Na Diramakini (diramakini@gmail.com)
Klabu ya Leicester City imetwaa Kombe la FA England baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea ndani ya dimba la Wembley jijini London.
Ushindi huo ulitokana na bao la mfungaji pekee dakika ya 63, kiungo Mbeligiji, Youri Tielemans akimalizia kazi nzuri ya beki wa England, Luke Thomas.
Kipigo hicho cha moja bila, kilifuta mipango ya Chelsea kuondoka na mataji mawili katika msimu huu.
Wakati hayo yakijiri, kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amesema timu yake ilifanya kila linalowezekana, lakini maamuzi ya Video Saidizi kwa Waamuzi (VAR) yaliwaumiza na kuwanyima ushindi katika mechi hiyo ya Mei 15, 2021.
Ameyesema hayo akizungumzia tukio la mchezaji wa Leicester, Ayoze Perez kuonekana kunawa mpira eneo la hatari lakini baada ya mapitio ya VAR ilionyesha hakukusudia.
“Wachezaji walisema mpira ulienda moja kwa moja mkononi.Unakuwa mchezo wa pili kwa kuumizwa na maamuzi kama hayo, VAR inatuumiza, utakumbuka mechi ya Arsenal pia ilitokea hivi, sio mtaalamu wa kutafsiri sheria ya huu kuwa mpira ulifuata mkono au mkono ulifuata mpira,”amesema Kocha huyo.
Chelsea pia walikuwa kwenye nafasi ya kupata goli baada ya mlinzi wa kushoto Ben Chilwell kukwamisha mpira nyavuni, lakini ilionekana kuwa alikuwa kwenye eneo la kuotea wakati huo.
Tags
Michezo