Watafiti kutoka Chuo Kikuu
kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) cha mjini Iringa wamegundua dawa ya
kuzuia sumu kuvu kwenye mazao ya nafaka inayotokana na mitishamba
ugunduzi unaotajwa kuleta suluhisho katika uhifadhi wa mazao hayo,
anaripoti Fredy Mgunda.
Akizungumza
katika maonesho ya sita ya utafiti, Dkt.Juma Mongoyo ambaye ni mkuu wa
idara wa kemia katika chuo hicho aliseama, walifanya utafiti kupitia
mmea aina ya Diospyros Mafiensis ambao uligunduliwa Mafia ambapo
walitumia mizizi yake katika utafiti na kuleta matokeo chanya ya utafiti
huo.
Mongoyo amesema kuwa, katika tafiti za mmea huo wamebaini
kuwa mizizi yake hufanya kazi ya kupunguza uzalishaji wa sumu kuvu na
kulinda nafaka isishambuliwe na fangasi aina ya Asperigillus flavus na
Asperigillus parasiticus wanaozalisha sumu kuvu kutokana na joto kali na
unyevunyevu unaotengeneza fangasi hao.
Dkt.Mongoyo amesema kuwa,
takwimu zinaonesha kuwa takribani ya watu million 4.5 duniani wanakula
sumu kuvu kwa kiwango tofautitofauti ambapo huchukua miaka 30 hadi
kujitokeza madhara yake huku akisema kuwa takwimu huonyesha takribani
watu laki moja na elfu hamsini na tano hupoteza maisha kila mwaka
duniani kote kutokana na tatizo la saratani ya maini inayosababishwa na
ulaji wa sumu kuvu.
Mtafiti Princess Ngowi kushoto akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho ya sita ya utafiti katika Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE).
Amesema kuwa, mizizi ya mmea huo wa diospyros mafiensis unauwezo wa kulinda nafaka na jamii yote inayoweza kushambuliwa na fangasi hao wajulikanao kama Asperigillus flavus na Asperigillus parasiticus
Akizungumza mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjjwa ya Binadaamu (NIMR), Prof.Yunus Mgaya alisema kuwa taasisi ya NIMR imeona ipo haja ya kushirikiana na chuo hicho cha Mkwawa kutokana na tafiti hizo wanazozifanya zina lengo moja na taasisi ya NIMR ya kulinda afya ya binadamu.
Amesema kuwa, tafiti iliyofanyika na Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es salaam Mkwawa kuhusiana na mmea unaotumika katika tiba asili ambayo wakatengeneza dawa yenye kemikali inayozuia fangasi isizalishe sumu ambayo ikiingia kwenye mahindi yanayotumiwa na binadamu husababisha saratani ya ini hivyo utafiti huo unaweza ukakinga jamii dhidi ya magonjwa yatokanayo na sumu kuvu.
Aidha, Profesa Yunus Mgaya ameongeza kuwa, katika kuboresha tiba nchini taasisi ya NIMR inajenga kiwanda cha kuzalisha dawa za asili zitokanazo na mimea ambazo zitakuwa kwa mfumo wa vidonge na unga tofuti na sasa hivi ambapo dawa nyingi za asili ni za maji.
Naye Dkt.Evaristo Haulle kutoka chuo cha Mkwawa amesema kuwa, ushirikiano wa taasisi zote za utafiti na za elimu ya juu kuwa na ushirikiano na asasi nyingine ni muhimu hivyo wamepokea kwa mikono miwili ushirikiano kati ya Mkwawa na NIMR.
Maonesho hayo ya utafiti yanajumuisha wanafunzi na walimu watafiti kutoka chuo kikuu hicho kishiriki cha elimu ikiwa ni maandalizi ya kwenda kushiriki maonesho ya wiki ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanayobeba kauli mbiu isemayo “utafiti na uvumbuzi endelevu kwa maendeleo ya viwanda”.
Tags
Habari