Muhutasari wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022


Dira:

“Kuwa na Serikali yenye kutoa huduma bora kwa jamii na yenye uhimili mzuri wa uchumi, umoja na maendeleo endelevu”.

Dhamira

“Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika sekta zote za SMZ na masuala ya Muungano kwa kufuata misingi ya Katiba na Sheria pamoja na kufuata misingi ya haki za binaadamu na ushirikishwaji”.


UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu lipokee, lijadili na hatimae likae kama Kamati ya Mapato na Matumizi ili liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na kwa unyenyekevu mkubwa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia afya njema na uhai na kwa uwezo wake anaendelea kutuwezesha kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Aidha, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuiweka nchi yetu katika hali ya amani na utulivu na kutujaalia mashirikiano na upendo miongoni mwetu.

2. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na wananchi wote wa Tanzania kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17/3/2021 na kuzikwa tarehe 26/3/2021 huko Chato Mkoani Geita. Aidha, natoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kifo cha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki tarehe 17/2/2021 na kuzikwa tarehe 18/2/2021 huko Mtambwe Pemba. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu wapendwa wetu hawa mahala pema peponi. Amin.

3. Mheshimiwa Spika, mauti ni haki na ni safari ya kila mmoja wetu, bila shaka wao wametangulia na sisi tupo nyuma yao. Hatutowasahau daima kwa mema waliyoitendea nchi yetu pamoja na uongozi wao uliotukuka uliokuwa na azma ya kulipeleka Taifa hili kwenye mafanikio makubwa. Sisi tuliobakia tutayaendeleza kwa dhati yale yote waliyodhamiria kuyafanya na kusimamia katika nchi yetu. Baada ya kusema hayo Mheshimiwa Spika kwa ridhaa yako sasa nawaomba Waheshimiwa tusimame kwa dakika moja kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wetu hawa.

4. Mheshimiwa Spika, baada ya salamu hizo za pole, sasa napenda kuchukua fursa hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Othman Masoud Othman kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awazidishie nguvu, hekima, busara na uimara wa kuiongoza nchi yetu ili kufikia katika uchumi wa juu.

5. Mheshimiwa Spika, pia, nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi yetu kuelekea katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Namuomba Mwenyezi Mungu amzidishie nguvu, afya, hekima na busara katika uongozi wake na kuweza kuifikia azma aliyo nayo ya kuipa maendeleo makubwa nchi yetu. Aidha, kwa namna ya kipekee nachukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza Viongozi wetu Wakuu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa namna walivyoiongoza nchi yetu na kuweza kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa mafanikio makubwa.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na mapumziko mazuri pamoja na familia zao.

6. Mheshimiwa Spika, Vilevile, shukurani za pekee zije kwako wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa namna unavyoliongoza Baraza hili la Wawakilishi na kwa wasaidizi wako pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza hili kwa namna walivyoanza vyema katika kuwatumikia wananchi katika kazi yao hii. Bila shaka tutaendeleza wajibu wetu huu ili tuweze kuleta maendeleo katika majimbo yetu na Zanzibar kwa ujumla.

7. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, kwa ridhaa yako sasa naomba nieleze kwa muhtasari hali ya masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Bila shaka masuala hayo yataelezwa kwa undani zaidi na Waheshimiwa Mawaziri wakati watakapowasilisha hotuba zao za bajeti.

Hali ya Uchumi wa Zanzibar

Hali ya Ukuaji wa Uchumi

8. Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa tangu mwanzoni mwa mwaka 2020, dunia imekuwa katika mtihani mkubwa wa kuwepo kwa janga la maradhi ya mripuko ya Covid – 19. Kutokana na juhudi mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na janga hilo, shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii duniani zimezorota ikiwemo uwekezaji na uzalishaji, kufungwa kwa mipaka na kusababisha kuporomoka kwa soko la utalii, kuongezeka matumizi ya Serikali katika miradi ya afya kuliko miradi mingine ya maendeleo, kupoteza wananchi wengi kwa vifo pamoja na kusimama kwa miradi mingi ya maendeleo.

9. Mheshimiwa Spika, wakati uchumi wa dunia ukiporomoka kufikia wastani wa asilimia 3.3 kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 2.8 mwaka 2019 na uchumi wa nchi za Afrika ukiporomoka kufikia wastani wa asilimia 2.1 mwaka 2020 kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2019. Uchumi wa Zanzibar umekua katika kipindi cha mwaka 2020 na ikiwa ni miongoni mwa nchi 11 katika bara la Afrika zilionesha ukuaji wa uchumi ingawa kwa kasi ndogo katika kipindi cha mwaka 2020.

10. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Zanzibar umekua kwa kasi ya wastani wa asilimia 1.3 mwaka 2020 kutoka wastani wa asilimia 7.0 mwaka 2019. Kasi hii ya ukuaji katika kipindi hiki pamoja na mambo mengine imetokana na kuongezeka kwa ukuaji wa sekta ndogo ya kilimo kufikia wastani wa asilimia 1.5 na ongezeko la samaki waliovuliwa ambao wamefikia tani 38,107.0 mwaka 2020 kutoka jumla ya tani 36,728.0 mwaka 2019. Vile vile, kumekuwa na ongezeko la ajira serikalini kufikia jumla ya ajira 41,892 kutoka ajira 38,795 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 7.9. Aidha, shughuli za ujenzi zimeongezeka kwa kufikia asilimia 6.5 mwaka 2020 kutoka asilimia 3.1 mwaka 2019 ikichangiwa zaidi na kuendelea kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, vituo vya afya na miradi mengine ya utoaji huduma.

11. Mheshimiwa Spika, sababu nyengine ni kuimarika kwa utoaji huduma kutoka Serikalini kufikia wastani wa asilimia 13.2 mwaka 2020 kutoka wastani wa asilimia 11.5 mwaka 2019, kuongezeka kwa huduma ya elimu kufikia wastani wa asilimia 9.7 kutoka wastani wa asilimia 7.5 mwaka 2019 pamoja na kuongezeka kwa usafirishaji wa zao la karafuu katika kipindi cha mwaka 2020 kufikia jumla ya tani 3,506.8 kutoka tani 1,744.9 mwaka 2019.

12. Mheshimiwa Spika, mafanikio yote hayo yanatokana na kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchini jambo ambalo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi.

Pato la Taifa na Pato la Mwananchi

13. Mheshimiwa Spika, Pato halisi la Taifa limeendelea kuwa zuri ambapo kwa mwaka 2020 lilifikia thamani ya Shilingi 3,116 bilioni ikilinganishwa na thamani ya Shilingi 3,078 bilioni mwaka 2019. Aidha, Pato la Taifa kwa bei za soko limefikia thamani ya Shilingi 4,209 bilioni mwaka 2020 kutoka thamani ya Shilingi 4,136 bilioni mwaka 2019. Hali iliyosababisha Pato la Mwananchi kufikia Shilingi 2,526,000 sawa na Dola za Kimarekani 1,099 kutoka Shilingi 2,551,000 sawa na Dola 1,115. Kipato hiki kimeifanya Zanzibar iendelee kubaki katika nchi za uchumi wa kiwango cha chini cha kati. Kupungua kwa Pato la mwananchi mmoja mmoja kumetokana na kukua kwa kasi ndogo ya uchumi na kuongezeka kwa idadi ya watu.

Mfumko wa Bei

14. Mheshimiwa Spika, kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma nchini imeongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2020 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 2.7 mwaka 2019. Kupanda huko kumesababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa zote za chakula. Bidhaa za chakula zilitoka wastani wa asilimia 2.8 mwaka 2019 hadi kufikia wastani wa asilimia ­5.8 mwaka ­2019. Aidha, bidhaa zisizo za chakula zimeshuka kutoka wastani wa asilimia 2.6 mwaka ­2019 na kufikia wastani wa asilimia ­ 1.7 mwaka ­2020.

Mwelekeo wa Hali ya Uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2021

15. Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa hali ya uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2021 unategemea kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025.

16. Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa lilitarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa baina ya asilimia 4 – 6 kwa mwaka 2020 kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuanza miradi mikubwa ya kipaumbele na maendeleo, kuwa na sera nzuri na jumuishi za uwekezaji pamoja na kuweka mifumo imara ya ukusanyaji kodi.

Hata hivyo, kutokana na kuendelea kuwepo kwa janga la ugonjwa wa Covid – 19 duniani, ­uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2021 unatarajiwa kukua kwa kasi ya chini ya asilimia 5.2. Hii ni kutokana na hali ya uchumi duniani iliyosabishwa na athari za Covid – 19 kwa sekta za uchumi ikiwemo utalii, biashara na uwekezaji.



Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali

17. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka ili kuweza kugharamia matumizi mbalimbali ya Serikali ikiwemo huduma za kijamii. Mbali na kuongeza vyanzo vipya vya kukusanya mapato, Serikali imeongeza usimamizi na ufuatiliaji katika maeneo yetu ya ukusanyaji mapato sambamba na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo katika maeneo yote. Jitihada hizo na hatua zilizochukuliwa tayari zimeonesha mafanikio ambapo takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na muendelezo wa ongezeko la mapato ya Serikali katika kipindi cha miezi sita iliyopita ambapo katika kipindi cha Januari – Machi 2021 zimekusanywa Shilingi Bilioni 236.2 kutoka Shilingi Bilioni 206.7 za Oktoba – Disemba 2020 na Shilingi Bilioni 153.9 za kipindi cha Julai – Septemba 2020.





18. Mheshimiwa Spika, kwa upekee naomba kuchukua nafasi hii kulipongeza Shirika la Bandari Zanzibar kwa hatua kubwa waliofikia katika kukusanya mapato kwa kipindi hiki kifupi ambapo kumekuwa na muendelezo wa ongezeko la makusanyo katika Shirika hilo. Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai – Septemba, 2020 Shirika lilikusanya Shilingi Bilioni 7.9 na kuongeza hadi Shilingi Bilioni 8.5 katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2020.

Ongezeko jengine lilishuhudiwa katika kipindi cha Januari – Machi, 2021 la Shilingi Bilioni 9.4. Bila shaka ongezeko hili la mapato linaenda sambamba na faida inayopatikana ambayo inachangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo katika vipindi hivyo Shirika limepata faida ya Shilingi Bilioni 2.8, Shilingi Bilioni 4.3 na Shilingi Bilioni 5.5 kwa kila kipindi.



19. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuzisisitiza Idara, Taasisi na Mawizara yetu yanayokusanya mapato kuzidisha kasi ya ukusanyaji na kuondokana kabisa kuvujisha mapato hayo. Bado huduma za Serikali kwa wananchi wake zinategemea sana mapato yetu ya ndani, hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha mapato yetu yanaongezeka kila mwaka ili tuzidi kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje.



Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2021/2022

20. Mheshimiwa Spika, ili kuwa na dira ya kufikia katika maendeleo tunayoyahitaji, Serikali imeweka Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo ambao utazingatia malengo na mikakati inayotokana na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050 ambayo inalenga, kuifikisha Zanzibar katika Kiwango cha Juu cha Uchumi wa Kati kupitia mihimili mikuu minne ambayo ni Mageuzi ya kiuchumi; Maendeleo ya rasilimali watu na huduma za kijamii; Kuimarisha miundombinu; na Utawala bora na uhimili. Aidha, Mwelekeo huu umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025.

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati wa ufunguzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi, ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, Maelekezo ya Serikali kiujumla pamoja na miongozo iliyotolewa na viongozi wakuu kupitia sekta tofauti. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imefanya uchambuzi wa programu na miradi mbalimbali na kuelekeza kuanza kwa taratibu za kuiendeleza miradi hiyo kwa njia tofauti na kuiweka katika maeneo manne kama ifuatavyo:-



(i) Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa na Serikali na Washirika wa Maendeleo kwa mwaka 2021/2022 ambayo ni ile inayoendana na dhana ya uchumi wa buluu, kuimarisha mapato na maendeleo ya uchumi na huduma za kijamii kwa ujumla. Programu na miradi katika eneo hili ni pamoja na kuendelea na matayarisho ya Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani na Mpigaduri; Ununuzi wa meli 4 za uvuvi; Kuendelea na uwekaji wa miundombinu ya maji katika visima vya Ras el Khaimah; Kuendelea na Ujenzi wa Hospitali Mpya ya rufaa na kufundishia Binguni; Kuendelea na utekelezaji wa programu ya ajira kwa vijana; na Kuanzisha na kuimarisha mifumo ya kidijitali ya utendaji kazi kwa ujumla, ukusanyaji mapato, usimamizi wa matumizi, manunuzi na utunzaji wa kumbukumbu za usajili wa mali za umma.



(ii) Miradi itakayotekelezwa kwa ubia katika kuimarisha dhana ya mashirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Maeneo yalikusudiwa kuwemo katika kundi hili ni pmoja na Kuendeleza Uwanja wa Biashara na Maonyesho ya Kimataifa Zanzibar (Nyamanzi); Ujenzi wa masoko na stendi maeneo ya Chuini (Kwanyanya), Jumbi, Mkokotoni, Machomane na Ng’ombeni; Kuendeleza sekta ya maziwa; Uvunaji wa maji ya mvua kupitia ujenzi wa makinga maji; na Ujenzi wa kituo cha usarifu na uhifadhi wa bidhaa za samaki.



(iii) Miradi inayopendekezwa kutekelezwa na sekta binafsi ni miradi katika maeneo ya Ujenzi wa nyumba za makaazi; Ujenzi wa viwanda vya mwani; Kuongeza thamani ya zao la dagaa; Kuanzisha mashamba ya kufugia samaki na Kuanzisha mashamba ya kibiashara ya kufugia majongoo bahari.



(iv) Miradi ya kipaumbele inayopendekezwa kufanyiwa Upembuzi Yakinifu (Feasibility Study) ambayo sekta husika zinapaswa kuanza kutayarisha maandiko ya miradi hiyo ambayo inajumuisha Kuanzisha vituo vya kulelea na kukuza wajasiriamali katika kila Mkoa, Unguja na Pemba; Kuanzisha na kuendeleza maeneo ya Viwanda (Industrial Parks);

Uanzishwaji wa viwanda bunifu vya kuchakata mazao na matunda na mboga mboga (Agro processing innovation hub); Uimarishaji wa kituo cha kisasa cha taarifa (Data centre) kwa kuondoa vifaa chakavu na kuweka mifumo mipya; Ujenzi wa kiwanda cha dawa na Ujenzi wa kituo cha uchunguzi wa maradhi yatokanayo na kazi.

21. Mheshimiwa Spika, Miradi ilio katika kundi la kwanza itatekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 na ya makundi mengine itatekelezwa kuanzia mwaka 2021/2022 au miaka ya mbele.

Sekta ya Uchumi wa Buluu

22. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Nane imedhamiria kuijenga Zanzibar mpya yenye uchumi wa kisasa kwa kuzingatia matumizi na usimamizi endelevu wa bahari na rasilimali zake pamoja na ukanda wa pwani kwa jumla. Itakumbukwa vyema wakati wa uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi katika hotuba yake Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo pia imeelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa kwa maana ya Uchumi wa Buluu (Blue Economy).

Alisema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbalimbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini. Hivyo, Serikali itaendelea kusimamia, kuratibu na kuimarisha maendeleo ya Uchumi wa Buluu Zanzibar ikiwemo uvuvi na utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeongeza nguvu kwenye uwekezaji, ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya uchumi wa buluu ikiwemo utafutaji wa mafuta na gesi asilia; ujenzi wa bandari mpya za uvuvi; uimarishaji wa uvuvi wa bahari kuu, ujenzi wa mitambo na viwanda vya kuhifadhi, kusarifu na kuchakata dagaa na samaki pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uvuvi wa matenga (Fish Cage Farming).

23. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) inaendelea na Mradi wa Ujenzi wa Diko na Soko la Samaki, Malindi ulioanza mwaka 2019. Mradi huu unaotarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 14.7 hivi sasa umefikia asilimia 55 ya ujenzi wake ambapo kwa takriban mwaka mmoja ulisimama kutokana na kuibuka kwa maradhi ya Covid – 19 duniani kote. Mradi unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa Serikali mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

24. Mheshimiwa Spika, kumalizika kwa mradi kutasaidia wananchi kuuza na kununua samaki katika mazingira yanayozingatia usafi na usalama. Aidha, mradi huu unatarajia kuzalisha ajira zaidi ya 6,500 kwa wananchi wetu watakaotoa huduma mbalimbali katika diko na soko hilo.

25. Mheshimiwa Spika, Vilevile, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Shirika la Kimataifa la Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) itatekeleza lengo la ununuzi wa meli mpya nne za kisasa za uvuvi. Meli hizo pia zitashirikisha wataalamu kutoka nje kwa lengo la kujenga uwezo wa wavuvi wetu wa Zanzibar. Aidha, mkazo mkubwa pia umewekwa katika kuendeleza ufugaji wa mazao ya baharini kama vile samaki, kaa, pweza, majongoo bahari na ukulima wa mwani.

26. Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga kuisimamia vyema sekta hii na wananchi wapo tayari kutekeleza na kunufaika na matokeo chanya yanayotokana na uchumi wa buluu. Ni matumaini yetu kuwa wakati tunaendelea na shughuli hizo, uchumi wetu utakua kwa kasi na maendeleo katika sekta mbalimbali yatapatikana ikiwemo kuimarika zaidi huduma za kijamii.

27. Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa wananchi wenzangu kwa vile nchi yetu imezungukwa na bahari na rasilimali zake ni vizuri kuiona dhana ya uchumi wa buluu kama fursa kwa mabadiliko ya kiuchumi. Ni vyema tukaiunga mkono Serikali yetu katika utumiaji mzuri wa rasilimali hiyo. Katika ulimwengu wa sasa uchumi wa buluu ni kati ya maeneo yanayoangaliwa kwa jicho la kipekee nasi tuendelee kuitumia dhana ya uchumi wa buluu kama mkakati wa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu si kwa mtu mmoja mmoja tu bali kwa Taifa kwa ujumla.

Uimarishaji Uchumi na Maendeleo ya Uwekezaji

28. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kusimamia masuala ya uwezeshaji na uwekezaji nchini, Serikali itendelea kutekeleza sheria na miongozo ya kazi; upatikanaji wa ajira za staha hasa kwa vijana na kuimarisha programu za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

29. Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kuimarisha huduma za uwekezaji nchini, Serikali imeimarisha utoaji wa huduma kwa kuweka Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Center) ambapo taasisi zinatoa huduma kwa mashirikiano katika kituo kimoja. Taasisi hizo ni ZIPA, Uhamiaji, Kamisheni ya Ardhi, Kamisheni ya Kazi, Bodi ya Mapato, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Kamati ya Udhibiti na Usimamizi wa Ujenzi (DCU).

Kituo hiki kinatoa huduma za vibali vya kazi na ukaazi, vibali vya ujenzi, usajili wa makampuni na huduma za kodi na mazingira kwa wawekezaji. Kituo hiki kimefanikiwa kupunguza urasimu na muda wa upatikanaji wa vibali vya kazi na ukaazi kutoka wiki tatu hadi wiki moja kwa wawekezaji. Tunaamini kuwepo na kufanyakazi kwa kituo hiki pamoja na mfumo wa kielektroniki wa kusajili wawekezaji unaoandaliwa na ZIPA kutasaidia zaidi kuondoa urasimu na usumbufu kwa wawekezaji wetu.

30. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeazimia kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa ni Kisiwa cha Uwekezaji Maalum. Tayari Serikali ipo katika hatua ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Kukuza na Kulinda Uwekezaji Zanzibar namba 14 ya mwaka 2018 ili kuenda sambamba na azma hiyo. Jadweli nambari tatu na nambari sita za Sheria hiyo yamefanyiwa marekebisho ili kuweka vivutio maalum kwa uwekezaji Pemba. Serikali inaendelea kuweka mifumo na taratibu mbalimbali itakayowavutia wafanyabiashara wakubwa wa nje na ndani ya nchi kuwekeza kisiwani Pemba. Tunaamini uwekezaji huo utakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi wa kisiwa cha Pemba na Zanzibar kwa jumla.

31. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa suala la ajira kwa vijana bado limekuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyetu. Katika kufikia azma yetu ya ajira 300,000 kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeanza kuchukua hatua kwa kuratibu upatikanaji wa ajira katika maeneo mbalimbali.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Machi 2021, Serikali imeratibu upatikanaji wa ajira 1,272 (Wanaume 603 na Wanawake 669) ndani ya nchi katika sekta binafsi za hoteli, viwanda, skuli binafsi na ulinzi. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Wakala Binafsi wa Ajira imeweza kuratibu upatikanaji wa ajira 842 kwa vijana wetu (Wanaume 59 na Wanawake 783) katika nchi mbalimbali ikiwemo Oman, Qatar na Dubai kwa kazi za ulezi wa watoto, udereva, ulinzi, upishi na kazi za nyumbani.

32. Mheshimiwa Spika, Serikali vilevile kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeendelea kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali ya wananchi ili kuweza kuanzisha na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Hadi sasa jumla ya mikopo 617 yenye thamani ya Shilingi 637,425,000 (Pemba Shilingi 221,900,000 na Unguja Shilingi 405,525,000) imetolewa. Mikopo hiyo hutolewa ama kwa vikundi au mtu mmoja mmoja. Pia, kupitia Idara ya Vyama vya Ushirika vimesajiliwa Vyama vya Ushirika 318 (Unguja: 155; Pemba: 163) ikiwemo SACCOS moja. Tunaamini vikundi hivi vyote vinatoa mchango mkubwa katika kuongeza ajira kwa wananchi wetu na kuwaongezea kipato cha kukidhi mahitaji yao hasa yale ya muhimu.

33. Mheshimiwa Spika, Kwa upande mwengine, Serikali kupitia Kamisheni ya Kazi imewapatia vibali vya kazi jumla ya wageni 1,129 kutoka mataifa mbali mbali yakiwemo Italia, India, China, Uingereza na Nchi za Afrika ya Mashariki ili kuweza kufanya kazi hapa nchini.

Uanzishaji wa Maeneo ya Viwanda

34. Mheshimiwa Spika, katika azma yake ya kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kuanzisha Maeneo ya Viwanda (Industrial Parks) katika kila Wilaya za Zanzibar nje ya utaratibu wa ZIPA. Kupitia mradi huu unaosimamiwa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, maeneo hayo yatawekewa miundombinu yote wezeshi kwa ajili ya viwanda vinavyotarajiwa kujengwa na kufanyakazi. Mpaka sasa maeneo matatu (3) ya viwanda tayari yameshatengwa ambayo ni Eneo la Viwanda la Chamanangwe, Eneo la Viwanda la Nungwi na Eneo la Viwanda la Dunga. Serikali tayari imeanza kuliwekea miundombinu muhimu eneo la Chamanangwe lililoko Wilaya ya Wete, Pemba ikiwemo huduma ya umeme, maji na barabara.

35. Mheshimiwa Spika, maeneo yote matatu (3) yatakuwa yakiendelezwa hatua kwa hatua kadri ya fedha zitakapopatikana na Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na washirika wa maendeleo ili kwa pamoja tuweze kuweka miundombinu yote muhimu katika maeneo haya na mengine yatakayowekwa katika kila Wilaya.

Zao la Karafuu

36. Mheshimiwa Spika, zao la karafuu bado linaendelea kuwa moja ya vielelezo vya utambulisho wa Zanzibar na ni moja kati ya vyanzo vyetu vikuu vya fedha za kigeni. Aidha, zao hili limekuwa tegemeo kubwa kwa wakulima kupata fedha na kuendeleza shughuli na mahitaji yao ya kiuchumi na kijamii.

37. Mheshimiwa Spika, kutokana na hali ya uchumi duniani kuendelea kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kusambaa kwa maradhi ya Covid – 19 na kuongezeka kwa nchi zinazozalisha zao hilo duniani, soko la karafuu nalo limekuwa likitikisika kwa kupanda na kushuka. Licha ya hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa mnunuzi pekee wa zao hilo hapa nchini kutoka kwa wakulima ili kuweza kulidhibiti na kulisimamia ipasavyo kiuzalishaji na kiubora.

38. Mheshimiwa Spika, katika usimamizi huo, Serikali imeamua kutumia utaratibu wa mkulima kulipwa asilimia 80 ya bei ya soko la dunia. Kupitia utaratibu huu, baada ya Serikali kuuza karafuu hizo, iwapo karafuu imeuzwa kwa bei zaidi ya iliyonunuliwa kutoka kwa mkulima, mkulima huyo atalipwa tofauti ya bei iliyouzwa karafuu yake.

Hata hivyo, wananchi wafahamu zao hili litakwenda kibiashara zaidi kutokana na soko la dunia litakavyokuwa. Suala la uwazi wa bei litatolewa taaluma zaidi.

39. Mheshimiwa Spika, Pamoja na hayo, Serikali itaendelea na jitihada za kutafuta masoko zaidi ya karafuu duniani ili karafuu zote zinazozalishwa ziwe na soko la uhakika na pia kupata bei nzuri. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta wawekezaji watakaoweza kuanzisha viwanda vya kusarifu karafuu ili kuiongezea thamani karafuu yetu. Vilevile, tutakiimarisha Kiwanda chetu cha Makonyo kilichopo Pemba ili kiweze kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na zenye ubora wa kimataifa.

40. Mheshimiwa Spika, Niwaombe wakulima wetu wa karafuu kuzidisha juhudi za kutunza ubora wa karafuu zao ili ziendelee kuwavuta wanunuzi wetu katika soko la dunia na Serikali kwa upande wake itahakikisha inaweka miundombinu ya zao hilo ikiwemo mikopo kwa wakulima, utoaji wa miche ya mikarafuu bila ya malipo, ujenzi na ukarabati wa vituo vya ununuzi, huduma ya bima kwa wanaopata ajali wakati wa uchumaji karafuu, ujenzi wa barabara maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi na elimu kwa wakulima.

Maendeleo ya Sekta ya Utalii

41. Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Utalii inaimarika na kuleta tija zaidi katika nchi yetu.

Serikali inaendelea kufanya mikutano inayohusu masuala ya utalii kwa njia ya mitandao (zoom meeting) kutokana na kuendelea kwa janga la maradhi ya Covid – 19 duniani. Mikutano hiyo iliyofanywa ni pamoja na Shirika la Ndege la KLM, Giant Tour Operator ya Marekani, Tanzania Qatar Business Forum na Russia Tanzania Cultural Center pamoja na Afisi zote za Kibalozi za Tanzania zilizoko nchi za nje. Mikutano hii imesaidia katika kuhakikisha kuwa ramani ya Zanzibar kama kituo cha utalii inaendelea kubakia kwenye macho na mawazo ya wasafiri ulimwenguni kote pamoja na kudhibiti masoko yetu ya utalii ya asili na kuibua masoko mapya. Serikali pia imeandaa muongozo wa kuendesha shughuli za utalii nchini kwa kuzingatia uwepo wa maradhi ya Covid – 19 duniani ili kuendelea kuikinga nchi yetu na maambukizi ya Korona lakini pia kuwahakikishia wageni kuwa wanatembelea eneo salama.

42. Mheshimiwa Spika, Vilevile, Serikali inaendelea kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii vilivyopo Zanzibar ndani na nje ya nchi kwa njia ya picha (vitual) pamoja na kuratibu mafunzo ya kitaalamu ya habari za kitalii kwa waandishi wa habari 18. Waandishi watano (5) wanatoka Kampuni ya 24 Travel Channel ya Urusi, waandishi wanne (4) kutoka Kampuni ya Russian TV, waandishi sita (6) kutoka Nile TV International ya Misri na waandishi watatu (3) kutoka Kampuni ya Botravail ya nchini Ufaransa. Waandishi hao walifanikiwa kutengeneza filamu kutoka kwenye vivutio vya utalii na kuzionesha filamu hizo kwenye televisheni za nchi zao ili kuitangaza zaidi Zanzibar na kuongeza idadi ya wageni wanaokuja nchini kwetu.

43. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa dhana ya utalii kwa wote, Serikali imewahamasisha Wazanzibari kuwekeza katika sekta ya utalii na tunashukuru dhana hiyo imeitikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, jumla ya miradi 60 ya wazalendo imeanzishwa ikiwemo nyumba za kulaza wageni, kampuni za kuandaa misafara ya watalii, mikahawa na kampuni za michezo ya baharini. Miradi hii vilevile imesaidia katika kutoa ajira za moja kwa moja kwa jamii yetu.

44. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kupanga mikakati mizuri ya ukuzaji utalii wetu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kufanya tafiti za utokaji wa wageni pamoja na kufanya ukaguzi wa miradi ya utalii na doria katika maeneo ya utalii.

Kuendelea kutoa mafunzo kwa watoa huduma za utalii na Masheha juu ya sheria na kanuni ili kuboresha huduma wanazozitoa kwa wageni na kutoa mafunzo juu ya njia bora za kufanya utalii kwa manufaa ya nchi yetu. Wito wangu kwa wanaotoa huduma za utalii kuendelea kushirikiana na Serikali kwa namna zote katika kuiendeleza sekta hii muhimu ambayo ina tija kubwa kwa nchi yetu.

45. Mheshimiwa Spika, suala la utalii linaendana sana na kuitangaza Zanzibar kihistoria na kitamaduni. Katika kuiunganisha historia ya Zanzibar na utalii, Serikali imefanya utafiti mdogo na kuweza kupata taarifa za historia kwa maeneo ya Chemchem, kwa Mazinge na Shangani yaliyopo Mkokotoni (Unguja) na utafiti juu ya Mji wa Mkumbuu kwa Pemba kwa lengo la kutaka kuurudisha katika hali yake ya awali na kuweza kuvutia zaidi. Vile vile tunaenedelea kuyatangaza maeneo yetu ya kihistoria ndani na nje ya nchi kwa kuchapisha vipeperushi pamoja na kuweka mabango ya maelezo ambayo yatasaidia kufahamika kwa historia katika maeneo ya kihistoria kama Bungi, Mvuleni, Mtoni na Maruhubi.

46. Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Wizara inayosimamia Mambo ya Kale kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu, kusimamia kwa ukaribu zaidi miradi ya Uhifadhi wa Majengo na maeneo ya wazi kwa mujibu wa Mpango Mkuu wa Uhifadhi (Conservation and Heritage management Plan), kushirikiana na sekta binafsi katika uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe kwa kuufanya Mji huu kuwa kivutio zaidi cha utalii na kuongeza Pato la Taifa pamoja na kuzidi kutoa elimu kwa wananchi na kuwataka kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Sekta ya Utalii ili kufikia azma ya Serikali ya “Utalii kwa Wote”.

Upatikanaji wa Maji Safi na Salama pamoja na Umeme

47. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora ya maji safi na salama imefanikiwa kurejesha huduma hiyo katika baadhi ya maeneo baada ya kufanya matengenezo katika visima vilivyokuwa na hitilafu Unguja na Pemba. Jumla ya visima 25 vimefanyiwa matengenezo kati ya visima 85 kwa Unguja na Pemba sambamba na kuzifanyia matengenezo pampu na Mota 9. Aidha, jumla ya pampu 8 zimenunuliwa na kufungwa katika Kisima cha Kiembe Samaki kwa Bakathir, Bumbwini Kidanzini, Mfenesini, Bumbwisudi NB5, NB7, NB8, Bumbwini Uwandani na Kiashange JP5 – 2. Pampu hizo hivi sasa zinafanyakazi na kusambaza maji katika maeneo hayo na maeneo mengine.

48. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza juhudi za kutunza na kuhifadhi vianzio vya maji, Serikali imefanikiwa kuyalinda kwa kuyawekea uzio maeneo 86 kati ya 315 kwa Unguja na Pemba. Vilevile Serikali imefanikiwa kutafuta Hatimiliki za maeneo ya visima na vyanzo vya maji ambapo maeneo 67 yamepatiwa Hatimiliki kati ya maeneo 302 kwa Unguja na Pemba.

49. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora ya maji safi na salama. Hivi sasa inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Maji Zanzibar (Rehabilitation and Improvement of Water Supply System in Zanzibar – “RIWSSZ”) wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 92.18.

Mradi huu unatarajiwa kuchimba visima 64 vyenye uwezo wa kuzalisha jumla ya lita 792,000 kwa saa na kujenga matangi 14 (matangi saba (7) ya ardhini yenye uwezo wa kuhifadhi lita 101 milioni kwa siku na matangi saba (7) ya juu yenye uwezo wa kuhifadhi lita 54.45 milioni kwa siku). Tunaamini baada ya kukamilika kwa mradi huu utakaohusisha maeneo ya Wilaya za Magharibi A, Magharibi B na Kati kutakuwa na upatikanaji endelevu wa maji safi, salama na ya kutosha na kwa gharama nafuu kwa watu na sekta zote katika maeneo husika. Aidha, kupitia mradi huu kutakuwa na utaratibu wa kutumia teknolojia za usimamizi wa rasilimali maji zenye kuzingatia utunzaji wa mazingira, kwa kukuza uchumi, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.

50. Mheshimiwa Spika, licha ya jitihada hizo, bado natoa wito kwa Mamlaka ya Maji – ZAWA kujitahidi kutumia vifaa bora katika miundombinu yao ya usambazi maji kwani kumebainika hitilafu nyingi katika miundombinu yao hali inayosababisha kuvuja kwa maji na wakati mwingine wananchi kukosa maji kabisa licha kuwepo kwa miundombinu. Aidha, ni vyema wakawatathmini upya wakandarasi wao kwa miradi mbalimbali juu ya uwezo wao wa kutoa huduma waliokubaliana.

51. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huduma za umeme, Serikali kupitia Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) imefanikiwa kupunguza maeneo yanayopata matatizo ya umeme mdogo Unguja na Pemba.

Katika kipindi hiki jumla ya maeneo 29 kati ya 64 kwa upande wa Unguja na tisa (9) kati ya 52 kwa upande wa Pemba yameondokana kabisa na tatizo hilo. Aidha, Shirika limefanikiwa kupeleka umeme katika vijiji 29 Unguja na vijiji 20 Pemba. Pamoja na mambo mengine, usambazaji wa umeme katika vijiji vingi kumetokana na punguzo kubwa la ada ya uunganishaji umeme kutoka Shilingi 460,000 hadi Shilingi 200,000

52. Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu, hadi mwishoni mwa mwezi wa Machi 2021, jumla ya wananchi 10,410 kutoka maeneo mbalimbali hasa ya vijijini wameungiwa umeme ambapo katika kipindi hicho kwa bei ya awali inakisiwa wananchi 4,850 tu ndiyo wangehudumiwa. Jitihada zote hizi zinachukuliwa ili kuweza kuyafikia maeneo yote ya Zanzibar kwa kuyapa huduma bora za umeme.

Huduma za Afya

53. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kusimamia sera yake ya kuwa wananchi wanapata huduma za afya bila ya gharama yoyote kama inavyostahiki. Hivyo, jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili upatikanaji wa huduma hii uwe endelevu ikiwa ni pamoja na kujenga na kuvifanyia matengenezo vituo vya afya pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa afya kwa lengo la kuwawezesha kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa.

54. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kutekeleza mikakati mbalimbali ili kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinanavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga. Miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa ni kufanya uhakiki wa vifo hivyo ili kubaini sababu zilizopelekea na kuchukua hatua stahiki. Aidha huduma za chanjo kwa watoto chini ya umri wa mwaka mmoja zinaendelea kutolewa katika vituo vya afya Unguja na Pemba ili kuwakinga na maradhi mbalimbali hatarishi.

55. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ugonjwa wa malaria, tunashukuru Mungu unaendelea kudhibitiwa na kubakia chini ya asilimia moja. Hata hivyo, yapo baadhi ya maeneo ambayo hutoa wagonjwa zikiwemo Wilaya za Mjini, Magharibi ‘A’ na Magharibi ‘B’. Katika kipindi hiki cha utekelezaji, jumla ya wagonjwa 440,715 walichunguzwa vimelea vya malaria, kati yao wagonjwa 2,626 sawa na asilimia 0.6 waligunduliwa kuwa na vimelea hivyo na wote walipatiwa matibabu stahiki.

Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga ikiwemo kutumia vyandarua na kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la upigaji dawa majumbani ili tuendelee kuupiga vita ugonjwa wa malaria hapa nchini.

56. Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuhakikisha tunaimarisha zaidi huduma za matibabu, upatikanaji, utunzaji na usambazaji wa dawa, huduma za mpango wa damu salama, huduma za udhibiti wa kemikali, chakula, dawa na vipodozi. Aidha, tutahakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya tiba; ununuzi wa vitenganishi vya vinasaba (DNA) pamoja na vifaa vya maabara unakuwa endelevu sambamba na kuongeza idadi ya rasilimali watu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kila inapohitajika.

57. Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa wanajamii wenzangu tuendelee kutumia huduma zinazotolewa na hospitali zetu zilizomo katika Wilaya zetu na inapobidi katika Hospital za Rufaa. Vilevile, niendelee kuwakumbusha kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na maradhi yasiyoambukiza na ya mripuko ambayo yamekuwa yakiibuka siku hadi siku yakiwemo saratani ya matiti, kisukari, shindikizo la damu na ulinganisho wa uzito na kimo cha mwili (BMI) pamoja na kujikinga na maradhi ya miripuko kama vile kipindupindu na Covid – 19 kwa kufuata miongozo ya wataalamu wetu wa afya.

Sekta ya Elimu

58. Mheshimiwa Spika, Kama tunavyofahamu tarehe 23 Septemba 1964 Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi alitangaza elimu bila malipo kwa Wazanzibari wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news