Na Adili Mhina, Ubungo
Zaidi ya nusu ya idadi ya walimu wote wa
shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es
Salaam watakuwa ni miongoni mwa watumishi wa Umma watakaopanda madaraja
hivi karibuni baada ya Serikali kutoa vibali vya kupandisha madaraja
Watumishi wa Umma nchi nzima.
Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Kinondoni, Florah Kapange (kulia) akitoa maelezo ya zoezi la kupandisha madaraja walimu wa Wilaya hiyo kwa Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape. Mkurugenzi huyo alifanya ziara ofisini hapo kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa zoezi upaandishaji wa madaraja kwa walimu.
Kwa mujibu wa taarifa za ofisi ya Tume ya Utumishi wa Walimu
(TSC) Ubungo, Wilaya hiyo ina jumla ya walimu 3,253 wa shule za msingi
na sekondari za Serikali. Katika idadi hiyo, walimu 2,184 ni wa msingi
na 1069 ni wa sekondani.
Katika zoezi la kupandisha madaraja
walimu nchini, TSC Wilaya ya Ubungo imeeleza kuwa inatarajia kupandisha
jumla ya walimu 1,733 ambapo walimu 1,152 ni wa shule za msingi na
walimu 581 ni wa sekondari.
Idadi hiyo imetolewa jana na Kaimu
Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Ubungo, Florah Kapange alipokuwa akitoa
taarifa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya
Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape kuhusu maendeleo ya zoezi
la kupandisha madaraja walimu katika Wilaya yake. Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape akikagua nyaraka kwenye jalada la mmoja wa walimu wanaotarajiwa kupandishwa daraja ili kujiridhisha kama nyaraka zote zinazohitajika zipo sawa. Ukaguzi huo ameufanya wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Ubungo iliyolenga kuona maendeleo ya zoezi ya upandishaji madaraja walimu.
Kapange alieleza kuwa kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Serikali
kuhusu zoezi hilo, Wilaya hiyo ina zaidi ya nafasi 2000 za kupandisha
madaraja walimu huku walimu wenye sifa za kupanda ni 1,733.
“Baada
ya kufanya uchambuzi tumepata walimu 1,733 wenye sifa za kupanda
madaraja. Hivyo, ikama yetu tuliyonayo inatosha kabisa kuwapandisha
walimu wote wenye sifa”, alisema.
Alisema kuwa tangu kibali cha
kuwapandisha madaraja walimu kitoke, watumishi wa TSC katika wilaya hiyo
wamekuwa wakifanya kazi muda wote ili kuhakikisha wanaendana na muda
uliopangwa na Serikali katika kukamilisha zoezi hilo.
“Kama
unavyotuona hapa tumekuwa na kazi kubwa ya kuchambua majalada ya walimu
wote ili tubaini wale wenye sifa za kupanda. Na hadi sasa tupo katika
hatua nzuri, tunakamilisha uchambuzi na tumeanza kuandaa orodha ya wale
wanaotarajiwa kupanda ili tuiwasilishe kwenye Kamati ya Wilaya ambayo
itakaa ndani ya siku mbili zijazo”, alisema.
Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Ubungo wakiwa katika zoezi la kuandaa orodha ya walimu wenye sifa za kupanda madaraja katika wilaya hiyo.
Alisisitiza kuwa Walimu wa Wilaya hiyo wasiwe na wasiwasi juu ya
zoezi hilo kwani timu yake inafanya kazi kwa uangalifu mkubwa
kuhakikisha kila mwalimu mwenye sifa ya kupanda daraja anapata haki
yake.Zinazofanana soma hapa Walimu 1,333 kupandishwa madaraja wilayani Kinondoni.
“Nitumie fursa hii kuwaondoa hofu walimu wote wa Wilaya ya
Ubungo kuhusu kupanda madaraja. Ubungo tuna nafasi za kutosha kwa
walimu, yaani tumechukua idadi yote ya walimu wenye sifa na bado nafasi
zimebaki. Tuko makini sana, hatutamuacha hata mwalimu mmoja mwenye sifa
ya kupanda,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi Hape alieleza kuwa
ameridhishwa na namna zoezi hilo linavyotekelezwa huku akiwasisitiza
watumishi wa ofisi hiyo kuhakikisha wanazingatia miongozo na taratibu
zilizotelewa ili kila mwalimu apate anachostahili. Mtumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wa Wilaya ya Ubungo akiendelea kuchambua nyaraka katika majalada ya walimu ikiwa ni zoezi la kubaini walimu wenye sifa za kupandishwa madaraja.
“Niwapongeze sana kwa namna mnavyoendelea na zoezi hili, natambua
kuwa kazi hii inachosha maana majalada ni mengi na kazi inatakiwa
ikamilike ndani muda mfupi. Lakini niwaombe sana msije mkafanya kazi
kwa kulipua, TSC ipo kwa ajili ya walimu hivyo ni wajibu wetu
kuwahudumia kwa ubora”, alisema.
Hape alisema kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuondoa
kero na mamalamiko ya walimu yaliyodumu kwa muda mrefu kuhusu
mdadaraja, ndiyo maana alitoa maelekezo kuhusu jambo hilo.
Mtumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wa Wilaya ya Ubungo akiendelea kuchambua nyaraka katika majalada ya walimu ikiwa ni zoezi la kubaini walimu wenye sifa za kupandishwa madaraja. Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape (wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele, aliyevaa gauni) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa (TSC) Wilaya ya Ubungo wakati wa ziara yake wilayani hapo iliyolenga kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa zoezi la kupandisha madaraja walimu. Pembeni yake (mwenye miwani) ni Kaimu Katibu Msaidizi wa Wilaya hiyo, Florah Kapange.
“Lazima tujue kwamba tusipofanya kazi kama inavyotakiwa hatutaeleweka. Yaani Rais amesikia kilio cha walimu na ametuelekeza tuwapandishe madaraja alafu sisi tugeuke kuwa kikwazo, hakuna mtu atakayetuvumilia. Kila mtu akitekeleza wajibu wake vizuri hatutasikia mwalimu anayelalamika kuhusu madaraja”, Hape alisisitiza.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015, TSC ndiyo chombo kilichopewa mamlaka ya kusimamia ajira na maendeleo ya walimu ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kusajili walimu (wapya kazini), kuthibitisha kazini, kupandisha vyeo/madaraja, kubadilisha cheo walimu waliojiendeleza kimasomo pamoja na kutoa vibali vya kustaafu kazi ya ualimu.
Tags
Habari