Chongolo atoa maagizo kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Daniel Chongolo ameutaka Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kutumia vikao vyao kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowahusu wanawake badala ya kutumia nafasi hiyo kuseng'enyana, kupeleka ajenda za siri jambo ambalo halina maslahi kwa Taifa.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Baraza Kuu la Wanawake wa umoja huo katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chama.

Chongolo amesema kuwa, kumekuwa na tabia ya kuitisha vikao mbalimbali, lakini badala ya kujadili ajenda zenye maslahi ya Chama na Taifa ,wanaanza kuwajadili watu,kuwazomea na nongwa jambo ambalo sio utaratibu.

Amesema kuwa, wanawake wanapaswa kuwa mwarobaini wa kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wanawake mijini na pembezoni vijijini kwani wengi hawana mitaji , sehemu za kufanya biashara na manyanyaso.

"Hili ni jeshi kubwa, lakini wapo baadhi wanaliaibisha kwa tabia zao niwasihi muache tabia ya kujadili watu kwenye vikao vyenu mara huyu ni mweusi,mwembamba ,mnene. Jambo ambalo sio utaratibu kabisa ,kumbukeni huko vijijini wanawake wanachangamoto nyingi ambazo zinapaswa kutatuliwa hasa mama wajasiriamali wakiwemo mama ntilie.

"Na wengine hutumia nafasi hiyo namna ya kugawana nafasi na kutengeneza makundi ambayo hayana tija. Hilo halikubaliki na mkae mkijua mimi ni bingwa wa kusimamia Ilani ya Chama lazima tusimamie miiko kwa maslahi ya Taifa letu,"amesema Chongolo.

Katika hatua nyingine amewataka wabunge wanawake kuhakikisha wanasimamia zile asilimia nne zinatotengwa na Halmashauri kwa ajili ya wanawake ili waweze kujiendeleza kwenye Biashara zao na kujiinua kiuchumi tofauti na hapo fedha hizo zitaishia kwenye mikono ya wajanja.

Hata hivyo amewataka kuhakikisha wanaimarisha chama kuanzia ngazi ya tawi kwa kushawishi watu kujiunga na chama na kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za wanachama wanapolipa ada, jambo ambalo ni uhai wa chama na sio kuwa na wanachama wengi ambao sio hai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news