Mbunge mstaafu wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa amewakumbuka watoto yatima wa kituo cha Masjid Nour kilichopo Kata ya Mlandizi Wilaya ya Kibaha Vijijini kwa kuwapa vyakula ili viweze kuwasaidia katika futari kipindi cha mwezi huu wa Ramadhani, anaripoti Rotary Haule.
Mbunge mstaafu waJimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa(aliyesimama mbele) akiwa pamoja na wazee waishio katika mazingira magumu na baadhi ya madiwani katika hafla ya kugawa msaada wa vyakula vya futari juzi Mlandizi Kibaha Mkoani Pwani.(Picha na Rotary Haule).
Mbali na watoto hao, lakini pia Jumaa ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa futari hizo kwa wazee wanaoishi katika mazingira waliopo katika maeneo mbalimbali ya Kibaha Vijijini.
Hafla ya ugawaji wa futari hiyo imefanyika katika ofisi yake binafsi iliyopo Kata ya Janga Wilaya ya Kibaha Vijijini na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa chama wakiwemo madiwani.
Akizungumza mara baada ya kugawa futari hiyo Jumaa,alisema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa utaratibu aliokuwa akiufanya tangu akiwa mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini.
Jumaa amesema kuwa, watoto yatima ni sehemu ya jamii ambayo inastahili kupata mahitaji muhimu kama binadamu mwingine na kwamba jukumu la kuwalea na kuwatunza yatima ni la kila mtu.
Amesema,watoto yatima hupatikana kwa matatizo mbalimbali ikiwemo Wazazi kufariki,kutupwa na hata katika masuala mengine lakini hawana mtu wa kuwasaidia zaidi yetu sisi.
"Nimekuwa na utaratibu wangu wa kuwakumbuka watoto yatima kwa kuwapa chochote na ukizingatia tupo katika mwezi mtukufu ambao na wao wanahitaji kupata futari ndio maana nimeona niwaletea futari ili ziweze kusaidia katika kipindi hiki cha Ramadhani,"alisema Jumaa.
Jumaa ametaja vyakula hivyo kuwa ni sukari,unga wa ngano,mchele,tambi, mafuta ya kupikia,njugu mawe,tende maharage na unga wa sembe ambapo vimegawanywa kwa wazee na watoto hao.
Mmoja wa wazee hao Shabani Hamisi, alimshukuru Jumaa kwa kujitoa katika kuwasaidia wazee wasiojiweza na hata yatima na kusema jambo hilo linapaswa kuigwa na viongozi wengine wa Chama na Serikali na hata watu binafsi.
Hamisi alisema kuwa, mara nyingi wazee wamekuwa wakisahaulika hasa katika mambo muhimu lakini kwa kitendo cha Jumaa kuwakumbuka katika mwezi mtukufu ni ishara ya kuonyesha upendo kwa wazee wasiojiweza,watoto yatima na jamii nyingine.
Diwani wa Kata ya Janga kupitia CCM, Abdallah Kiddo alimshukuru Jumaa kwa kutoa futari hizo huku akisema mwenyezi Mungu amlinde katika shughuli zake za kila siku kwakuwa kazi aliyoifanya ni baraka kwa mwenyezi Mungu.
Kiddo alisema, anakumbuka Jumaa akiwa mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini ilikuwa kawaida yake ya kutoa sadaka ya futari kwa makundi maalum hasa kipindi cha Ramadhani na nilidhani alivyokosa ubunge atavunja utaratibu huo.
"Mimi nilikuwa nikifikiria huyu Jumaa alivyokosa ubunge hatutamuona tena huku jimboni, lakini amekuwa mtu wa tofauti kwani licha ya kukosa ubunge, lakini bado anakuja kutuhudumia hakika Mungu ambariki sana,"alisema Kiddo.
Hata hivyo, Kiddo alimtaka Jumaa kuendelea na utaratibu huo kwa kuwa ndio sehemu na msingi katika jamii na kwamba ikiwezekana wengine waige kutoka kwake.
Tags
Habari