NIC lawapa faraja yatima, wenye mahitaji maalum jijini Mwanza

Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa watoto yatima na wajane jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa futari, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Elirehema Doriye amesema zoezi la kushiriki futari na kutoa zawadi kwa wahitaji katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan litafanyika katika mikoa minne ambapo mpaka sasa wameshakwenda katika mikoa ya Tanga, Tabora, Mwanza na watamalizia katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kwa mwaka huu tutafanya kwenye mikoa minne lakini mwakani tutaongeza zaidi ili kuwafikia waislamu wengi zaidi na kushiriki katika ibada,"amesema Dkt.Doriye.

Aidha, Dkt.Doriye amesema wameamua kufanya hivyo kwasababu ni muhimu kwao kurudisha katika jamii kwani wanachokipata kinatoka katika jamii ambayo wanaifanyia huduma hiyo na imewawezesha kufikia mafanikio hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella alilipongeza Shirika la Bima la Taifa NIC kwa kutoa msaada kwa wahitaji pamoja na kushiriki Futari katika mwezi huu wa ibada kwa waislam kote Duniani.
“Shirika la Bima lilipotea katika ramani sasa naliona linafufuka linakuja tena kwenye soko la bima na wote tuliopo hapa ndio washirika kwahiyo hii sio hasara ni uwekezaji na ninaamini italipa tu kwa maana imefanyika katika mazingira yenye baraka,"amesema RC Mongella.

Pamoja na hayo RC Mongella amezitaka taasisi zingine pamoja na watu binafsi kuiga mfano uliofanywa na Shirika la Bima la Taifa NIC kwa kuwa mstari wa mbele kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji ili kwa pamoja tuweze kuinyanyua jamii yetu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news