Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza juhudi za Serikali ya India za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI

Dkt.Mwinyi
amesema kuwa, Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na India ambao umeipelekea nchi hiyo
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi yake ya
maendeleo.
Katika maelezo hayo, Rais Dkt.Mwinyi ametumia fursa
hiyo kuipongeza Serikali ya India kwa kuiunga mkono Zanzibar katika
sekta ya afya, elimu, maji, kilimo, biashara, huduma za jamii,
uendelezaji wa rasilimali watu na nyinginezo.
Aidha, Rais
Dkt.Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya India ya ujenzi wa chuo cha
amali huko kisiwani Pemba ambacho kitatoa mafunzo ya utalii pamoja na
usarifu wa vyakula mbalimbali.
Amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia
kwa kiasi kikubwa kutimiza malengo ya Serikali ya kukuza ajira kwa
vijana pamoja na kuifanya Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uwekezaji
sambamba na kuweza kutoa mafunzo kwa vijana katika kuendeleza sekta
maendeleo ikiwemo utalii.
Rais Dkt.Mwinyi pia, amezipongeza
juhudi za Serikali ya India za kuuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za maji safi na salama.
Pia,
Rais Dkt.Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na India
katika kusaidia masuala tiba pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa
wanafunzi kutoka Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi
ametumia fursa hiyo kuzikaribisha kampuni binafsi za India kuzitumia
fursa mbalimbali zilizopo hapa Zanzibar kwa kuja kuwekeza.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatafuta namna bora ya kuzitumia huduma za mikopo zinazotolewa na India kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi amemuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Mapema Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi zake Zanzibar, Bhagwant Singh ameupongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kusisitiza kwamba nchi yake itauendeleza kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Balozi Singh amempongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kasi kubwa ya maendeleo sambamba na azma yake ya kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kuahidi kwamba India itaendelea kuziunga mkono juhudi hizo.
Aidha, Balozi Singh alieleza kwamba nchi yake itaendea kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar zikiwemo zile za muda mfupi kwa watendaji wa Serikali kupitia Mpango wa India Technical and Economic Cooperation Program” (ITEC) na “International Forestic Science’(IFS).
Pia, Balozi huyo alieleza hatua za nchi hiyo za kuendelea kusaidia upatikanaji wa vitendelea kazi na kuleta wakufunzi katika Chuo cha Amali huko Vitongoji Pemba mradi ambao utawasaidia sana vijana katika kuwapatia mafunzo ya utalii na usafifu wa vyakula na hatimae kuwajengea soko la ajira.
Balozi Singh alilipokea wazo la Rais Dkt.Mwinyi la kuwakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka nchini India kuja kuwekeza hapa Zanzibar na kuahidi kulifanyia kazi.
Tags
Habari