Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 kupitia Miradi ya Uendelezaji Miji imejenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.53 katika Kata ya Shangani Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa gharama ya Shilingi bilioni 7.09, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Pia katika mwaka wa fedha 2019/20 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara Serikali imejenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 0.85 katika kata ya Shangani kwa gharama ya shilingi milioni 232.98.
Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga (CCM) bungeni jijini Dodoma.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Mheshimiwa Hassan Mtenga.
Awali Mbunge Mtenga alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za lami katika Kata za Ufukoni,Magomeni na Shangani katika Manispaa ya Mtwara Mikindani?.
Naibu Waziri huyo akijibu swali hilo amesema,katika mwaka wa fedha 2020/21 Serikali imetenga shilingi milioni 117.38 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 0.55 kwa kiwango cha lami katika mtaa wa Maduka Makubwa ambapo mkandarasi anaendelea na ujenzi.
Pia amesema,Serikali imeendelea kuzifanyia matengenezo barabara mbalimbali katika Manispaa ya Mtwara.
"Na katika mwaka wa fedha 2020/21 barabara zenye urefu wa kilomita 22.37 zimefanyiwa matengenezo na kilomita 1.3 zinaendelea na matengenezo kwa gharama ya Shilingi milioni 74.19 katika kata za Ufukoni na Magomeni,"amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha, kwa mujibu wa Silinde, Serikali inatambua ukuaji wa haraka wa Mji wa Mtwara na itaendelea kuupa kipaumbele cha barabara za lami na mifereji ya maji ya mvua kwa kadri ya upatikanaji wa fedha huku akisema
Serikali imeendelea kujenga mindombinu ya barabara na kufanya matengenezo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Tags
Habari