Na Diramakini (diramakini@gmail.com)
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisuka vema safu ya uongozi wake ambayo amesema kwa maono yake itamsaidia kuifikisha Tanzania katika matokeo chanya kwa haraka.
Mtenga ameyasema hayo mjini Dodoma wakati akizungumza namna ambavyo anavyoguswa na teuzi mbalimbali za Rais Samia ambazo zimelenga kufananikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2020-2025.
Alisema kuwa, ukubwa wa Ilani hiyo ambayo ina kurasa zaidi ya 300 umebeba mambo mengi ambayo yamelenga kutoa huduma bora kwa Watanzania kuanzia mijini na vijijini, hivyo uteuzi wa watu makini kama anaoufanya Rais Samia utawezesha kwenda kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kazi kubwa na nzuri, nichukue nafasi hii kumpongeza kwa teuzi zake ambazo zinalenga kwenda kuimarisha nguvu ili kila mmoja kwa nafasi yake asimamie utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imeainishwa katika ilani.
"Hatua ambayo itaendelea kulifanya Taifa letu kustawi kiuchumi, ninaamini kwa kasi hii na kila mmoja akifanya kazi kwa bidii, tutarajie maendeleo makubwa hapa nchini,"amesema Mtenga.
Amesema, miongoni mwa miradi ambayo anaamini itaendelea kutekelezwa kwa kasi ni pamoja na ile ya maji, nishati, afya, miundombinu, elimu, uwekezaji na uchumi na mingine mingi ambayo ilianzishwa na inatarajiwa kuanzishwa kwa maslahi mapana ya Watanzania.
Tags
Habari