Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema kuwa, kwa kipindi cha mwezi Januari, 2021 hadi Machi 30, 2021 limekabiliana na matukio mbalimbali ya moto, maokozi na ajali za barabarani, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Pamoja na kukabiliana na matukio hayo pia limeendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto, kutoa elimu kwa umma pamoja na kufanya uchunguzi wa matukio ya moto.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini INSP J. K. Mwasabeja kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma
Amesema, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2021 Jeshi limekabiliana na matukio ya moto 366 ambayo yamesababisha vifo vya watu 10, kati ya hao wanaume 8, wanawake 2, matukio hayo yalisababisha majeruhi 30 kati ya hao wanaume 22 na wanawake 8. Pia Shule zipatazo 16 zimeungua katika kipindi hiki cha miezi mitatu na kusababisha uharibu wa miundombinu na kuteketea kwa vifaa mbalimbali.
Pia amesema, jeshi limefanya maokozi katika maeneo mbalimbali zikiwemo ajali za barabarani, mafuriko, kwenye migodi, mashimo ya vyoo, mito, mabwawa, baharini pamoja na maeneo mengine. Jumla ya matukio ya maokozi ni 196. Matukio hayo ya maokozi yalisababisha vifo 103 kati ya hao wanaume ni 85 na wanawake 18. Maokozi hayo yalikuwa na majeruhi 276 kati ya hao wanaume ni 137 na wanawake 139.
Katika kutafuta sababu za matukio hayo. Jeshi linautaratibu wa kufanya uchunguzi ili kubaini vyanzo na kutoa taarifa kwa umma pamoja na ushauri ili kupunguza matukio hayo kujirudia. Hata hivyo Jeshi limebaini majanga mengi ya moto yanatokana na uzembe, hujuma na hitilafu za umeme, kwa upande wa maokozi tumebaini ni uzembe na wananchi kutozingatia tahadhari zinazotolewa na taasisi mbalimbali za serikali.
Pia Jeshi tumebaini Wanafunzi wanachaji simu kwa kificho kwa kutumia nyaya za umeme zilizopita darini, kutumia heater, kutumia pasi bila kuwa waangalifu, mishumaa wakati umeme ukikatika katika shule za bweni.
Ili kupunguza majanga ya moto shuleni, Jeshi liliingia makubaliano na Chama cha Skauti Tanzania, kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto na maokozi kwa Skauti Tanzania Bara, na baada ya Skauti kupatiwaa mafunzo hayo waweze kuwafundisha Wanafunzi wenzao. Kazi hiyo imeshaanza na Skauti kutoka katika Mikoa kadhaa wanaendelea kupata mafunzo hayo.
Aidha Jeshi linaendelea na mikakati ya kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu ikiwemo Masoko, Nyumba za ibada, shule zote za bweni na kutwa na viwanja vya michezo.Kwa huduma ya haraka juu ya majanga ya moto na maokozi Piga namba 114.
Tags
Habari