Na Adili Mhina
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewataka walimu wanaofundisha wanafunzi bila kuzingatia taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kutumia zana za kufundishia kuacha tabia hiyo mara moja kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili na miiko ya kazi ya ualimu.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama akiongea katika mkutano wake uliowahusisha wadau wa elimu (Walimu, Walimu Wakuu, Waratibu Elimu Kata, Wathibiti Ubora wa Shule, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Kamati na watumishi wa TSC pamoja na viongozi wa CWT) kutoka Wilaya ya Singida. Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida, hivi karibuni.
Onyo hilo limetolewa hivi karibuni na Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Singida ambapo pamoja na mambo mengine alifanya mkutano uliowahusisha Walimu, Wakuu wa Shule, Waratibu Elimu Kata, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Wathibiti Ubora wa Shule, Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) pamoja na Kamati na Watumishi wa TSC wa Wilaya ya Singida.
Mkutano huo uliofanyikia katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo wilayani hapo, ulilenga kuwajengea uwezo walimu juu ya kanuni na taratibu za utumishi wa walimu kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake za mwaka 2016 ambazo ndizo zinazoongoza kada hiyo katika masuala ya ajira, maadili na maendeleo kiutumishi.
Nkwama alisema kuwa kwa sasa kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya walimu hususan wanaofundisha shule za sekondari kuingia darasani kufundisha bila kutumia zana za kufundishia kama taratibu zinavyoelekeza jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kazi hiyo.
Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa Katibu wa TSC na Wadau wa Sekta ya Elimu wa Wilaya ya Singida.
“Tulipita kwenye shule zaidi ya 50 za msingi na sekondari kuangalia jinsi walimu wanavyotekeleza majukumu yao. Kwa upande wa shule za msingi hatukuona shida sana lakini kwa walimu wa shule za sekondari tuligundua hawatumii zana za kufundishia kama utaratibu unavyoelekeza,” alisema.
Nkwama alifafanua kuwa utaratibu wa mwalimu kufundisha kwa kutumia zana zinazohitajika uliwekwa ili kumsaidia mwanafunzi kuelewa na kuwa na kumbukumbu nzuri wa kile anachofundishwa, hivyo ni lazima kila mwalimu azingatie utaratibu huo ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Sambamba na hilo Nkwama alieleza kuwa pamoja na serikali kujitahidi kusambaza vitabu shuleni, walimu wengi hawafundishi kwa kutumia vitabu badala yake wanatumia uzoefu tu jambo ambalo ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanafunzi kutofanya vizuri katika masomo yao.
Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Singida, David Brown akitoa taarifa ya utendaji kazi wa ofisi yake kwa Katibu wa TSC (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa Katibu wa TSC na wadau wa sekta ya elimu wa Wilaya ya Singida (hawapo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida, hivi karibuni.
“Serikali imefanya kazi nzuri ya kuleta vitabu mashuleni hivyo walimu wanapaswa kufundisha huku wakifanya rejea kwenye vitabu hivyo, na ni muhimu wawajengee wanafunzi tabia ya kusoma vitabu mbalimbali vya kiada za ziada ili kuongeza uelewa wa kile wa kile wanachofundishwa darasani,” alisema.
Alionya kuwa kila mwalimu azingatie taratibu za kazi na kufanya maandalizi yote yanayotakiwa ikiwa ni pamoja na kufanya maadalio ya somo, kutumia nyezo zinazohitajika kulingana na somo husika kabla ya kuingia darasani kufundisha.
“Kuna walimu tumesahau wajibu wetu, ndiyo maana tumekutana hapa ili tukumbushane kurudi kwenye mstari. Kama wote tukifundisha kwa kuzingatia taratibu, nina imani kuwa wanafunzi watafanya vizuri na tutafikia malengo ya serikali katika eneo la taaluma,” alisema.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia elimu katika Mkoa wa Singida, Nelas Mulungu akitoa neno la shukrani kwa Katibu wa TSC wakati wa mkutano wa Katibu huyo na wadau wa sekta ya elimu wa Wilaya ya Singida uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida, hivi karibuni.
Katibu huyo aliweka bayana kuwa TSC ina majukumu mengi ya kutekeleza ili kuboresha ustawi wa walimu, na haipo kwa ajili ya kusubiri walimu wafanye makosa ili iwafukuze kazi kama baadhi ya wadau walivyokuwa wanaitazama siku za nyuma.
“Hatupendi hata kidogo kuwafukuza kazi walimu, tumejikita sana katika kuwaelimisha ili wawe na mwenendo mzuri na watekeleza majukumu yao bila matatizo. Tunajua wengi wanaelewa na wanajirekebisha, lakini kwa wale ambao hawataki kibadilika, hapo inabidi sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TSC Wilaya ya Singida, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wilayani hapo, David Brown alisema kuwa Wilaya hiyo inahudumia Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambazo zina jumla ya Walimu 2,392.
Afisa anayeshughulikia masuala ya Ajira na Maendeleo ya walimu kutoka TSC Makao Makuu, Francis Gwankisa akiwasilisha mada wakati wa Mkutano wa Katibu wa TSC na wadau wa Elimu wa Wilaya ya Singida uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida, hivi karibuni.
Mwalimu Ruth Kiranga wa Shule ya Msingi Unyianga iliyopo katika Wilaya ya Singida, akiuliza swali kwa Katibu wa Tume (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa Katibu huyo na wadau wa sekta ya elimu wa Wilaya ya Singida.
Aliongeza kuwa katika zoezi linaloendelea la kupandisha vyeo watumishi wa Umma, Wilaya yake imepandisha vyeo walimu 1,351 idadi ambayo ni sawa na asilimia 56.5 ya walimu wote wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha shule za Serikali katika Wilaya hiyo.
Kwa upande wa maadili, Brown alisema kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya kwa walimu kutokana na ofisi yake kufanya kazi kwa ushirikiano na Ofisi ya Elimu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wathibiti Ubora wa Shule, Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili pamoja na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika kuwaelimisha walimu kuzingatia miiko na maadili ya kazi hiyo.
“Mwaka 2018 kulikuwa na mashauri ya nidhamu 18, mwaka 2019 mashauri 12 na mwaka 2020 mashauri 13 na hadi mwezi mei mwaka huu 2021 tumefungua mashauri matatu tu, hii ni kwa sababu tumewafikia walimu wengi na kuwapa elimu,” alisema.
Mwalimu Gadiel Maree wa Shule ya Msingi Unyakumi iliyopo katika Wilaya ya Singida, akitoa maoni wakati wa mkutano wa Katibu wa TSC na wadau wa sekta ya elimu wa Wilaya ya Singida.
Baadhi ya Walimu wa Wilaya ya Singida wakiwa katika Mkutano wa Katibu wa TSC (hayupo pichani) na wadau wa sekta ya elimu wa Wilaya ya Singida. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida, hivi karibuni.
Naye Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu Kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape alieleza kuwa walimu wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili hata ujazaji wa fomu za Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS) uwe na uhalisia.
“Unachukua OPRAS ya mwalimu kila sehemu ukiangalia amejaziwa vizuri sana lakini ukija kukutana na matokeo ya wanafunzi anaowafundisha unakuta wana sifuri. Tunataka OPRAS iweze kutusaidia kujua kiuhalisia kama mwalimu ni mchapakazi au la na hii tunaweza kupima kwa kuangalia ubora wa wanafunzi wake kitaaluma,” alisema.
Kwa upande wake Afisa anayeshughulikia Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Francis Gwankisa aliwakumbusha walimu kuwa na utaratibu wa kufuatilia taarifa za michango yao kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF) ili kuhakikisha usahihi wa michango yao na kama ikibainika kuna dosari wawasilishe taarifa kwa mwajiri ili ifanyiwe kazi mapema.
Naye Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Elimu mkoani hapo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Nelas Mulungu alimshukuru Katibu wa TSC kwa kufika wilayani hapo na kukutana na wadau hao huku akisema kuwa elimu waliyoipata itasaidia kila mtu kuboresha utendaji wa kazi katika eneo lake.
Tags
Habari