TASAF KUFIKISHA RUZUKU KAYA ZOTE MASIKINI NCHINI

Na Robert Kalokola, Geita

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umeanza mpango wa pili wa kutambua kaya zote maskini Tanzania Bara na Visiwani ili ziingizwe rasmi katika mkakati wa kunusuru kaya masikini nchini.
Janeth Maduhu Afisa wa Sheria Makao makuu ya Tasaf, (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog)

Afisa wa Sheria Kutoka Tasaf Makao Makuu, Janeth Maduhu amesema kuwa mpango wa kwanza ulishirikisha kaya maskini kwa asilimia 70 na sasa hivi mpango wa pili utamaliza asilimia 30 zilizokuwa zimesalia.

Janeth Maduhu amesema hayo Mjini Geita katika Ukumbi wa Kituo cha Uwekezaji (EPZ) katika mafunzo ya kuwezesha timu ya wataalam 60 ambao watafanya kazi ya kutambua kaya masikini katika ngazi ya vijiji na mitaa.

Mpango wa pili wa Tasaf wa kutambua Kaya Masikini utafikia kaya zote katika vijiji na mitaa yote Tanzania Bara pamoja na Shehia zote Zanzibar.

Aidha, mpango huo wa pili utatambua wananchi wenye ulemavu kwa ajili ya kuongezwa kwenye mpango wa ruzuku pamoja na wanafunzi wanaosoma kidato cha 5 na 6.

Zoezi la kuwajengea uwezo wataalam wa kutambua Kaya Masikini limeanza rasmi Mjini Geita ambalo linafanyika kwa muda wa siku mbili mfululizo ambalo linahusisha matumizi ya Vishikwambi (Tablets) wakati wa kufanya kazi hiyo.

Mratibu wa Tasaf wa Halmashauri ya mji wa Geita, Upendo Kilonge amesema kuwa zoezi hilo la kutambua kaya masikini katika halmashauri hiyo litafanyika katika mitaa 38 tu ambayo ni sawa na asilimia 30 ya kaya zilizosalia katika mpango wa kwanza.

Amefafanua kuwa, mpango wa kwanza ambao unaendelea kunufaisha wahusika,ulijumuisha vijiji vyote 13 na mitaa 27 na kwamba kwa mpango huu wa pili kaya zote zenye sifa zitaingizwa kwenye mpango.

Upendo Kilonge amewasihi wananchi wenye sifa stahi kujitokeza wakati wa zoezi ili waweze kutambuliwa na wataalam ambao watashirikiana na viongozi wa maeneo husika.

Aidha, amesema hadi sasa Tasaf wameanza kuingia kwenye mfumo wa kulipa ruzuku kwa walengwa kwa njia ya mitandao ( e-payment) ili malipo hayo yamfikie mlengwa mwenyewe.

Amesema, changamoto kwenye mfumo huo wa kulipa kwa njia ya mitandao ya simu ambayo wamesha kumbana nayo, ni baadhi ya ndugu kutokuwa waaminifu.

Ametaja kuwa baadhi ya matukio ni kwa badhi ya wazee kutoa nywila (passwords) zao za mitandao ya simu kwa wajukuu au ndugu na fedha inspowekwa, inatolewa bila kumueleza mhusika.

Amesema, wanapoenda kumuomba asaini kukubali kupokea fedha yake inaonekana fedha haijapokelewa kumbe ilisha ingia na kutolewa bila kujulishwa na ndugu yake au mjukuu wake.

Ameeleza kuwa,inalazimika kuanza kazi ya kutafuta mawakala wa simu ili kujiridhisha kama kweli fedha ilitolewa au la.

Amewataka ndugu na jamaa ambao wanasaidia wazee au walemavu kuwatolea fedha benki au kwenye simu,kuwa waaminifu na kuwafikishia fedha zao pindi Tasaf inapoingiza ruzuku hizo.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii unalenga kuinua vipato vya watu maskini ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuweza kumudu maisha na kupatq huduma za kijamii kama vile afya na elimu.
Upendo Kilonge Mratibu wa Tasaf Wa Halmashauri ya mji wa Geita. ( Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news