Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Samwel Kiboye (No.3) amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi wote kwa ujumla kumpa ushirikiano wa dhati na kumuunga mkono mkuu wa Mmoa huo ,Mhe.Robert Gabriel Luhumbi kusudi afanikishe malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Amesema, ili maendelo yazidi kufanyika kwa wananchi wa mkoa huo chama hicho na wananchi wote wanajukumu la kumpa ushirikiano wa karibu huku akisema kuwa chama hicho kitashirikiana naye kwa masilahi mapana ya wana Mara.
Ameyasema hayo leo Mei 25, 2021 wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofika Makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mjini Musoma kujitambulisha pamoja na kukabidhiwa ilani ya chama hicho. Na kupata fursa ya kuzungumza na viongozi wa chama hicho kutoka Wilaya za Mkoa wa Mara.
"Mkuu wa Mkoa mpya aliyekuja tumpe ushirikiano tusifanye majungu na migogoro. Tumuunge mkono yeye pamoja na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kusudi mkoa wetu upige hatua kubwa za kimaendeleo hili ndilo ombi langu kwa wana CCM wote na Wananchi wote wa Mara,"amesema Kiboye.
Pia, amewahimiza wana mara wote kushirikiana na serikali,huku akiwahimiza kutotumia mitandao ya Kijamii kusemana kwa mabaya bali waunganishe nguvu kwa pamoja kufanya kazi kwa bidii na kumuomba Mungu afanikishe mipango ya Serikali ya maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.Robert Gabriel Luhumbi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumchagua kuwa Mkuu wa Mkoa huo. Ambapo ameahidi kushirikiana na wana CCM na wananchi wote kwa ajili ya maendeleo.
"Nimetoka Mkoa wa Geita wenye utajiri mwingi wa dhahabu, Mara pia kuna utajiri wa dhahabu, Hifadhi kubwa ya Serengeti, Ziwa Victoria na ardhi nzuri ya kilimo pamoja na mifugo kwa wingi lazima rasilimali hizi ziwanufaishe wananchi. Mimi ni Mtumishi nimeingia kazini rasmi nikuahidi mwenyekiti ushirikiano kwa maendeleo ya wanaMara,"amesema Luhumbi.
Ameongeza kuwa, Kutokana na utajiri wa Mkoa wa Mara hususani uwepo wa makampuni makubwa ndani ya mkoa huo atahakikisha anafanya uchunguzi wa kina kuona fedha wanazotoa kwa namna gani zimefanya kazi kwa kuunda kamati maalumu ambayo pia itahusisha wanachama wa CCM. Amesema nia ni kuona wana Mara wakinufaika na rasilimali zilizomo ndani ya mkoa huo.
"Lazima viongozi wa chama wakiwemo kwenye kamati nitakazoziunda, na pia nataka viongozi wa chama waheshimiwe na washirikishwe kwa kila hatua,kama Tarime ina madini nahitaji kuona Tarime ikiwa Jiji, kama Serengeti ina hifadhi kubwa lazima nione Serengeti imewanufaishaje wananchi. Tusitafute mchawi mbali, tutakabana kuona rasilimali za Mara zinanufaisha wanaMara siyo watu wachache,"amesema Luhumbi.
Katika hatua nyingine Luhumbi ameahidi kufanya ziara katika kata za mkoa huo. Huku akiahidi kuwatumikia wananchi wote kwa moyo mmoja, ili kiwaletea mapinduzi ya kiuchumi pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi yeyote anaomewa kupata haki yake.
Tags
Habari