Na Anneth Kagenda, Diramakini Blog
WANANCHI Kata ya Ndugumbi Wilaya ya Kinondoni wametakiwa kuwa katika hali ya utulivu wakati wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanesco wakiendelea kufanya marekebisho ya nguzo na nyaya za umeme.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Diwani wa kata hiyo, Thadey Siriamaka Massawe, mara baada ya kukagua zoezi la marekebisho ya nyaya hizo lililokuwa likifanyika kwenye kata yake na karibu kabisa na ilipo Ofisi ya Kata hiyo.
Mara baada ya kuona mwenendo mzuri na kasi ya hali ya juu iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi hao amesema kuwa ni vyema sasa wananchi wakawa na uvumilivu wa muda mfupi kwani badaye huduma ya umeme itarudi kwenye hali yake ya kawaida.
"Lakini pia nimeona ipo haja ya kupitia na kukagua ili kujihakikishia kwamba wananchi wangu hawaathiriki na marekebisho yanayoendelea lakini pia nitoe pongezi kwa Tanesco kwamba wanafanya kazi nzuri kwa lengo la kuwasogezea huduma muhimu wananchi,"amesema
Hata hivyo, amesema kuwa ni vyema kwa wananchi wakaendelea kutunza na kulinda miundombinu ya umeme kwa madai kuwa kufanya hivyo kutaifanya miundombinu hiyo kuendelea kudumu kwa muda mrefu na kuwaondolea usumbufu wa kukatika katika kwa umeme.
Tags
Habari