Na Mwandishi Diramakini
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philp Mpango amezitaka kampuni zote zinazoagiza mbegu mbalimbali kutoka nje ya nchi kuzalisha hapa nchini ili kuwezesha uwekezaji wa ndani.

Ameyasema hayo leo Mei 27, 2021 kwenye Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kumbukizi ya Kifo cha Hayati, Edward Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.
“Napenda nichukue nafasi hii kuzitaka kampuni zote ambazo zinaagiza mbegu kutoka nje kuzalisha mbegu hapa nchini na Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo haya na wasisubiri tuwaulize.


“Lakini taasisi zetu za magereza na Jeshi la Kujenga Taifa ni lazima zijizatiti katika kuzalisha mbegu bora na nawataka pia wakuu wa taasisi hizo wajipime utendaji wao wa kazi, tumechelewa sana hatuwezi kwenda kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kwa mwenendo wa tija ambayo tumeuelezea,"amesema Makamu wa Rais.
Dkt.Mpango amepongeza, jitihada zinazofanywa na chuo katika kuboresha teknolojia za kilimo uvuvi na mifugo na kuongeza kuwa pamoja na jitihada hizo bado tija siyo ya kuridhisha katika kuzalisha mazao ya kutosha.
“Napongeza jitihada zenu mlizozifanya katika kuonesha umahiri wenu katika kuboresha teknolojia za kilimo,uvuvi na mifugo, napenda nisisitize kuwa jitihada hizo bado hazitoshi.Hatuna budi sote kwa pamoja Serikali, Chuo Kikuu cha Kilimo, taasisi sekta binafsi na watu wengine tuangalie teknolojia hizi zinazovumbuliwa zinawafikiaje wakulima wa kawaida na kwa gharama nafuu,"amesema.


Mkuu wa Chuo cha SUA, Jaji mstaafu Joseph Warioba akimkaribisha Makamu wa Rais amesema, lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ilikuwa kutaka kutoa elimu ya kilimo na mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na kuwa na akiba ya kutosha.
Jaji Warioba amesema, hata hivyo bado malengo yaliyokusudiwa hayajafikia na kwamba inahitajika waendelee na kufanya utafiti vijijini kuhakikisha wanapata kilichokwamisha jitihada hizo.
Kwa upande wake,Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Raphael Chibunda kwenye risala yake amesema, chuo hicho toka kianzishwe kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mitaala kutoka mitatu mwaka 1984 hadi 106 sasa.



Prof.Chibunda amesema, kumekuwepo ongezeko la wanafunzi kutoka 400 mwaka 1984 hadi kufikia wanafunzi 14,581 na kuwafanya kupanua shughuli zao katika mikoa ya Katavi,Arusha,Njombe na Ruvuma.
Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo, Prof. Chibunda amesema wanakabiliwa na changamoto ya upungufu na uchache wa miundombinu ya kufundishia na watumishi wa kada mbalimbali hususani wa taaluma katika chuo hicho.
Tags
Habari