Na Diramakini (diramakini@gmail.com).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 25 Mei, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwana wa Kifalme Faisal bin Farhan Al Saud.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje ya Saudia Arabia,Mwanawakifalme Mhe. Faisal Bin Farhan Al Saud mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Mei, 2021.
Mhe. Rais Samia amemshukuru Mwana wa Kifalme Faisal kwa kufanya ziara hiyo hapa nchini na kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia ambayo inatoa ufadhili katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu hapa nchini.
Amemtaka kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia Mtukufu Salman bin Abdulaziz Al Saud na kumhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Saudi Arabia katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na ustawi wa jamii.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje ya Saudia Arabia Mwanawakifalme Mhe. Faisal Bin Farhan Al Saud mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Mei, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje ya Saudia Arabia Mwanawakifalme Mhe. Faisal Bin Farhan Al Saud mara baada ya mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Mei, 2021.
Baadhi ya maeneo ambayo Mhe. Rais Samia ameomba kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na Saudi Arabia ni kuimarisha biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi, mazao ya kilimo, kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania na kuanzisha ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Saudi Arabia Visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwana wa Kifalme Faisal amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa uhusiano na ushirikiano mzuri wa Saudi Arabia na Tanzania na amemhakikishia kuwa Saudi Arabia ipo tayari kuuimarisha zaidi uhusiano huo katika maeneo mbalimbali yakiwemo biashara na uwekezaji, na ameeleza kuwa Saudi Arabia inahitaji kupata mazao mengi ya chakula.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje ya Saudia Arabia Mwanawakifalme Mhe. Faisal Bin Farhan Al Saud mara baada ya mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Mei, 2021. (PICHA NA IKULU).
Amebainisha kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia kushirikiana ili kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili ikiwa ni pamoja kuwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia ili kukuza utalii na biashara.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Masauni.
Tags
Kimataifa