Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa watu wengi duniani wanatumia ulaji wa chumvi mara mbili ya kiwango kilichopendekezwa kwa siku na shirika hilo hivyo kujiweka katika hatari kubwa ya magonjwa ya moyo na viharusi ambavyo vinaua watu wanaokadiriwa kuwa milioni 3 kila mwaka.
Kwa mujibu wa UNnews, WHO imetoa muongozo huo mpya wa viwango vya matumizi ya chumvi ulimwengu katika zaidi ya makundi 60 ya vyakula ambavyo vitazisaidia nchi kupunguza viwango vya chumvi katika chakula ili kuboresha lishe na kuokoa maisha.
Mwongozo huo wa kimataifa “wa viwango vya chumvi katika makundi tofauti ya vyakula” ni kwa ajili ya nchi na viwanda ili kupunguza kiwango cha chumvi katika makundi ya vyakula vinavyosindikwa au vinavyotengenezwa viwandani.
Shirika hilo limesema kote duniani ulaji wa vyakula vilivyosindikwa ni chanzo kinachoongezeka kwa kasi cha matumizi ya chumvi.
Kinachochanganya, ni kwamba bidhaa kama hizo za chakula zilizosindikwa mara nyingi huwa na viwango tofauti vya chumvi katika nchi tofauti.
Sasa viwango vinavyolingana vya WHO vitaonyesha nchi jinsi gani zinavyoweza kupunguza malengo yao, kulingana na mazingira ya chakula chao, na kuhimiza viwanda kupunguza kiwango cha chumvi ipasavyo katika vyakula vilivyosindikwa na kusonga mbele kufikia lengo la WHO la kupunguza asilimia 30 ya ulaji wa chumvi duniani ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Who, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema, “Watu wengi hawajui kiasi gani cha chumvi wanachokula au hatari zinazoletwa na ulaji wa chumvi kupita kiasi.
"Tunahitaji nchi kuanzisha sera za kupunguza ulaji wa chumvi na kuwapa watu taarifa wanazohitaji ili kufanya uchaguzi sahihi wa chakula.
"Tunahitaji pia sekta ya chakula na vinywaji kupunguza viwango vya chumvi katika vyakula vilivyosindikwa. Viwango vipya vya WHO vinazipa nchi na sekta ya vyakula muongozo wa mwanzo wa kutathmini na kuanzisha sera za kubadilisha mazingira ya chakula na kuokoa maisha,”amesema.
Muongozo huo mpya wa WHO wa kiwango cha kimataifa cha ulaji wa chumvi unalenga aina mbalimbali za vyakula vilivyosindikwa na vya makopo ambavyo vinachangia ulaji mkubwa wa lishe yenye chumvi nyingi.
Vyakula kama mikate iliyosindikwa na kufungwa katika vifurushi, vitatafunwa vitamu, bidhaa za nyama za makopo na jibini ni miongoni mwa aina ya bidhaa za chakula zenye chumvi nyingi vilivyobainiwa na muongozo mpya wa kimataifa wa ulaji wa chumvi.
Kupunguza kiwango cha chumvi kwa kubadilisha muundo wa vyakula vilivyosindikwa ni mkakati uliothibitishwa wa kupunguza ulaji wa chumvi miongoni mwa watu watu, haswa katika maeneo ambayo matumizi ya vyakula vilivyosindikwa ni makubwa.
WHO inasema hatua hiyo inaweza pia kuzuia vyakula vilivyosindikwa kuwa chanzo kikuu cha chumvi katika nchi ambazo matumizi ya vyakula vilivyotengenezwa viwandani inaongezeka haraka.
Nchini Uingereza, malengo ya hiari ya watengenezaji wa vyakula kurekebisha bidhaa za vyakula yalipunguza ulaji wa chumvi kwa watu wazima kwa takribani kwa asilimia 15 kati ya 2003 na 2011 na kuonyesha kwamba kuweka malengo katika makundi mbalimbali ya vyakula kunaweza kufikia upunguzaji wa maana wa matumizi ya chumvi.
Kwa mujibu wa Dkt. Tom Frieden Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkakati Muhimu wa Kujikita na Kuokoa Maisha (Resolve to save Lives) "Upatikanaji wa vyakula vya bei nafuu, vyenye afya ni muhimu sana kwa watu wote katika kila nchi, viwango hivi vya kimataifa ni hatua muhimu ya kwanza.
"Kadri ladha ya watumiaji inavyobadilika na maendeleo ya teknolojia, serikali za nchi mbalimbali na WHO wanaweza kupunguza kasi ya matumizi ya chumvi kwa muda hadi pale malengo ya upunguzaji wa kiwango kinachotakiwa cha chumvi yatakapotimizwa. Tunapopunguza matumizi ya chumvi hatua kwa hatua, chakula chetu bado kitakuwa na ladha nzuri, na ni mioyo yetu tu ndiyo itakayojua utofauti! ”
Viwango hivi vipya vinazinduliwa wakati ambao ni mwaka muhimu wa sera ya chakula na lishe.
Mkutano wa mifumo ya chakula wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Septemba na mkutano wa lishe kwa ajili ya ukuaji utakaofanyika Desemba itawakutanisha wadau mbali mbali ili kubadilisha mifumo ya chakula kwa kutoa fursa kwa juhudi za kitaifa, kikanda na za kimataifa kuboresha mazingira ya chakula na kutoa ahadi zikiwemo kupunguza kiwango cha chumvi kilichomo kwenye kwenye vyakula vilivyosindikwa.
Tags
Kimataifa