Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe
amezindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora ulilofanyika katika
ukumbi wa Mtemi Isike ulipo katika Ofisi za mkuu wa mkoa huo tarehe 8
Mei, 2021.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora, hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.Uzinduzi ulifanyika Mei 8, 2021 Tabora.
Mwongozo huo umetayarishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na
Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Mkoa chini ya ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Mwongozo wa uwekezaji ni
nyenzo muhimu itakayosaidia kuzitangaza fursa zilizopo hapa mkoa wa
Tabora zipate wawekezaji na kusaidia kuinua hali ya uchumi wa watu wa
mkoa huu na Taifa kwa ujumla,”Alisema Waziri Mwambe.
Waziri
Mwambe amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo
mkubwa wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara ili
kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama akihutubia wakati wa uzinduzi huo.
“Nimesoma mwongozo kuhusu utajiri na fursa nyingi zilizopo katika mkoa
huu zikiwemo za maliasili, madini, mifugo, kilimo cha tumbaku, pamba,
alizeti pamoja na shughuli za ujasiriamali mdogo na wa kati hivyo
zitumieni kwa tija ya uchumi wa taifa kwa ujumla,”alisisitiza Waziri
Mwambe.
Aliongezea kuwa, zipo fursa mpya zinazojitokeza katika
mkoa huu ambazo ni pamoja na bomba la mafuta ghafi linalotoka Hoima
nchini Uganda hadi Tanga na kupiti mkoa wa Tabora, ujenzi wa reli ya
kisasa ya SGR, umeme wa REA, barabara za lami, Maji toka Ziwa Victoria
na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali.
Aidha
Waziri alieleza matarajio yake kuhusu hali ya uwekezaji katika mkoa huo
ikiwemo, kuona kila mtendaji wa Serikali ataondokana na urasimu, na
vikwazo visivyo na tija ambavyo vinawakwaza wawekezaji wanapofika katika
mkoa kuwekeza.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akitoa salamu za Wizara yake wakati wa uzinduzi huo.
Akihitimisha hotuba yake, aliutaka mkoa kuendelea kushirikiana na Kituo
cha Uwekezaji cha Kanda (TIC) kilichopo Kigoma kuanzisha Kituo cha
kutolea huduma kwa pamoja (One Top Centre) na kuhakikisha kinakuwa na
rasilimali za kutosha.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama alisema Mpango huu utawawezesha
wakulima hususan vijana kupata pembejeo na masoko ya kuaminika ya bidhaa
zao na kuhakikisha wanajikita katika kilimo cha mashamba ya Pamoja.
“Programu
ya Kilimo cha Mashamba ya Pamoja (Block Farming) inaratibiwa na Wizara
ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha wananchi hususan vijana kufanya
kilimo biashara chenye tija na kuongeza uzalishaji katika sekta ya
kilimo ambapo kupita kilimo cha pamoja vijana watawezeshwa kupata mbolea
kwa urahisi, kupata pembejeo za kilimo, kuwekewa utaratibu mzuri na
nafuu wa kusafirisha bidhaa zao kutoka shambani hadi sokoni na
watawezeshwa kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao,”alisistiza Waziri
Mhagama.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa salamu za wizara yake wakati wa uzinduzi huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe pamoja na viongozi alioambata nao wakionesha kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji kwa Mkoa wa Tabora mara baada ya uzinduzi rasmi.
Mfumo huu ukisimamiwa vizuri ndio njia sahihi itakayoiwezesha
nchi yetu kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo. Mfumo huu unachochea
matumizi ya teknolojia za kisasa na kuwezesha tija kubwa katika sekta
ya kilimo.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Philemon Sengati
alishukuru hatua muhimu ya uzinduzi wa mwongozo huo, huku akieleza namna
mkoa utakavyohakiksha unatekelezwa kwa vitendo na kukiri ni tukio la
kihistoria na la heshima kwa mkoa kwa ujumla.
Alifafanua kuwa,
uwepo wa mwongozo huo utasaidia kutangaza fursa na vivutio vya uwekezaji
ikiwemo ardhi, idadi kubwa ya mifugo takribani milioni 3.7, utalii wa
kihistoria, uwepo wa madini na mapori ya akiba pamoja na misitu ya
hifadhi inayofaa kwa ufugaji wa nyuki na uvunaji wa mazao ya misitu.
“Zipo
sababu nyingi za kuwekeza Tabora ingawa hili la utashi wa kisiasa
limechochea kuvutia wawekezaji katika kuhakikisha changamoto na vikwazo
vinaondolewa kwa wakati,”alisema Dkt. Sengati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya KilimoTanzania (TADB), Japhet Justine akitoa salamu za ofisi yake wakati wa uzinduzi huo.
Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU) .
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP hapa nchini, Bi.Christine Musisi alisema UNDP itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Alisema UNDP itaendelea kusaidiana na Mikoa katika utekelezaji wa miongozo hii kwa kutoa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha panapohitajika.
“UNDP kwa Kushirikiana na Serikali, Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) zimefanikisha kuandaa miongozo katika mikoa 25 na miongozo hiyo ipo katika hatua mbalimbali na itazinduliwa siku za hivi karibuni,”alisema Musisi
Mawaziri wengine waliohudhuria na kutoa neno ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.
Tags
Habari