Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu ametangaza nafasi za ajira za walimu 6,949 wa Shule za Msingi na Sekondari zinazolenga kujaza nafasi wazi za watumishi waliokoma utumishi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kuacha kazi, kufukuzwa kwenye utumishi na kustaafu, anaripoti Adili Mhina (TSC). Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akitangaza ajira za walimu 6949 wa shule za msingi na sekondari katika mkutano wake na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.
Waziri Ummy alitoa kauli hiyo Mei 9, 2021 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za TAMISEMI jijini Dodoma kwa lengo la kutoa taarifa ya ofisi yake kupata kibali cha ajira kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Tumepata kibali cha ajira za walimu 6,949 pamoja na watumishi 2,726 wa Kada ya Afya. Hivyo, nachukua fursa hii kuutangazia umma kuwa taratibu za kuanza mchakato wa kuomba ajira hizo umekamilika na kwamba waombaji wote wenye nia ya kuomba, sasa wanaweza kufanya hivyo”, alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akitangaza ajira za walimu 6949 wa shule za msingi na sekondari katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma. Pembeni yake ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli.
Alifafanua kuwa waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi ajira.tamisemi.go.tz kuanzia Mei 09 hadi 23 mwaka huu.
Hata hivyo, alieleza kuwa kwa upande wa watu wenye ulemavu hawatalazimika kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao badala yake watatuma maombi yao yakiwa katika nakala ngumu.
“Kwa ndugu zetu wenye ulemavu wanaweza kutuma maombi yao kwa nakala ngumu. Maombi hayo yaeleze aina ya ulemavu na yaambatane na picha kisha yatumwe kwa Katibu Mkuu TAMISEMI. Nakala ya Maombi hayo itumwe Ofisi ya Waziri Mkuu ili Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu aione.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama akiwa katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.
Waziri Ummy alisema Ofisi yake imebainisha sifa mbalimbali za kitaaluma ambazo waombaji wanapaswa kuwa nazo kulingana na muundo wa kada ya ualimu wa shule za msingi na sekondari nchini.
Akianza kueleza sifa za zinazotakiwa kwa walimu wa shule za msingizi, Waziri Ummy alisema katika nafasi ya Mwalimu Daraja IIIA, mwombaji anatakiwa kuwa mhitimu wa Astashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Michezo, Astashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Astashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum.
Aliongeza kuwa mwalimu Daraja la IIIB anatakiwa mhitimu mwenye Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Awali, Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi na Stashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, ambaye pia ni Kamishna wa TSC, Susan Nussu, akiwa katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na waandishi wa habari uliofanyika Mei 09, 2021 jijini Dodoma.
Vilevile, alisema kuwa katika nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIC anatakiwa mhitimu mwenye Shahada ya Ualimu katika masomo ya “English Language, History na Geography”.
Kwa Upande wa shule za sekondari, Ummy alifafanua kuwa nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIB inahitaji mhitimu wa Stashahada ya Ualimu wa masomo ya “Physics, Mathematics, Biology na Chemistry”.
Pia, katika nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIC mwombaji anatakiwa kuwa na sifa mojawapo kati ya Shahada ya Ualimu, Shahada ya Elimu Maalum na Stashahada ya Uzamili katika Elimu (Post Graduate Diploma in Education) katika masomo ya “Physics, Chemistry, Biology na Mathematics”.
Waziri ummy aliongeza kuwa kwa waombaji waliopata elimu Nje ya Nchi, wanatakiwa kuzingatia taratibu zilizowekwa za kupata uthibitisho wa elimu zao kwa mamlaka zinazohusika kabla ya kuomba ajira hizo.
“Waombaji wote waliosoma Elimu ya Sekondari Nje ya Nchi wanatakiwa kupata namba ya ulinganifu wa matokeo kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA). Waombaji waliosoma Vyuo Nje ya Nchi wanatakiwa kupata Ithibati ya masomo yao kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Ummy alisisitiza kuwa kila mwombaji ni lazima awe Raia wa Tanzania mwenye umri usiozidi miaka 45, awe na namba ya kitambulisho cha Taifa, awe na vyeti kamili vya mafuzo ya fani aliyosomea na asiwe mwajiriwa wa Serikali au aliyewahi kuajiriwa na Serikali.
Mkutano huo wa Waziri na Waandishi wa Habari ulihudhuriwa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama ambaye Ofisi yake ndiyo Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za masingi na sekondari walioajiriwa katika utumishi wa Umma.
Tags
Habari