WAZIRI MCHENGERWA: TAIFA HALIWEZI KUENDELEA KWA KUWA NA VIONGOZI NA WATUMISHI WANAOENDEKEZA MAJUNGU BADALA YA KAZI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi na watumishi katika taasisi za umma kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuendekeza majungu mahala pa kazi jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya Utumishi wa Umma na Taifa kwa ujumla, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-Utumishi).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Magu.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Watumishi na Viongozi wasiowajibika hawana nasafi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imedhamiria kutoa huduma bora kwa wananchi, na kuongeza kuwa atahakikisha Utumishi wa Umma unakuwa na rasilimaliwatu yenye tija.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, Utumishi wa Umma ndio injini ya nchi hii, hivyo Viongozi na Watumishi wa Umma hawana budi kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema kuna baadhi ya Viongozi na Watumishi wenye nyadhifa wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kukandamiza watumishi walio chini yao kwa kusikiliza majungu na fitina.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (mwenye miwani) akipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe Salum Kali alipowasili Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kabla ya kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya leo ili kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu alipowasili Wilayani hapo kabla ya kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya leo ili kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali.

“Tuache kutumia nyadhifa tulizo nazo vibaya hivyo tufanye kazi, na kama kuna mtumishi ambaye amekuwa akitekeleza majukumu yake kikamilifu apewe ushirikiano na andelezwe ili aweze kutoa mchango mkubwa kwa taifa badala ya kujengewa uadui.

Aidha, amewataka Watumishi wa Umma kuwa na utamaduni wa kujiendeleza ili waweze kufika mbali. “Jambo lolote lenye mafanikio ni lazima lianzie mbali, hivyo ni vema kujiendeleza badala ya kubweteka,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kuzungumza na Watumishi Wilayani Magu kabla ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Kijiji cha Nyashigwe Wilayani Magu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news