Jamii yatakiwa kuchukua tahadhari mvua za masika

Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar imeitaka jamii kuchukua tahadhari juu ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha ili kuepukana na majanga ambayo yanaweza kujitokeza, anaripoti Khadija Khamis (Maelezo) Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Devisheni na Athari za Mapema, Omar Ali Mohamed wakati wa kujadili mwelekeo wa mvua za masika katika Kikao cha Wadau wa Maafa kilichofanyika katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi.

Amesema, hali ya mvua inayoendelea kunyesha ni ya kiwango cha wastani vilevile ipo haja ya jamii kuchukua tahadhari kutokana na athari zinazoendelea kujitokeza katika maeneo mbali mbali.

Amefahamisha kuwa, madhara yanayoweza kujitokeza na kuleta athari katika maisha ya watu na mali zao ambayo yanatokana na mvua za masika ni mafuriko, maradhi ya mlipuko, upepo mkali, Rradi,ajali za barabarani, ajali za Bbaharini pamoja na kuanguka au kuporomoka kwa majumba.

Aidha aliitaka jamii kuchukua hatua za mapema kabla ya majanga kutokea kwa kuepuka kukaa au kupita katika maeneo hatarishi yakiwemo kwenye miti mikubwa nguzo za umeme pamoja na barabara au madaraja yaliloathirika.

Alieleza kuwa tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa ni kuhakikisha wananchi wanahama katika maeneo hatarishi na kuhamia maeneo salama.

Alifahamisha katika mvua hizi zinazoendelea kunyesha iko haja ya wazazi na walezi kuweka ulinzi kwa watoto wao kutosogelea katika madimbwi ya maji ya mvua na kutoa taarifa za haraka kwa taasisi husika iwapo kutatokea madhara yoyote ya miundombinu ya maji au umeme.

Hata hivyo Mkuu huyo aliwataka Wadau wa Maafa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi kwa kuchukua njia mbadala kwa zile sehemu zilizopata athari ili kuepusha ajali,kwa kurejesha miundombinu hatarishi iliyoharibika kabla ya kuleta madhara katika maisha ya watu.

Alizitaka mamlaka husika zichukuwe jukumu la kutambua miundombinu ya barabara zilizoharibika na kutayarisha njia mbadala za kupita au kuweka daraja za dharura ili huduma iendelee kupatikana kwa wananchi.

Nae Mkuu wa Shughuli za Hali ya Hewa (TMA) Zanzibar, Hafidh Juma Bakari alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa imetoa taarifa ya muelekeo wa mvua za masika zilizonyesha katika kipindi cha mwezi Machi na April zilikuwa ni za wastani wa asilimia 40,na zinatarajiwa kumalizika wiki ya tatu ya Mwezi wa Mei.

Alifahamisha kuwa mvua zimebakisha muda mchache kumalizika taarifa iliotolewa na Mamlaka hiyo kwa muelekeo wa mvua za masika zitaendelea kunyesha katika wiki mbili za mwanzo wa mwezi mei ambazo zitakuwa ni za wastani na chini ya wastani wakati mwengine zinaambatana na upepo mkali na vipindi vya jua na katika wiki ya tatu zitapungua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news