BAADHI ya wananchi na wafanyabiashara ya mawe wa Kijiji cha Fella wilayani Misungwi mkoani Mwanza wamevamia mgodi wa Kokoto wa Rhino Plant Equipment and Transport Ltd uliopo kijijini humo na kusomba mawe yaliyopasuliwa huku wakidai wana maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.
Mwananchi wa kijiji cha Fela wilayani Misungwi mkoani Mwanza, akichukua mawe kwenye eneo la mwekezaji wa kuvunja mawe Rhino, ambapo kuna mvutano na kusababisha kusitishwa uzalishaji.
Mwananchi wa kijiji cha Fela wilayani Misungwi mkoani Mwanza, akichukua mawe kwenye eneo la mwekezaji wa kuvunja mawe Rhino, ambapo kuna mvutano na kusababisha kusitishwa uzalishaji.
Wamedai Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alisema iwapo mwekezaji hatosaini mkataba na wanakijiji wataendelea kuvamia mpaka hapo atakaposaini mkataba ambao Serikali ya kijiji ilimtaka mwekezaji huyo kuusaini.
Uvamizi huo umefanyika toka Mei 4 hadi 9 mwaka huu ambapo wananchi walivamia ndani ya mgodi huo na kukusanya mawe na kisha kuwauzia wenye maroli bila idhini ya mwekezaji huku wakidai wanafanya hivyo kama njia ya kumshinikiza mwekezaji kusaini mkataba wa upangaji katika eneo la mgodi huo.
Akizungumzia uvamizi huo, Mkuu wa Usalama wa Mgodi huo Nasa Mwakambonja alisema kuwa mgogoro huo ulianza Oktoba mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa kijiji hicho Marco Lutubija kuwashinikiza wasaini mkataba mpya kama wapangaji tofauti na makubaliano yao ya awali ikiwemo kulipa Serikali ya Kijiji Sh milioni 25 kila mwaka kama mchango wa kijamii (CSR) na wamelipa.
Alisema kutokana na mgogoro huo, Mwenyekiti aliwasimamisha wasiendelee na uzalishaji hadi hapo watakapo saini mkataba huo vinginevyo wananchi wataingia kusomba mawe yaliyochenjuliwa mgodini humo na kuyauza kwa wenye maroli ili wajipatie fedha.
“Kweli Mei 4 mwaka huu wananchi zaidi ya 60 walivamia na maroli wakaanza kusomba mawe na kuwauzia wenye maroli kila trip Sh 20,000, uvamizi huo umeendelea hadi leo (Mei 9) ambapo zaidi ya trip 200 zimeisha sombwa na kuuzwa kwa wenye marori,” alieleza Mwakambonja.
Afisa huyo wa mgodi, alisema wao siyo wapangaji kwani wamefuata taratibu zote za uwekezaji mgodi na kununua eneo hilo kwa wananchi waliokuwa wakilimiliki kuwalipa fidia.
Alisema ili kuepusha madhara yasiyokuwa ya lazima baada ya wananchi hao kuvamia, hawakuona sababu ya kutumia nguvu kuwadhibiti wananchi hao hivyo walitoa taarifa ya katika kituo cha polisi Misungwi (MIS/RB/736/2021).
Mkuu wa ulinzi wa mgodi wa kupasua mawe wa Rhino Nasa Mwakambonja, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wananchi wa kijiji cha Fela kuvamia mgodi na kuchukua mawe.
“Lakini tulishangazwa sana maofisa wetu wawili walioenda kutoa taarifa polisi waliitwa na DC wakitarajia kuwa watapata ufumbuzi wa uvamizi huo lakini waliswekwa ndani kwa madai ya kukataa kusaini mkataba wa uwekezaji wa kijiji hicho,” alieleza.
Kwa upande wake Mwenyelkiti wa kijiji, Marco Lutubija akizungumzia sakata hilo alikiri kuruhusu wananchi kuingia mgodini na kusomba mawe kuishinikiza kampuni ya Rhino ambayo imegoma kufunga mkataba wa nao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Fela Marco Lutubija, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza, kuhusu mvutano wao na mgodi wa kuvunja mawe wa Rhino uliopelekea mgodi huo kufungwa.
Alisema suala hilo linazo baraka za Mkuu wa Wilaya na kwamba wasipokubali kusaini mkataba ambao unawataka kuwa wapangaji kwa muda wa miaka saba wananchi wataendelea kuchukua mawe yaliyopasuliwa na mwekezaji maana kisheria milima wanaochenjua mawe ni mali ya kijiji hicho.
“Tuliwaambia wasimame kwanza kuzalisha hadi wasaini mkataba lakini saa wamesimama jumla ndiyo maana tukaruhusu wananchi waingie kuchukua mawe na kuuza wajipatia rizki ili waje tusaini mkataba, bila hivyo wakikiuka hatuwezi kuwabana kisheria, tunawadai Sh milioni 25 na ukamilishaji wa choo cha shule yetu ya msingi,” alisema Mwenyekiti huyo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Sweda akizungumza kwa njia ya simu bila kueleza kwanini aliamuru wasimamizi hao wawekwe ndani, alisema mgogoro huo anaufahamu na alisha agiza pande zote mbili zifuate sheria huku akidai milima yote iliyopo katika vijiji ni mali ya vijiji husika na wala havimilikiwi na mtu kama mijini.
Tags
Habari