Leo Mei 7,2021 Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa amewataka Watanzania kupuuza taarifa zilizorushwa na moja ya runinga kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu ameagiza wafungwa wa kisiasa nchini kuachiwa huru.
Msigwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, taarifa hiyo haina ukweli wowote na Mheshimiwa Rais hawezi kuingilia uhuru wa Mahakama.
“Mheshimiwa Rais hajazungumza kitu chochote kuhusiana na wafungwa wa kisiasa,nchi yetu haina wafungwa wa kisiasa,"amesema.
Msigwa amesema kuwa kupitia video fupi inayosambaa kueleza taarifa hiyo pia imeeleza kuwa, Mheshimiwa Rais amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwaachia wafungwa hao wanaodaiwa 23 ambao hawapo.
“Mheshimiwa Rais haingilii uhuru wa Mahakama pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali haendeshi masuala kama haya ya mahakamani kwa mujibu wa sheria zetu na taratibu zetu hivyo Watanzania wapuuze taarifa hizo hazina ukweli wowote,"amesisitiza.
Msigwa amesema, mpaka sasa Serikali imeanza kuchukua hatua na ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi, Kenya inachukua hatua kufuatilia kwa nini chombo hicho kimepotosha kiasi hicho.
Tags
Habari