Corona yakwamisha nyongeza mishahara, Rais Samia aagiza waliondolewa kazini kulipwa mafao yao

“Ndugu zangu mimi ni mama, mama ni mlezi,Dai hili ni la msingi na la kweli. Mishahara haijaongezwa muda mrefu. Kutokana na mlipuko wa ugonjwa Corona uwezo wetu kiuchumi umepungua, imekuwa vigumu kwangu kuongeza mishahara lakini tutaboresha maslahi ya wafanyakazi, mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, mimi binafsi natamani kuongeza mishahara mwaka huu ila kwasababu mbalimbali nimeshindwa, uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka asilimia 6.9 hadi 4.7 kwa sababu ya Corona, nawaahidi mwakani siku kama ya leo nitapandisha mishahara;...ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.

Hayo yamesemwa leo Mei Mosi, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akiwahutubia wafanyakazi mbalimbali katika Kilele cha Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kitaifa ambazo zimefanyika jijini Mwanza.

Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa,Serikali inatarajia wafanyakazi kati ya 85,000 hadi 91,000 watapanda madaraja mwaka ujao na kuajiri watumishi 40,000 katika Idara ya Elimu na Afya nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wafanyakazi mbalimbali (hawapo pichani) katika Kilele cha Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kitaifa ambazo zimefanyika Jijini Mwanza leo Mei 1, 2021 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. (Picha na Ikulu).

Rais Samia ameagiza kuundwa mara moja kwa bodi ya mishahara itakayomwezesha kufahamu kiwango cha kuongeza katika mishahara ya watumishi wa umma na sekta binafsi nchini.

Pia amewaomba radhi wafanyakazi kwa kutokidhi kiu yao ya ongezeko la viwango vya mishahara ambapo amesisitiza kuwa,inaumiza kuona wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa kipindi kirefu.

Mbali na hayo kwa kuanzia, Rais Samia amesema kuwa,Serikali imepunguza kodi na tozo mbalimbali katika mishahara ya wafanyakazi nchini.

Wakati huo huo, Rais Samia imeagiza wafanyakazi wote wenye elimu ya darasa la saba walioondolewa kazini lakini hawakughushi vyeti walipwe mafao na stahiki zao zote.

"Wapo waliosita kutekeleza maelekezo ya malipo haya kwa kisingizio cha kutotolewa mwongozo, mwongozo ndio huo sasa nimetoa,"amesema.

 
Awali Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) wameiomba Serikali ipandishe mishahara ya wafanyakazi wa sekta zote binafsi na umma ikiwemo kutolea maamuzi  suala la wafanyakazi waweze kupata stahiki zao zinazotokana na jasho lao kwa wakati.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Said Wamba ameyasema hayo wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi  ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kilele hicho.

Amesema, kauli mbiu  katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu ni “Maslahi bora,Mishahara Juu”Kazi iendelee" ambapo zipo sababu nyingi za msingi  zilizowasukuma kuunda na kupitisha kauli mbiu hiyo kwa mwaka huu.

Katibu Mkuu huyo amesema,ni wazi kwamba wafanyakazi wa sekta rasmi na walio katika sekta rasmi ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa nchi hivyo mishahara haijaongezwa kwa wafanyakazi hapa nchini miaka nane kwa sekta isiyo rasmi na miaka sita kwa sekta ya umma.

Aidha, amesema hali hiyo imesababisha kupungua kwa ari na mori wa kazi, hivyo kupunguza ufanisi na uwajibikaji mahali pa kazi huku gharama za maisha zimezidi kupanda wakati stahiki na ujira zimeendelea kuwa duni nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news