Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa kinara wa ubunifu wa huduma na bidhaa katika soko na kutengeneza faida kubwa inayoiwezesha benki hiyo kutoa gawio kwa wanahisa wake.
Dkt. Mwigulu ametoa pongezi hizo wakati wa Semina ya Elimu ya Fedha na Uwekezaji iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa Wanahisa unaotarajiwa kufanyika hapo kesho 22 Mei 2021 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Akielezea namna ambavyo Serikali inajivunia utendaji wa Benki hiyo, Dkt. Mwigulu alisema Benki ya CRDB imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa kusaidia miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, pamoja na kuwekeza katika kupanua wigo wa ufikishaji huduma na kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa wananchi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba akihutubia katika
Semina ya Elimu ya Fedha na Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa
Wanahisa na Watanzania katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Arusha (AICC). Semina hiyo ilihudhuriwa na zaidi ya watu 2,000 ambao
wengi walihudhuria kupitia mtandao.
“Serikali inaichukulia Benki hii kama Benki kiongozi, na namna ambavyo mmekuwa mkifanya vizuri inadhihirisha hilo. Nimesikia hapa mwaka jana mmetengeneza faida kubwa pamoja na changamoto ya COVID-19, hii inaonyesha uimara wa benki hii na uimara wa sekta ya fedha nchini kwetu, hongereni sana na asanteni kwa kutupa heshima,”alisema Dkt. Mwigulu huku akiwahamasisha Watanzania kuwekeza katika hisa za Benki ya CRDB ili kupata faida.
Dkt. Mwigulu alisema ili sekta ya fedha iweze kufanya vizuri zaidi na uchumi wa Tanzania uendelee kukua kunahitajika elimu ya kutosha juu ya masuala ya fedha na uwekezaji kwa wananchi. Alisema kwakutambua hilo mwaka 2011 Serikali ilianzisha Mpango wa Taifa wa Elimu ya Fedha ikiwa na lengo la kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala ya fedha, kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa.
“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuwa bega kwa bega na Serikali katika kutoa elimu hii kwa wananchi, hii inaonyesha ni jinsi gani mnaishi maono ya Serikali, asateni sana,”aliongezea Dkt. Mwigulu ambapo pia alibainisha amekuwa akifuatilia semina hizo zinazoendeshwa na Benki ya CRDB ikiwamo ile ya uwezeshaji iliyofanyika mwezi Apri 2021 katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Dkt. Mwigulu pia alielezea mikakati mbalimbali inayowekwa na Serikali katika kuboresha sekta ya fedha nchini ambapo alisema Wizara yake inampango wa kuandaa kikao kazi cha mabenki na wadau wengine wa sekta ya fedha ili kujadili changamoto zilizopo na maeneo ya uboreshwaji ili kuweza kufikia lengo. “Naiomba Benki ya CRDB kama Benki kiongozi kuongoza katika hili, naamini mtatusaidia kuyaongoza mabenki na taasisi nyengine za fedha katika hili,”aliongezea Dkt. Mwigulu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay akitoa hotuba yake katika Semina ya Elimu ya Fedha na Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wanahisa na Watanzania katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Akitaja baadhi ya mambo ambayo Serikali imapanga kuyajadili, Dkt. Mwigulu alisema ni pamoja na uboreshaji wa sera za usimamizi wa sekta ya fedha, kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara hususan wajasiriamali wadogo kwa kuhakikisha benki zinatoa mikopo yenye riba rafiki, kuongeza ajira kwa wananchi, kupanua wigo wa biashara katika nchi jirani na kuwajengea wafanyabiashara uwezo wa kushiriki katika biashara katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alimshukuru Dkt. Mwigulu kwa kuikaribisha benki hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya fedha nchini. Vilevile alimhakikishia kuwa benki hiyo itakwenda kuandaa sera ambayo itakwenda kuelekeza na kusimamia uwezeshaji katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini. “Mheshimiwa Waziri nikuahidi kuwa tutakwenda kufanyia maelekezo yako kazi kwa kuweka mikakati itakayoongeza ushiriki wa benki yetu katika kukuza uchumi,” alisisitiza Dkt. Laay.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya Semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hapa nchini pamoja na kupata uelewa wa huduma za benki hiyo zitakazowasidia kuboresha maisha yao.
“Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.
Aidha, Nsekela alisema kuwa mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imependekeza gawio la shilingi 22 kwa hisa kufuatia ikiwa ni ongezeko la asilimia 29.4 kulinganisha na gawio la shilingi 17 kwa hisa lililotolewa mwaka jana ikitokana na kuongezeka kwa faida ya benki hiyo mwaka 2020 kufikia shilingi bilioni 175. “Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza ndani ya Benki yetu ili nawao waanze kunufaika na fursa hii,” alisisitiza Nsekela.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika Semina hiyo ikiwamo; Elimu ya Fedha na Uwekezaji, Biashara ya Hisa Kidijitali, Huduma za Bima na CRDB Wakala.
Washiriki wa Semina hiyo waliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo huku wakisema imesaidia sana kuongeza uelewa juu ya masuala ya fedha na uwekezaji.
Baadhi ya washiriki walipendekeza semina hiyo kufanyika mara kwa mara kwani bado uelewa wa masuala ya fedha na uwekezaji katika jamii bado ni mdogo.
Tags
Habari