NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Ripoti zilizotufikia usiku huu zinaeleza kuwa, mfanyabiashara Bilionea Mtanzania na Diwani mstaafu wa Mbagala Kuu, Yusuf Manji amerejea Tanzania.
Ujio huo unaelezwa kuwa, ni hatua nyingine muhimu za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha mahusiano mema na wafanyabiashara wazawa ili kuhakikisha wanasaidia kujenga uchumi wa Tanzania.
Chanzo cha uhakika kimemweleza MWANDISHI DIRAMAKINI kuwa, Manji amereja nchini kimyakimya.
Ujio huu unaelezwa kuwa ni neema kwa wadau wa soka nchini, kwani kuondoka kwake kulikuwa mwanzo wa Yanga SC kuyumba kiuchumi.
"Inawezekana ndiyo safari ya timu yetu nzuri iliyoanguka tangu mwaka 2015, Simba wakachukua nafasi, ikarejea tena. Inshallah, tunamuombea ndugu yetu heri aweze kuanza upya, tupo naye pamoja,"kimedokeza chanzo hicho.
Bilionea huyo ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti na Mfadhili wa Klabu ya Yanga amewasili nchini jioni ya Juni 1, 2021.
Aidha, Yusuf Manji baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julias Nyerere amehojiwa na baadhi ya maafisa wa Uhamiaji juu ya uhalali wake wa kuingia nchini Tanzania.
Manji baadae aliachiwa baada ya maafisa hao kujiridhisha kuwa ni Mtanzania na alikuwa na haki ya kuingia nchini muda wowote.
Yusuf Manji ni nani?
Yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Quality Group Limited (QGL), kampuni binafsi inayomilikiwa na familia ya Manji.
Kulinganaa na wasifu wake, tajiri huyo ana ukwasi mkubwa wa fedha.
Mafanikio yaliyotokana na stadi za kipekee katika usimamizi wa biashara baada ya kuchukua kampuni iliyokuwa ikijihusisha na magari ya baba yake jijini Dar es Salam mwaka 1995 na kuibadilisha kuwa kampuni ya kimataifa yenye mafanikio na inayofanya kazi katika Mataifa mbalimbali Duniani ikiwemo Tanzania yenyewe,Umoja wa Falme za Kiarabu, India na Kenya.
Kampuni ambayo inaundwa na kampuni tanzu zaidi ya 10 ikijihusisha na uwekezaji katika magari,bidhaa za uhandisi, biashara za kimataifa, vifaa, mali zisizohamishika, usindikaji wa chakula, ushauri, usafirishaji, aluminium na sekta ya uvuvi.
Kampuni yake inakadiriwa kuajiri zaidi ya watu 3,500 ambapo unufaisha wategemezi 10,000 kila siku. Manji anatajwa kuwa mstari wa mbele kutoa udhamini kwa wanafunzi mbalimbali ikiwemo kusaidia misaada mingi kabla na baada ya matukio ya dharura katika jamii. (Ripoti hii imeandaliwa na Mwandishi Diramakini kwa maulizo; diramakini@gmail.com).