MAJALIWA: KAMILISHENI UJENZI WA MACHINJIO YA VINGUNGUTI

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

WAZIRI MKUU Kassim ameziagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa yaliyopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kazi ya uchinjaji ng’ombe katika Machinjio ya Kisasa Vingunguti jijini Dar es Salaam, leo, Mei 17, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kazi ya uchinjaji mbuzi katika Machinjio ya Kisasa Vingunguti jijini Dar es Salaam, leo, Mei 17, 2021.

Ametoa agizo hilo leo Mei 17, 2021 alipotembelea mradi wa machinjio ya kisasa yaliyopo Vingunguti Jijini Dar es salaam.

"Mstahiki Meya na Mkurugenzi, tunahitaji machinjio haya ili tuweze kuanza kazi, lakini pia Jiji na ushiriki wa wafanyabiashara mifugo zungumzeni kila siku ili mfikie hatua kwamba lini muanze, tunataka tuondoke kwenye eneo hili la zamani, kamilisheni hizo asilimia tano zilizobaki".

Amesema kuwa mpaka sasa asilimia 95 ya ujenzi wa mradi huo imekamilika ikiwemo mitambo ya kuchinjia na eneo la maji taka wakati tangi la kuhifadhia maji, chumba baridi cha kuhifadhia nyama na kuweka sakafu eneo la nje ya kiwanda ambapo mpaka kufikia Juni 30, 2021 kazi zote zitakuwa zimekamilika.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha mifereji ya maji taka yanayotoka katika machinjio hayo yaelekezwe kwenye mifereji maalum hadi mtoni ili yasiingie kwenye makazi ya watu.
Ng’ombe akiingizwa kwenye mtambo maalum wa kuchinjia katika machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyakagua, leo, Mei 17, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mburugwa Matamwe (wa pili kulia) ambaye ni Mhandisi na Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam,leo, Mei 17, 2021.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa ni vyema wafanyabiashara wakaanza kutumia machinjio hayo ya kisasa na yeyote anayetaka kutumia aruhusiwe "mitambo ipo tayari, ni vyema tukawazoesha ili muweze kujua taratibu, mwenyekiti unaweza kuwa unaandaa baadhi ya ng'ombe wakawa wanakuja kwenye machinjio mapya.

Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha anakamilisha haraka taratibu za ujenzi wa sehemu ya reli inayoingia katika machinjio hayo kwa ajili ya kushusha ng'ombe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara wa mifugo wakati alipokagua ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, leo, Mei 17, 2021. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

"Tunataka tuwe na reli fupi inayoingia hapa kwa ajili ya kushusha ng'ombe, hili lifanyike kwa haraka, kusanya fedha ndani ya jiji, safisha eneo hili na tuwape Shirika la Reli watujengee tawi la kuingia hapa, huu ni mradi mkubwa".

Waziri Mkuu amewaasa wafanyabiashara hao kuacha kupiga mihuri ya moto mifugo ili kuifanya ngozi kuwa na thamani " ngozi yoyote ile ikiweka alama huwa inapoteza thamani, tuelimishane ili tuache kuchora mifugo yetu".

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo ambao umefikia asilimia 95, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jumanne Shauri amesema mradi utagharimu shilingi Bilioni 12.49 utakapokamilika na utasaidia kupanua wigo wa masoko ya nje na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ng'ombe na mbuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news