw. Daudi Maeji amesema Kwa Bajeti ya Jiji la Tanga walipanga kutoa Mikoa ya asilimia 10 yenye jumla ya shilingi Bil. 1.2 na mpaka sasa wameshatoa shilingi Mil 994 sawa na asilimia 81% ya malengo tuliyojiwekea.
Tags
Habari