Na Angela Msimbira, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu ameagiza kuanzia Julai Mosi mwaka Huu, kuanza uhakiki wa tiketi za kielektroniki katika usafiri wa mabasi yaendayo kwa haraka kwa kutumia mfumo wa POSS ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Hassani Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu kuboreshwa kwa usafiri huo.
Amesema kuwa utekelezaji wa hilo ni hatua za awali wakati unasubiriwa mfumo mkubwa utakaohuisha matumizi ya kadi na mageti ambao ndio utakaokuwa ni suluhu ya kudumu.
Waziri Ummy ametaka uhakiki huo wa kutumia poss kuanza haraka wakati mfumo mkubwa unaotarajiwa kutekelezwa Novemba mwaka huu, unasubiriwa ili kuepuka udanganyifu, wizi na upotevu wa mapato.
“Nataka mapema tuwe tumekomesha utoaji wa tiketi zisizohakikiwa, hapa tunaruhusu wizi kufanywa watu wanakuwa na vitabu vyao vya tiketi, Rais Samia na Waziri Mkuu waliyasema haya,” amesema Waziri Ummy.
Ameendelea kusema kuwa matumizi ya tiketi hizo kunapelekea kujitokeza kwa udanganyifu na wizi wa mapato kutokana na baadhi ya watendaji wasio waaminifu kuingiza sokoni tiketi zao na kusisitiza kuwa lazima kuwepo kwa utaratibu unaohakikisha tiketi zinatolewa moja kwa moja katika mashine na kumfikia abiria wakati huo.
Amesema, kuna changamoto nyingi zinazotokana na utoaji wa huduma katika mabasi yaendayo kasi ambazo kimsingi zinapaswa kutatuliwa kwa lengo la kumuondolea usumbufu mwananchi huku ikibainika kuwepo kwa hali kila upande kutotimiza majukumu yake kikamilifu.
Waziri Ummy amewaagiza watendaji wa Wakala wa mabasi yaendayo haraka ( DART) pamoja na mtoa huduma wa mabasi hayo (UDART) kukutana Dodoma katika kikao kitakachofanyika kesho ili kutafuta suluhisho la changamoto ya mabasi hayo Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na hilo Waziri Ummy amesema mrundikano wa abiria katika vituo vya mwendokasi ni vyema ukapatiwa ufumbuzi kutokana na kujawa na kero nyingi zinazowasababishia usumbufu abiria na hivyo kupoteza malengo ya mazima ya uanzishwaji wa mradi huo ulioanza kutumika mwaka 2016 ukilenga kuondoa changamoto ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Aidha, amewataka shirika la mabasi yaendayo kasi (UDART) ukajidhatiti kwa kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuzidi kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kupandishwa ya kupewa kazi ya kujenga mradi huo katika mikoa mingine ikiwemo ya Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa DART Dk Edwin Mhede amesema malengo ni kuhakikisha wanatatua changamoto zote zilizopo sambamba na kubuni mikakati mipya ili kutimiza malengo ya taasisi hiyo iliyopewa jukumu la kutoa huduma za usafiri kwa wananchi.
Amesema wao kama wakala wa utoaji wa huduma za usafiri wa mabasi yaendayo kasi, watahakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa zenye viwango bora huku akisisitiza kila mmoja akitekeleza majukumu yake kati ya wakala huo na UDART mambo yatakuwa mazuri.
Aidha katika ziara hiyo Waziri Ummy pia ametembelea karakana ya mabasi hayo inayojengwa katika eneo la Ubungo ili kujionea maendeleo yake pamoja na karakana ya Jangwani Jijini Dar es Salaam.
Tags
Habari