Rais Dkt. Mwinyi:Tumedhamiria kuimarisha mishahara ya wafanyakazi kada ya kati nchini

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ina azma ya kutekeleza utaratibu wa kuimarisha viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa ‘kada ya kati’, pale hali ya uchumi itakapozidi kuimarika, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
 
Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Mei 1, 2021 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.
Amesema wafanyakazi wa eneo hilo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwa vile ndilo lenye wataalamu, ikiwemo walimu, wafanyakazi wa afya na wengineo ambapo hivi sasa wamekuwa wakilipwa mishahara duni.
 
Rais amesema kuwa,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba ilikuwa na nia njema ya kuimarisha mishahara kwa wafanyakazi wa ngazi zote kwa awamu tatu, hata hivyo hatua hiyo ilishindwa kukamilika kutokana na kuibuka kwa ugonjwa Corona na kuathiri ukusanyaji wa mapato na hivyo utaratibu huo kuishia kwa kuimarisha viwango vya mishahara ya kima cha chini hadi kufikia shilingi 300,000.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji, Mhe.Mudrik Ramadhan Soroga na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Ndg. Ali Mwalimu, alipowasili katika viwanja vya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akielekea katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yalioadhimishwa Kitaifa katika Mkoa wa Mjini Magharibiu Unguja na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar.Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) Ndg. Ali Mwalimu akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar, kabla ya kumkaribisha mgeni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na Wafanyakazi.

Aidha, amesema Serikali inalenga kuangalia upya utaratibu wa malipo ya kiunua mgongo kwa wafanya kazi waliostaafu (maarufu kwa jina la vikokotoo) ikiwa na lengo la kuwanufaisha wafanyakazi, wakati huu ambapo wafanyakazi na wastaafu wengi wanalalamikia utaratibu huo.

Akigusia upande wa wastaafu na wazee, Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha maslahi yao, kwa kuhakikisha malipo ya viinua mgongo kwa wastaafu na pencheni jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70 zinazendelea kutolewa kwa wakati na bila usumbufu.

Amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kupunguza umri huo wa wazee pamoja na kuongeza kiwango cha posho, pale hali ya uchumi itakapoimarika.Akizungumzia juu ya changamoto mbalimbali zilizoelezwa katika Risala ya Wafanyakazi, ambapo nyingi zinahusiana na maslahi yao, alisema Serikali inazifahamu changamoto hizo na tayari imeanza kuzichukulia hatua, hivyo akawataka wafanyakazi kuendelea kuvuta subira kwa imani ya kupatiwa ufumbuzi hatua kwa hatua.

Alieleza kuwa taratibu na tathmni za miundo ya Utumishi Serikalini inaendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha watumishi wote wanapata haki zao pamoja na kujengewa mazingira bora ya kufanyakazi ili kuongeza ufanisi.Alisema kipindi kifupi cha Uongozi wa Awamu ya nane, Serikali imeanza vyema utekelezaji wa malengo yake kwa mujibu wa Mipango mikuu, ikiwemo ilani ya Uchaguzi mkuu wa CCM wa 2020-2025, MKUZA 11, Dira ya Zanzibar (2020-2050) pamoja na mingine ya kisekta na kimataifa.

Alisema hali ya nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi serikalini inaendelea kuimarika, huku kukiwepo nidhamu katika matumizi ya fedha za umma kwa kiasi kikubwa.Alisema kumekuwepo ufanisi katika utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi katika sehemu mbali mbali za utoaji huduma, ikiwemo hospitali, vituo vya Afya na Ofisi za Serikali.

MKURUGENZI wa Jumuiya ya ZANEMA Ndg. Salah Salim Salah akitowa salamu za Wafanyakazi wa Zanzibar katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi iliofanyika katika ukumbi Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanziubar

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Bi. Mwatum akisoma Salamu za Wafanyakazi wa Zanzibar wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi iliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akizungumza wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yalioadhimishwa katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimishi ya Siku ya Wafanyakazini Duniani Mei Mosi yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

“Lazima tuendelee kujenga mazingira bora zaidi ya kuwafanya wananchi wajenge imani na wanufaike vizuri na huduma zinazotolewa serikalini pamoja na kuwaondolea urasimu na usumbufu usio na lazima,"amesema.
 
Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali na kutumia fursa za uwekezaji ziliopo nchini, huku akiwakumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria na wajibu wa kulipa kodi na tozo mbali mbali, kuwapa mikataba wafanyakazi pamoja na kuwawekea fedha zao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF).
 
Aidha, amewakumbusha wafanyakazi kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kufanyakazi kwa bidii na nidhamu ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii, akibainisha mafanikio ya serikali yanategemea mchango mkubwa kutoka kwao.

Dkt. Mwinyi alitoa shukurani kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa ushirkiano mkubwa inaotoa, sambamba na kuupongeza Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa kushirikiana vyema na Wizara ya Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, sambamba na kutoa shukurani kwa wafanyaakzi waliotunukiwa zawadi mbali mbali.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR), Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga alisema janga na ugonjwa wa Corona liloikumba Dunia, limeathiri ukuaji wa ajira Zanzibar, huku akiwashauri waajiri wote waliofunga Ofisi zao kutokana na ugonjwa huo kutafakari upya kwa kigezo kuwa wafanyakazi ni kiungo muhimu katika Taifa.Aidha, alisema Wizara hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Idara mbali mbali ili kuona sekta ya kazi inaimarika na kukuza ajira.

Nae, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyaakzi (ZATUC) Mwalim Ali Mwalim aliiomba Serikali kuliangalia kwa makini suala la Vikokotoo, kwa msingi kuwa limekuwa likilalamikiwa na wafanyakazi na wastaafu wengi kutokana na athari zake.

Katibu Mkuu ZATUC, Mwatum Khamis Othman, alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliofikiwa katika kuleta ustawi wa haki za wafanyakazi, alizitaja changamoto kadhaa zinazowakabili, ikiwemo kimya cha Serikali katika kupandisha mishahara na viinua mgongo kwa wastaafu.
 
Amesema, kuna changamoto ya kukosekana utaratibu mzuri wa upandishaji wa madaraja na nyongeza za mwaka pamoja na upatikanaji wa posho mbali mbali za wafanyakazi, ikiwemo mazingira magumu.

Alieleza kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya viongozi ya kutofuata taratibu za ajira pamoja na ucheleweshaji wa malipo ya madeni ya wafanyakazi, ikiwemo nauli.
“Kuna changamoto ya wafanayakzi wa mikataba ambao hufanyakazi kwa muda mrefu katika Halmashauri za wilaya”, alisema.Vile vile, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vyama vya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), Salah Salim salah aliwataka wafanyakazi kubadilika kwa kutoa huduma bora katika maeneo yao ya kazi, kwa kigezo kuwa Dunia hii ni ya ushindani.
WAFANYAKAZI wa Taasisi za Serikali na Binafsi wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani ) akihutubia katika maadhimisho hayo yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi Mfanyakazi Bora kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Tawi la Pemba Ndg. Ali Thani Awesu, wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar. RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya Mfanyakazi Bora kutoka Shirika la Bandari Zanzibar Ndg Masoud Haji Juma, wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
BAADHI ya Wafanyakazi Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupom pichani) akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Baadhi ya Wafanyakazi Bora kutoka Taasisi mbalimbali Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa akiwasilisha salam za wafanyakazi wa Mkoa huo, alitoa pongezi kwa hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa stahiki na haki za wafanyakazi, hususan katika sekta binafsi ikiwemo biashara ndogo ndogo.Alisema pamoja na changamoto mbali mbali zilizojitokeza ikiwemo Ugonjwa wa Corona, Serikali imeweza kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati muafaka.

Maadhimisho hayo yalioambatana na kauli mbiu ya “Uwajibikaji na Haki ndio msingi wa maendeleo ya Zanzibar”, yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said, ,Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news