Dar yatolewa na Mtwara robo fainali ya soka UMISSETA

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Kipigo cha magoli 5-4 ilichokipata timu ya soka ya wavulana ya mkoa wa Dar es salaam dhidi ya wenyeji Mtwarakwa njia ya mikwaju ya penati kimeiondoa timu hiyo katika kinyang’anyiro cha kuwania kombe la UMISSETA mwaka huu.

Licha ya kupoteza mchezo huo, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Dar es salaam walikuwa wakiongoza kwa magoli 2-0, lakini hali ya mchezo ilibadilika kipindi cha pili na kupelekea kusawazisha magoli hayo.
Hadi dakika 90 za mchezo kumalizika timu hizo zilifungana magoli 2-2, huku magoli ya Dar yakifungwa na wachezaji Juma Ahmad na Ibrahim Hussein kutoka sekondari ya Makongo huku magoli ya Mtwara yakifungwa na Ikram saidi na Abdul Mussa.

Katika mikwaju ya penati Mtwara walishinda 5-4, huku penati ya tano ikiwekwa wavuni na mchezaji AbdulAziz Said na kuibua nderemo na vifijo kwa wakazi wa Mtwara na viunga vyake.

Mara baada ya mchezo huo kocha timu ya soka ya mkoa wa Dar es salaam Abel Mtweve na viongozi wake iliwabidi kufanya kazi ya ziada kuwabembeleza wachezaji wa Dar waliokuwa wakibubujikwa na machozi kutokana na kutoamini kutolewa kwenye mashindano ya UMISSETA mwaka huu.
Naye Kocha wa Mtwara Mwalimu Hamis alisema wachezaji wake walishinda mchezo huo kutokana na wachezaji wake kucheza kwa morali na kujiamini hasa baada ya kuwa nyuma kwa magoli 2-0 katika kipindi cha kwanza aliwaambia hawana cha kupoteza wakikaba sana na kupambana kwa nguvu zao zote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kusimamia mchezo wa mpira wa miguu wa UMISSETA Israel Nkongo alisema kuwa ushindani na msisimko katika mchezo huo umeongezeka mwaka huu.

Nkongo ambaye ni refarii wa kimataifa alisema kuwa UMISSETA ya mwaka huu imeibua vipaji vingi vya wachezaji wanaofaa kucheza ligi kuu ya Tanzania lakini ameshangazwa kutoona wawakilishi wa vilabu vikubwa kuja kuona vipaji vya usakataji kabumbu.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya soka ya UMISSETA amewataka viongozi wa vilabu vikubwa kuyafuatilia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwani ndiyo chimbuko la wachezaji wote wakubwa waliowahi kuvuma na wanaocheza ligi kuu hivi sasa.

Aliwataka viongozi hao kuondokana na kasumba ya kila mwaka wakati wa usajili kukimbilia nje ya nchi kusaka vipaji vya soka ilhali wachezaji wenye vipaji wapo katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.

Katika michezo ya nusu fainali ya soka itawakutanisha wenyeji Mtwara watakaochuana na Dodoma na mabingwa watetezi wa kombe hilo Geita watachuana na timu ya soka ya Pemba leo katika Uwanja wa Chupo cha Ualimu Mtwara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news