Waziri Ummy akoshwa na utendaji wa watumishi TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu, ameridhishwa na kiwango cha utendaji kazi cha watumishi wa Ofisi hiyo kwakujitoa na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake bila kutegea, anaripoti Atley Kuni (OR-TAMISEMI).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo, amesema pamoja na muda mfupi alionao katika Wizara, lakini amekoshwa na kiwango cha utendajikazi, kwakuwa watumishi wa TAMISEMI wamekuwa wakijitoa kwa muda wa ziada ili kukamilisha malengo waliyojiwekea.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri zilizofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21. Baadhi ya kazi hizo ni pamoja na kukamilisha Jengo la Ofisi katika Mji wa Serikali wa Magufuli (Magufuli City) Mtumba na kuhamia, Usimamizi na Ufuatiliaji wa Ujenzi wa Majengo ya Utawala katika Mikoa, Halmashauri, Tarafa, Kata, Mitaa na Vijiji,"amesema Mhe. Ummy.

Waziri Ummy amesema, Ofsi ya Rais-TAMISEMI, imefanya kazi kubwa ya usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa Hospitali za Wilaya na Vituo vya Kutolea Huduma za Afya pamoja na kusimamia na kufanikisha uandikishaji wa Wanafunzi wa Darasa la Kwanza kutokana na Sera ya Elimu bila malipo lakini pia amepongeza kwa usimamizi imara ulio wezesha kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita.

“Natambua kumekuwa na Ongezeko la Mapato ya ndani katika ngazi ya Halmashauri kutoka vyanzo mbalimbali kama vile, ushuru wa mazao, ushuru wa huduma, vibali, ushuru wa magulio na masoko, ada za shule kwa Kidato cha Tano na Sita na ada za uchangiaji huduma za afya na vyanzo vinginevyo kulingana na mapato lindwa ya Halmashauri husika, hii yote ni kazi yakupigwa mfano ambayo TAMISEMI mmeweza kusimamia ikiwepo Ujenzi wa madarasa, Maabara, Mabwalo na Mabweni katika shule zetu,"amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema mabaraza ya wafanyakazi yapo kisheria hivyo yatumike katika kujadili kwa kina mambo yote waliyopanga ili tija iliyo kusudiwa ipatikane.

“Sote tunatambua kwamba Mabaraza ya Wafanyakazi ni Vyombo vya Kisheria vilivyoundwa chini ya Sheria ya Mashauriano katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2003 Kifungu cha 30(3) (The Public Service Negotiating Machinery, Act 2003) kwa lengo la kuongeza tija na uwajibikaji mahali pa kazi”.


Awali akimkaribisha kwa ajili ya uzinduzi wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, alisema Madhumuni ya Baraza la Wafanyakazi ni kutoa fursa kwa watumishi kupitia wawakilishi wao, kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi ya watumishi kwa upande mwingine.

“Baraza la Wafanyakazi linaongeza ushiriki wa Wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli za Taasisi yao kama ilivyofafanuliwa katika Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Sura 105,"amesema Prof. Shemdoe.

Kupitia kikao hicho Wajumbe wa baraza hilo la wafanyakazi, limepitisha kwa kauli moja bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI yenye jumla ya shilingi 7,683,329,644,800.00 kwa ajili ya Fungu Na.56 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Fungu no. 2. Tume ya Utumishi wa Walimu na Mafungu 26 ya Mikoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news