NA FRESHA KINASA
Wasomi wa fani mbalimbali waliohitimu na wanaoendelea kuhitimu vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini, wameaswa kuwa na mawazo mbadala ya kubuni na kuvumbua fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazowasaidia kujiajiri na hivyo kuondokana na changamoto ya ajira.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph ameyasema hayo leo Mei 25, mwaka huu wakati akizungumza na Diramakini Blog.
Mwalimu Makuru amebainisha kuwa, Tanzania ni Taifa ambalo kwa sasa lina idadi kubwa ya wasomi wanaohitimu vyuo vya kati, vyuo vya ufundi (VETA) na vyuo vikuu hivyo wanapaswa kuondokana na dhana ya kuajiriwa kwani Serikali haiwezi kumudu kuwaajiri wote kwa pamoja.
Amesema, ujuzi na utaalamu wanaoupata katika vyuo wanapaswa kuutumia kubadilisha changamoto zilizopo katika jamii yao na kuzigeuza ziwe fursa kiuchumi hususani kubuni miradi mbalimbali, kufanya biashara pamoja na kutumia Sekta ya Kilimo ambayo ina nafasi kubwa ya kutoa ajira kwa vijana na Watanzania kwa ujumla.
"Ukweli ni kwamba, kila mwaka wasomi wanahitimu vyuo mbalimbali na kurudi kukaa wakisubiria Serikali iwaajiri. Serikali imekuwa ikitangaza nafasi chache tu za ajira na tumekuwa tukishuhudia idadi kubwa ya wasomi hujitokeza kuomba ajira, lakini wachache hubahatika, lazima pawepo na njia mbadala wanapohitimu wawaze kujiajiri kwa kutumia maarifa, elimu na ujuzi ambao hufundishwa vyuoni,"amesema Mwalimu Makuru.
Aidha, Mwalimu Makuru ameiomba Serikali kutengeneza mazingira bora na wezeshi ya kuwawezesha wasomi kupata mitaji pindi tu wanapohitimu masomo yao ikiwemo kuweka utaratibu wa kuwapa mikopo kama ambavyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwani itasaidia wengi kupata mitaji tofauti na ilivyo sasa.
"Serikali inatambua kuwa haiwezi kuwaajiri wasomi wote, ni vyema sasa ikaweka mfuko maalumu wa kuwakopesha wahitimu pindi tu wanapomaliza masomo yao. Kusudi mwenye kuanzisha kilimo awe na mtaji, na mwenye kuanzisha biashara vivyo hivyo, badala ya kumuacha ajitegemee mwenyewe kwani wengi wanapohitimu masomo yao huwa hawana mitaji, jambo hili lingefaa sana naiomba Serikali ilizingatie,"amesema Mwalimu Makuru.
Pia aliiomba Wizara ya Uwekezaji kuongeza kasi ya kuwawezesha wahitimu wanaohitimu kada mbalimbali hapa nchini waweze kupata mitaji yenye riba nafuu pamoja na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha Watanzania wanaohitimu waweze kufanya biashara kwa uhuru, haki pamoja na kuwaendeleza kimkakati ili siku za usoni waweze kufikia mafanikio.
"Wakiendelezwa vyema, wataweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kuajiri Watanzania wenzao na kuweza kuisaidia Serikali kupambana na janga la ukosefu wa ajira ambalo limekuwa ni tatizo kubwa ndani ya Taifa letu. TRA iwe na utaratibu mzuri wa kuwapa muda wa matazamio wahitimu wanapokuwa wameamua kujiajiri ama kuwekeza katika miradi mbalimbali, itachochea wengi kupenda kujiajiri sio mtu leo anafungua biashara kesho TRA wanamfuata wanamwambia njoo ofisini na kuanza kukadiriwa mapato,"amesema Mwalimu Makuru.
Pia, aliiomba Serikali kuanzisha kitengo maalumu cha ufuatiliaji wa biashara zinazoanzishwa na wahitimu wa vyuo mbalimbali ili kuweza kuwapa elimu ya kibiashara pamoja na kuratibu changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili kutowakatisha tamaa katika biashara zao na uwekezaji wanaoufanya katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru aliiomba Wizara ya Elimu kuboresha mitaala ya elimu kuanzia chini hadi vyuo vikuu ili kuendana na hali ya sasa na mazingira yaliyopo. Kwani mitaala ya sasa inamwandaa mwanafunzi au mwanachuo kutegemea kuajiriwa na Serikali hivyo kuna haja ya mitaala kubadilika kumwandaa mwanafunzi au mwanachuo kujiajiri na kujitegemea pindi anapohitimu masomo yake.
"Mitaala inapaswa kutazamwa upya na kufanyiwa maboresho mazuri mfano wanafunzi waandaliwe kuanzia elimu ya chini kusomea fani anayoitaka mapema ili kumfanya aje kiwa mbobezi na kumfanya apende fani yake kama anapenda kilimo aandaliwe mapema na asome mchepuo wa kilimo, kama ni biashara asome biashara, kama ni mfugaji aandaliwe kuanzia chini, kama ni mwanamichezo au wasanii waandaliwe chini kusudi akija kukua aje kujitegemea kama ambavyo baadhi ya mataifa ya Ulaya mitaala yao ya elimu huwaandaa kuanzia chini,"amesema Mwalimu Makuru.
Pia ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia upya riba za ukopeshaji kwani zipo juu sana. Hivyo kujikuta mikopo hiyo haimsaidii mwananchi wa hali ya chini pindi anapochukua kwa ajili ya biashara yake kwani riba hizo zimekuwa siyo rafiki kutokana na asilimia za riba kuwa kubwa kati ya asilimia 21 hadi 24, alidai kiwango hicho ni kikubwa hivyo BoT ipitie upya riba za benki zote.
Hata hivyo, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupanua Diplomasia na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali zikiwemo nchi jirani za Afrika Mashariki, kwani kutawezesha shughuli za kibiashara na uwekezaji kufanyika kwa ufanisi na kuchochea fursa ya ajira, mahusiano mema ya kibiashara na kiuchumi ambapo aliwasihi wahitimu wote wanaohitimu masomo yao kuchangamkia fursa hiyo.
Tags
Habari