Na Shinyanga Press Club Blog
FAMILIA ya kijana Dennis Richard Katambwa (31) mkazi wa Bushushu wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga imeiomba Serikali kuingilia kati ili kujua hatma ya mtoto wao huyo aliyepotea tangu Machi 31, mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha.
Fundi Computer & CCTV Camera na Muuzaji wa Computer Dennis Richard Katangwa (aliyepotea/hajulikani alipo).
Kijana huyo ambaye ni fundi maarufu wa Kompyuta mjini Shinyanga lakini pia anajihusisha na kufunga kamera za CCTV pamoja na kuuza kompyuta na vifaa vyake, alipotea Machi 31, mwaka huu akiwa na gari lake na hajaonekana hadi sasa licha ya jitihada za familia hiyo kumtafuta kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.
Hata hivyo, Mapema mwezi huu inaelezwa kuwa Gari la kijana huyo lenye namba za usajili DFY 863 Toyota VITZ rangi ya blue bahari lilipatikana katika kijiji cha Natta wilayani Nzega likiwa limetelekezwa ambapo ndugu wa kijana huyo walipigiwa simu Mei 5,2021 kuhusu kuonekana kwa gari hilo.
Dada wa Dennis Richard Katangwa Bi. Winfrida Kalubale (kulia) na Baba Mzazi wa Dennis Bwana Richard Katangwa wakizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu Mei 17,2021 katika ofisi ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC)
Dada wa Dennis Richard Katangwa Bi. Winfrida Kalubale (kulia) na Baba Mzazi wa Dennis Bwana Richard Katangwa wakizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu Mei 17,2021 katika ofisi ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC)
Akizungumza Mei 17,2021 na Waandishi wa Habari katika ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC), Dada wa Dennis, Winfrida Kalubale akiwa ameambatana na baba mzazi wa kijana huyo, Richard Katangwa amesema kuwa siku ya Machi 31, 2021 ndugu yao akiwa kwenye mazingira yake ya kazi asubuhi alienda kupokea mzigo wa Computer eneo la washusha mizigo mbalimbali kutoka Dar es Salaam (Shy Elimu) mtaa wa Makongoro mjini Shinyanga na kuufikisha ofisini na kumwambia kijana anayemsaidia kuuza dukani aupange mzigo huo, kisha yeye akaondoka na flash akasema anarudi.
Lakini baada ya takribani dakika 45 gari lake lilirudi na watu wawili mwanamke na mwanaume ambao hawakushuka kutoka kwenye gari, wakafika karibu na ofisi kisha Dennis akampigia kijana wake awapatie laptop na Sh. 10,000.
Fundi Computer & CCTV Camera na Muuzaji wa Computer Dennis Richard Katangwa (aliyepotea/hajulikani alipo)
Ofisi ya Fundi Computer & CCTV Camera na Muuzaji wa Computer Dennis Richard Katangwa (aliyepotea/hajulikani alipo).
“Kijana akawapelekea kwenye gari wakashusha kioo wakachukua. Kazi zikaendelea lakini baadae wateja wakiwa wanakuja wanalalamika hawampati Dennis na simu hapokei, ilipofika jioni kijana akawa na mashaka kwamba kwanini boss wake hapokei simu, ikabidi aende nyumbani kuangalia akakuta Jirani nae analalamika kwamba wanampigia simu hawampati maana kaacha bomba chumbani linamwaga maji.
“Asubuhi simu ikawa inapigwa inaita tu lakini haipokelewi na sms hazijibiwi. Rafiki yake mmoja akaona simu yake iko mtandaoni (online) akamtumia sms kwamba mbona unatafutwa hupatikani baadae ile simu ikapotea hewani,” ameeleza Winfrida.
Fundi Computer & CCTV Camera na Muuzaji wa Computer Dennis Richard Katangwa (aliyepotea/hajulikani alipo) akiwa ofisini kwake
Fundi Computer &CCTV Camera na Muuzaji wa Computer Dennis Richard Katangwa (aliyepotea/hajulikani alipo) akiwa kwenye gari lake aina ya Toyota Vitiz lenye namba za usajili DFY 863
Akisimulia kwa masikitiko, Winfrida aliendelea kwa kueleza kuwa jitihada za kumtafuta ziliendelea na baadhi ya ndugu walikuja ndipo wakapata wazo la kwenda kuvunja mlango wa nyumbani kwake, ambako waliingia ndani lakini wakakuta kila kitu kiko sawa ndani ya nyumba.
"Tukaendelea na juhudi za kumtafuta, simu ikawa hewani mara inapotea, baada ya masaa 24 tukaenda polisi ambao mpaka leo wanaendelea kufuatilia. Leo ni siku ya 48 (49) hajaonekana na hatujui alipo, tunaomba serikali iingilie kati ili tujue kijana wetu yuko wapi,"amesimulia.
Wakiwa bado wako njia panda na huzuni kubwa, Jumatano ya Aprili 4, mwaka huu walipokea simu na kuelezwa kuwa gari la ndugu yao aliyepotea limeonekana wilayani Nzega mkoa wa Tabora ndipo walipofanya juhudi za kufuatilia kujiridhisha na kubaini kuwa ndilo gari lenyewe wakawasiliana na Jeshi la Polisi Nzega ambapo ulipofanyika utaratibu wa kulirudisha Shinyanga na mpaka sasa lipo katika kituo cha Polisi Shinyanga.
Amesema tayari familia hiyo imetoa polisi taarifa ya kupotelewa ndugu yao na kuandikiwa RB namba SHY/RB/1385/2021 ambayo walipewa Aprili Mosi, mwaka huu.
Tags
Habari