Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amezindua mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao utagharimu sh.trilioni 1.3 kwa vijiji 1,976 kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia sasa,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amezindua Mradi Kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili katika Kijiji cha Mpakali Wilayani Mbogwe Mkoani Geita (picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Mradi huo uliopo chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) utakamilika mwaka 2022 ambapo umezinduliwa katika Kijiji cha Mpakali Kata ya LugungaWiaya ya Mbogwe mkoani Geita.
Mkoa wa Geita una jumla ya vijiji 474, lakini vijiji 377 vimeishapata umeme na vijiji 97 havina umeme ambavyo vimetengewa na serikali takribani sh.bilioni 20 ili vijiji hivyo vilivyosalia vipatiwe umeme katika mradi huu uliozinduliwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Medard Kalemani amesema, serikali imeamua kutumia njia za kisayansi kulazimisha wananchi kuingiza umeme kwenye nyumba zao na kuutumia kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.
Ametaja njia hizo za kisayansi kuwa ni serikali imepunguza bei ya kuunganishiwa umeme kutoka 177,000 za awali hadi sh.27,000 na gharama za kulipia nguzo moja zilikuwa kati ya laki nane na zaidi lakini sasa hivi nguzo ni bure.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwaonyesha wananchi wa Kijiji cha Nyakasaluma Wilayani Mbogwe ,kifaa Maalum Cha Umeme Tayari (UMETA) kwa ajili ya matumizi ya kuunganishiwa umeme nyumbani(Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).
Ameeleza kuwa, njia hiyo ya kuondoa gharama zote hizo zinamrahishia mwananchi kumudu kulipia kiwango kidogo kilichopo hivyo kila mwananchi anatakiwa kutandaza waya kwenye nyumba yake na kulipia elfu 27 tu na kuunganishiwa huduma hiyo.
Waziri Kalemani amesema, viongozi wa vijiji na kata wahakikishe wanalipia gharama za kuunganishiwa umeme kwenye taasisi za umma ili mkandarasi wa REA anapofika eneo husika aunganishe umeme kwenye taasisi kama shule,zahanati,misikiti,makanisa na vituo vya afya zikiwa za kwanza.
Amewataka wananchi ambao nyumba zao siyo kubwa na mradi ukiwakuta utandazaji wa nyaya haujakamilika kwenye nyumba zao na siyo kubwa sana waombe kufungiwa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba yote.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA ,Wakili Julius Kalolo akizungumza katika uzinduzi huo amesema malengo ni kusambaza umeme vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2022 na vitongoji vyote ifikapo mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Wakili Julius Kalolo akizungumza katika uwashaji wa umeme katika Kijiji cha Nyakasaluma Wilayani Mbogwe Mkoani Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Amesema, kuanzia mwaka 2008 REA imeishafikisha umeme kwenye vijiji 10,294 hadi mwezi Machi 2021 sawa na asilimia 84 ya vijiji 12,268 vilivyopo Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa bodi ameongeza kuwa, ili kufikia malengo ya kufikisha umeme vijiji na vitongoji vyote,wakala umeandaa mpango kazi wa miaka mitano(2021/22- 2025/26 ambao umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Nyingine ni Sera ya Nishati ya Taifa ya 2015,ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020-2025) na hotuba ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli aliyoitoa akifungua Bunge la 12 ambapo mpango huo umejikita kufikisha umeme kwa Watanzania wote kwenye maeneo ya viwanda,madini ,kilimo,uvuvi na ufugaji.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akimkabidhi Mwananchi wa Nyakasaluma Wilayani Mbogwe ambaye ni mlemavu UMETA ambayo alimpa bure kwa ajili ya kuunganishiwa umeme nyumbani kwake bila kulazimika kusambaza nyaya nyingi ndani ya nyumba.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Amos Maganga amesema, mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo mdogo kilomita 3,450, msongo wa kati na ufugaji mashine umba (transfoma) 3,680.
Amefafanua kuwa, gharama za mradi huo ni takribani triloni 1.3 ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikishana na Benki ya Dunia na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18.
Mkurugenzi Magaga amebainisha kuwa, gharama za kuunganishiwa umeme kwa mteja wa njia moja ( single phase)ni 27,000/ na umeme wa njia tatu (three phase) ni 139,500.
Awali Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Josephat Maganga alimuomba Waziri wa Nishati, Medard Kalemani kupeleka gari katka ofisi ya TANESCO wailayani humo pamoja na pikipiki ili kusaidia watumishi wa shirika hilo kufanya kazi kwa ufanisi.
Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Nicodemus Maganga (aliyesimama) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyakasaluma,kulia ni waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ,wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa REA Amos Maganga na Mwenyekiti wa bodi Julius Kalolo. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Maganga amesema kuwa, watendaji wa Tanesco wilaya wanapata wakati mgumu kufikia wananchi hasa kipindi ambacho inapotokea dharura ya kukatika umeme kwa sababu hawana gari na pikipiki.
Waziri Kalemani ameahidi kuleta gari moja na pikipiki tatu ili ziweze kusaidia kutatua changamoto hizo.
Waziri wa Nishati Medard Kalemani amezindua mradi huo wa tatu mzunguko wa pili na kuwasha umeme katika Kijiji cha Nyakasaluma wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Tags
Habari