NA FRESHA KINASA
Kata ya Kigera Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara inakabiliwa na uhaba wa mipira ya kike na kiume (kondomu), kutokana na uhaba huo, Diwani wa kata hiyo, Alex Nyabiti (CCM) ameiomba kwa msisitizo Kamati ya Kudhibiti Ukimwi ya Manispaa ya Musoma kuongeza huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwekwa, kwani ina idadi kubwa ya wagonjwa kuliko kata zingine ndani ya manispaa hiyo.
Mheshimiwa Nyabiti amesema kuwa, kwa sasa ndani ya kata yake kuna boksi mbili pekee zilizofungwa ndani ya kata yake jambo ambalo linasikitisha.
Amesema,kkata nyingine za Manispaa ya Musoma zikiwemo zenye idadi ndogo ya watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) zina maboksi mengi katika maeneo yaliyotengwa.
Pia amesema kuwa, kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU ndani ya kata yake, ni vema idadi ya boksi zenye kondomu 18 zilizosalia baada ya mgao wa kuzisambaza kata mbalimbali kufanyika zipelekwe kwenye Kata ya Kigera ili kusaidia mapambano ya UKIMWI katika kulinda nguvu kazi ya Taifa hususan vijana.
Diwani wa Kata ya Kigera katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Alex Nyabiti. (Picha na Diramakini (diramakini@gmail.com).
"Niongezewe boksi, dispensa za kondomu kwenye kata yangu ambayo idadi ya watu wanaoishi na VVU ni kubwa, nimeshangaa kuona kamati imeleta boksi mbili tu wakati kata zenye idadi ndogo wamepata mgao mkubwa. Naomba boksi zote 18 zilizosalia nipewe katika kuhakikisha tunakabiliana na UKIMWI kwa kuwalinda vijana wetu ambao ni nguvu kazi kubwa ya Taifa,"amesema.
Kufuatia ombi lake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma, Haji Mtete alisema kuwa, kamati hiyo itakwenda kujiridhisha kuona namna ambavyo uhitaji ulivyo.
"Kamati haina shaka na ombi la Diwani wa kata ya Kigera kuongeza kondomu dispensa kwenye kata yake. Tutajiridhisha tu tuone namna uhitaji ulivyo na tutatekeleza ombi lake kwa maslahi ya kuokoa maisha ya wananchi na kulinda wananchi wetu,"amesema Mtete.
Naye Diwani wa Kata ya Kamunyonge Manispaa ya Musoma, Masumbuko Samson ameishauri Kamati ya Kudhibiti UKIMWI kuweka kondomu dispensa umbali ambao watoto hawataweza kuufikia na kuzichukua kwa matumizi yasiyofaa ikiwemo kuzifanya kama kipulizo.
Huku Meya wa Manispaa ya Musoma, William Patrick Gumbo akihimiza kamati hiyo kuzingatia taratibu na kanuni wakati wa kuweka kondomu katika maeneo mbalimbali kusudi ziongeze ufanisi katika mapambano ya UKIMWI huku akihimiza pia elimu indelee kutolewa kwa ufanisi ya kujikinga na UKIMWI kulinda kizazi na Taifa imara.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dkt.Magreth Shaku ambaye pia ni mratibu wa UKIMWI Manispaa ya Musoma alisema kuwa, walipokea kondomu boksi 104 na kusambaza sehemu mbalimbali kwa kuweka maeneo ya mialo, mikusanyiko ya watu, na sehemu zingine mbalimbali.
Eneo linaloonyesha unapopaswa kuchukua kondomu ukiwa mtaani mjini Musoma. (Picha na Diramakini (diramakini@gmail.com).
Amesema, takwimu za maambukizi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2021 kwa watu waliopima na kugundulika ni asilimia 2.9 ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu wamepima watu 11,104, ambapo wanawake ni 6588, wanaume ni 4516, na waliogundulika na maambukizi ni 324 ambapo wanawake ni 175, na wanaume ni 149.
Dkt.Shaku aliongeza kuwa, kati yao wagonjwa 318 wameanza dawa ambapo wanawake ni 190 na wanaume ni 128. Huku akisema kufikia mwishoni mwa mwezi Machi 2021, jumla ya wagonjwa 8,884 wapo kwenye matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU ambapo pia juhudi mbalimbali za kutoa elimu kwa wananchi katika makundi mbalimbali zinaendelea.
Tags
Habari