Na Mohamed Seif, Mwanza
WADAU
wa mabwawa wamesisitizwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo
na kuhakikisha mabwawa yanasajiliwa kwenye Mamlaka husika ili
yatambulike kisheria kwa lengo la kuepusha madhara yanayoweza
kujitokeza kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa
hivi karibuni Jijini Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo
vya Maji kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa wakati wa kufunga
warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo vya Maji, Rosemary Rwebugisa akizungumza wakati wa kufunga warsha ya Usalama wa Mabwawa. Kulia ni Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Abdallah Mataka na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa, Domina Msonge.
“Zingatieni Miongozo ya Usalama
wa Mabwawa, tunahitaji uwepo wa mabwawa yenye manufaa na ambayo ni
salama kwa viumbe hai na mazingira na si vinginevyo,” alielekeza
Rwebugisa.
Rwebugisa alisisitiza umuhimu wa kutumia Watalam wa
Mabwawa waliosajiliwa kuanzia hatua za awali za usanifu hadi hatua ya
usimamizi wakati tayari yameanza kazi ili kuepukana na changamoto
zinazoweza kusababisha madhara.
Alisema baaadhi ya mabwawa
hukutana na changamoto kadhaa huku mengine yakishindwa kukidhi matakwa
ya matumizi yaliyokusudiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya
kutoshirikisha wataalam. Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa, Domina Msonge akizungumza wakati wa warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
“Kabla hamjaanza
kuchimba ama kujenga mabwawa hakikisheni mnashirikisha wataalam ili
wajiridhishe kulingana na utaalam wao kama bwawa linalotarajiwa kujengwa
mahali hapo linastahili na pia namna gani lijengwe ili kuepukana na
changamoto zinazozuilika,” alisisitiza Rwebugisa.
Alizitaja
baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza endapo bwawa litajengwa bila
ushauri wa kitaalam ni pamoja na kuvuja, jambo ambalo alisisitiza kuwa
ni hatari kwa afya na maisha ya viumbe wanaozunguka eneo husika.
Alisema
jamii pia inapaswa kuelimishwa na kutambua umuhimu wa mabwawa hasa
ikizingatiwa kwamba mabwawa yanazo faida lukuki ambazo baadhi yake
alizitaja kuwa utunzaji wa mazingira kwa kuhifadhi taka hatarishi lakini
pia ni chanzo cha mapato kutegemeana na aina ya bwawa.
Baadhi ya washiriki wa warsha kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kutoka kwa wataalam (hawapo pichani).
“Mabwawa yana faida nyingi sana, ni muhimu jamii ikaelimishwa juu ya faida hizo lakini pia namna ya kuyalinda na kuyatunza ili kuepusha madhara,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu warsha, Rwebugisa alisema imejikita kujadili Miongozo ya Usalama wa Mabwawa na kwamba wadau walioshiriki wajitahidi kufuata miongozo walioijadili.
Alielekeza washiriki kuhakikisha wanaendelea kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha usalama wa mabwawa na kuendeleza mawasiliano ya karibu na ya kila mara na Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wake.
“Mapendekezo yenu tumeyachukua kwa maboresho kwani miongozo iliyopo sio misahafu hivyo tutakuwa tunaboresha kila tunapoona kwa pamoja umuhimu wa kufanya hivyo,” alisema.
Warsha hiyo imeshirikisha Viongozi kutoka Wizara ya Maji, Wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), Wizara na Taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.
Tags
Habari