Kituo cha Utafiti wa Kilimo ( TARI) Kihinga mkoani Kigoma kimeendelea kutekeleza kwa kasi agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuzalisha mbegu za michikichi zitakosambazwa nchi nzima ili kuhakikisha nchi inapata mafuta ya kutosha, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Agizo la Waziri Mkuu alilitoa hivi karibuni huku akiitaka Wizara ya Kilimo ikiimarishe kituo cha utafiti wa zao la michikichi cha Kihinga kilichopo mkoani Kigoma kwa kukitengea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu pamoja na barabara ili kuboresha shughuli za utafiti zinazofanywa kituoni hapo.
Aidha, aliitaka wizara hiyo ihakikishe suala la utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu zao la michikichi linaimarishwa na kupewa kipaumbele, na kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuhakikisha utafiti wa mbegu unaofanywa una tija.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na wadau wa zao la michikichi katika ukumbi wa NSSF, Kigoma ambapo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kuwekeza katika zao hilo ili kujiongezea kipato.
“Wizara ya Kilimo hakikisheni mnatumia vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa zao la michikichi. Pia tumieni magari maalumu kwa ajili ya kutolea elimu kwa umma kuhusu zao la michikichi na faida zake,”alibainisha Waziri Mkuu hivi karibuni.
Aidha, kutokana na wito huo TARI imeongeza kasi ambayo imewezesha idadi kubwa ya mbegu za michikichi kusambazwa na kuoteshwa huku nyingine zikiendelea kuzalishwa kama inavyoonekana pichani juu na chini.
Imeelezwa kuwa, mahitaji ya mafuta nchini kwa sasa ni zaidi ya tani 570,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 210,000 tu, hivyo, kiasi cha tani 360,000 huagizwa kutoka nje ya nchi na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 443 kila mwaka, hatua hii ya TARI inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika siku za usoni ambapo zitawezesha Taifa kujitosheleza kwa mafuta ya kula. (PICHA ZOTE NA JUNIOR MWEMEZI-AFISA HABARI WA TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO NCHINI-TARI).
Tags
Habari