Na Anthony Ishengoma, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amesema atachukua hatua kwa watu ambao hawataki kuchukua tahadhari kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya ugonjwa wa Corona hususani katika kipindi hiki ambacho wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona linaonesha kuna wagonjwa katika mkoa wa Shinyanga.
Dkt. Sengati alisema kuna wananchi na wadau ambao hawataki kuzingatia masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya ili kujikinga na ugonjwa wa Corona na kuwataka watambue kuwa kuna Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 inayotaka mtu ambaye anaambukiza wenzake kwa makusudi wakati kuna njia za kujikinga achukuliwe hatua.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akipokea Mashine ya maarumu ya kusaidia wagonjwa wa Corona kutoka kwa Dkt. Frank Mtimbwa wa Shirika la World Vision Shinyanga jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati katikati, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile kushoto pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Yasinta Mboneko kulia wakiwa wamebeba Mashine ya maarumu ya kusaidia wagonjwa wa Corona mara baada ya kukabidhiwa mashine hiyo na Shirika la World Vision Shinyanga jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Dkt. Sengati alisema hayo jana katika kikao cha Siku moja cha Kamati ya Afya ya Mkoa ambacho pamoja na mambo mengine kilikaa kujadili namna bora ya kukabiliana na mlipuko wa wimbi la tatu la ugonjwa wa corona ujulikanao kama Covid 19 katika Mkoa wa Shinyanga.
Dkt. Sengati pia aliwataka wadau kutoka Asasi za Kiraia pamoja na viongozi wadini kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa umma na kusisitiza wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu na kuongeza kuwa viongozi wadini wakitumia sauti zao zenye mamlaka ya Mungu zinapokelewa kwa haraka sana tofauti na makundi mengine katika jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akiongea na wajumbe wa Kamati ya Afya ya Mkoa wa Shinyanga jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Naye mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga Dkt. John Luzila aliziomba Asasi za Kiraia Mkoani Shinyanga kuangali upya maeneo ya ufadhili na kuziomba kuchangia mitungi ya gesi ambayo ni gharama kubwa kutokana na mgonjwa mmoja wa Covid kutumia mitungi mitatu hadi mitano kwa siku jambo ambalo ni kubwa kulinganisha mapato ya hospitali.
Dkt. Luzila aliwambia wajumbe wa kikao hicho kuwa gharama ya mtungi mmoja ni shilingi elfu hamsini na kwa uzoefu alionao mgonjwa mmoja anatumia shilingi 150,000/= hadi 250,000/=kwa siku na baadhi ya wagonjwa wanakaa ndani ya oksijeni kwa takribani wiki moja au mbili na kuwa mzigo mkubwa kwa hospitali kughalimia.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Eudas Ndungile alisema kwa Mkoa wa Shinyanga ni muhimu kuchukua hatua kwa kuwa mkoa huo unawageni wengi kutoka nchi jilani ambao wamekuwa wakipita katika Manispaa ya Kahama na kuongeza kuwa mkoa unavuta watu kutoka maeneo mengine kufanya kazi katika migodi na kufanya biashara ya madini.
‘’ Wafanyakazi wa migodini wamekuwa wakifanya kazi kwa kubadilishana na kusafiri katika maeneo mengine ya Nchi na hivyo kuchangia katika kuleta au kueneza ugonjwa huu katika migodi na kwa wakazi wengine maeneo jilani na migodi hiyo’’. Aliongeza Dkt. Ndungile.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Bw. Saimon Berege aliwaambia wajumbe wa Kikao hicho kuwa tayari Halmashauri yake ina wagonjwa wa Covid na wengine vipimo vinapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa hatua za kiuchunguzi uku akiwataja wagonjwa hao kutoka Kakola ambalo ni eneo jilani na mgodi mkubwa wa Bulyanhulu.
Aidha Bw. Saimon Berege ameishauri Serikali Mkoani Shinyanga kuwataka wananchi kuacha kwenda katika maeneo yenye Mikusanyiko na kuanza kuchukua hatua kama ilivyo kwa nchi nyingine kwa kuzuia watu kuendelea kujaa katika viwanja vya mipira kabla hali haijaanza kuwa mbaya zaidi.
Katika hatua nyingine Shirika la World Vision Mkoa wa Shinyanga limetoa msaada wa vya vifaa tiba kwa ajili ya kusaidia kujikinga na kusaidia matibabu ya ugonjwa wa Corona yenye thamani ya Tsh. Milioni 126.2 na kukabidhi vifaa hivyo kwa Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Shinyanga kama ilivyo mikoa mingine ya Tanzania inachukua hatua kuhakikisha inapambana na kuenea kwa ugonjwa wa Covid baada ya Wizara ya Afya kutoa tahadhari ya kuwepo kwa viashiria vya wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona.
Tags
Habari