Buku Tano Inatosha ya Jatu Plc yabisha hodi kwa Watanzania wote

Na Mwandishi Diramakini

Kampuni ya Jatu Plc inayojishughulisha na uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na masoko kupitia mkuu wake wa Idara ya Masoko, Mauzo na Mahusiano, Mary Chulle amesema wanaendelea na kampeni ya kuhamasisha watanzania kununua hisa kwa kauli mbiu inayosema Buku Tano Inatosha

Amesema, wafanyakazi wa kampuni hiyo wanazunguka katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuhimiza wananchi kuchangamkia fursa ya kununua hisa kupitia kampuni hiyo ili kuweza kuwa sehemu yao.
Akizungumza leo katika makao makuu ya kampuni hiyo, Mary amesema Jatu Plc ni kampuni inayoundwa na wazawa ambayo imejikita kwenye uzalishaji wa mazao mbalimbali hivyo imeamua kuinua kipato cha mwananchi wa hali ya chini kwa kununua hisa.

Amesema kuwa, kampeni ya Buku Tano Inatosha imelenga kuwanufaisha zaidi wakulima wadogo na hata hivyo ni vema wakajitokeza kwa wingi kununua hisa ambazo zitamfanya yeye kuwa sehemu ya familia ya Jatu.

"Kampuni yetu ya Jatu Plc inajihusisha na masuala ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima kupata mikopo isiyokuwa na riba na pia mazao wanayozalisha wanayatafutia soko la kuyauza kupitia masoko ambayo wanakuwa wamewatafutia.

"Ili mambo hayo yaweze kukamilika pia lazima kuwa na kiwanda kizuri kitakachowafanya wakulima wauze mazao na kuweza kupata mitaji, hivyo mradi wa Shilingi bilioni 7.5 umelenga kwenda kuimarisha sekta ya kilimo na kuweka miundombinu mizuri ya umwagiliaji na kuwa mfano kwa wakulima,"amesema.

Ameongeza kuwa, pia mradi huo utakwenda kujenga kiwanda kizuri ambacho kitamilikiwa na wakulima wadogo kwa kuzingatia kuwa Jatu ni ya watanzania wa kawaida ambao ni wa kipato cha chini na hata cha juu.

Amefafanua kuwa, wamekuja na kauli mbiu ya Buku Tano Inatosha na mtu yeyote anaweza kununua hisa 10 kwa kuazia na kuendelea na kampeni hiyo inaendelea nchi nzima katika mikoa tofauti kama Mwanza, Arusha, Dodoma, Mtwara, NJombe pamoja na Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa Idara anawaalika watanzania wote kununua hisa za Jatu Plc ukizingatia ni kampuni ya vijana wa kitanzania hivyo kabla ya kumalizika kwa kampeni ni vema wakapata hisa.

"Hisa hizi zinalenga mtu yeyote bila kujali anafanya nini na hisa moja inanunuliwa kwa shilingi 500, lakini tumekuja na kampeni ya Buku Tano Inatosha ambapo unapata Hisa kumi,"amesema.

Mary amesema ili kupata hisa unaweza kunanunua kwenye Benki ya NMB,CRDB DCB pamoja na ofisi za Jatu ambazo zipo nchi nzima ikiwemo mikoa ya Mwanza ,Arusha, Mbeya, Mtwara lakini pia katika mitandao ya Vodacom,Tigo Pesa, Airtel Money, na wakala wa Jatu ambao wanazunguka huko mitaani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news