Hedhi salama kwa wanafunzi wa kike bado changamoto

Na Derick Milton, Itilima

Licha ya serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu mara kwa mara ya hedhi salama kwa wasichana, jambo hilo limeendelea kuwa changamoto kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari na msingi.

Asilimia kubwa ya wanafunzi hao hasa wale wanaotoka familia duni, wanakosa vipindi kuanzia siku tatu hadi tano kila mwezi kutokana na kupata changamoto kipindi cha hedhi kwa kushindwa kuendelea na masomo.
Mwanzilishi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha kumsaidia mtoto wa kike (Save The Girl Foundation) Monica Patric anasema kuwa wanafunzi kike shule za Sekondari wanakosa masomo mwaka mzima kutokana na hedhi.

Monica amesema hayo leo wakati wa maazimisho ya siku ya mtoto wa Africa, ambapo taasisi hiyo imetoa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike shule za Sekondari Lagangabili na Itilima zilizoko katika Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.

“Wanafunzi wa kike kwa shule za msingi hasa wale ambao wanatoka familia duni, wao kila mwezi wanakosa masomo kwa siku tano, hii inaonyesha kuwa kwa miaka minne ambayo wanakuwa shule, mwaka mzima wanakosa masomo kutokana na hedhi,” anasema Monica

Anaeleza kuwa licha ya suala la hedhi kwa mwanamke kuonekana kama jambo la kawaida, lakini kwa wasichana ambao wanatoa familia duni limekuwa changamoto kubwa na kusababisha wengi wao kushindwa kufikia ndoto zao.

“Kama taasisi tumetoa taulo hizi kwa wanafunzi wapato 76, na tumetoa taulo za kutosha ambazo watazitumia hadi wanahitimu masomo yao kidato cha nne, na kuanzia leo kwa wanafunzi hawa hakuna hata mmoja ambaye atakosa masomo tena,” amesema Monica.

Aidha, amesema kuwa ili kuweza kupambana na changamoto hiyo, lazima elimu iweze kutolewa kwa makundi yote, wazazi, walezi pamoja na wanaume ili kila mmoja aweze kutambua umuhimu wa mtoto wa kike ambaye amepevuka hedhi kwake ni jambo la kawaida.

Ameeleza kuwa, kama taasisi lengo lao ni kuhakikisha wanatoa elimu rika, ambayo itawasaidia wanafunzi wa kike wasikose masomo kutokana na hedhi, bali waendelee na masomo hata kama watapata jambo hilo.

Baadhi ya wanafunzi walishukuru kwa msaada huo, ambapo mmoja wa wanafunzi hao Rehema Charles akaeleza kuwa kila mwezi ilimlazimu kukaa nyumbani siku tano pindi anapoingia kwenye hedhi.

"Nashukuru kwa msaada huu, sasa sitaweza kukaa nyumbani kwa sababu ya hedhi kutokana na taulo hizi ambazo tumepatiwa, ni kweli jambo la hedhi limekuwa changamoto kubwa sana kwetu kwani linatufanya kukosa masomo,” amesema Charles.

Katika risala yao wanafunzi wa kike wameitaka serikali pamoja na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wazazi au walezi kuacha suala la ubaguzi kwa watoto wa kike na wakiume.

“Kwenye jamii yetu mtoto wa kike yeye kazi zote za nyumbani anatakiwa kuzifanya huku wa kiume akipewa muda wa kujisomea, tunaomba ubaguzi huu upigwe vita kwani unatufanya watoto wa kike kikosa haki zetu,”amesema Minza Joseph msoma risala.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa halmashuari kama mgeni rasmi, Ofisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo Jonathan Buluba, amewataka wazazi wenye watoto wenye umri wa kuanza shule kuhakikisha wanakwenda shule kama haki yao ya msingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news