Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa mkoa mpya wa Simiyu David Kafulila amesema kuwa, atahakikisha anaendeleza yale yote mazuri hasa upande wa Elimu ambayo yalianzishwa na mtangulizi wake ambaye alikuwa Mkuu wa mkoa huo sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Kafulila amesema hayo leo, wakati wa hafla ya kukabidhiwa ofisi, ambapo amesema kuwa kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa mkoa huo siyo kwa ajili ua kuja kutengua bali kwa ajili ya kutimiliza.
Amesema kuwa mkoa wa Simiyu umefanya vizuri katika sekta ya elimu chini ya Anthony Mtaka, na kubainisha kuwa atahakikisha anaendeleza pale ambapo Mtaka ameacha na kufika mbele zaidi.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa, ameomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa mkoa huo, ili kuhakikisha wanafikia malengo makubwa ambayo mkoa umejiwekea na kuwaletea Maendeleo wananchi.
"Mkoa wa Simiyu unaso raslimali nyingi kama mifugo, kilimo, Madini, Jambo ambalo amesema ni fursa kubwa kwa wananchi wa mkoa huo kuzitumia na kuweza kujiletea Maendeleo," amesema Kafulila.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Tabora Anthony Mtaka akizungumza katika hafla, aliwashukuru watendaji wote wa serikali, viongozi, na wananchi kwa ushirikiano ambao walimpatia na kufikia malengo.