Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila amezizuia kuendelea kununua pamba kampuni mbili zilizopewa vibali vya kununua zao hilo kwenye mkoa huo katika msimu wa mwaka huu 2021/22.
Kafulila amezitaja kampuni hizo leo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, kamati ya ulinzi na usalama mkoa kuwa ni CHISANO Co. Ltd ya Wilayani Busega mkoani humo, pamoja na BIRCHARD Co. Ltd kutoka jijini Mwanza.
Amesema sababu za kufikia uhamuzi huo, inatokana na kampuni hizo kudaiwa kuhusika katika kuhujumu mbegu za pamba ambazo zilitolewa na Bodi ya pamba kwenda kwa wakulima.
Kafulila amesema kuwa kampuni hizo zilihujumu mbegu hizo kiasi cha tani 20, ambazo zilikamatwa mwezi Novemba, 2020 uko Wilayani Busega zikiwa zinapelekwa kwa ajili ya kuchakata mafuta badala ya kwenda kwa wakulima.
Ilidaiwa kuwa mbegu hizo zilikamatwa zikiwa kwenye kiwanda cha Chisano, huku zikiwa zimepakiwa kwenye gari la kampuni ya Birchard na zilikuwa maalumu kwenda kwa wakulima lakini zikakutwa zinapelekwa kukamuliwa mafuta ya kula.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa ameagiza vyama vyote vya msingi ambavyo vilikuwa vimepokea pesa kwa ajili ya kukusanya pamba kutoka kwenye kampuni hizo visitishe mara moja na pesa hizo zirujeshwe.
“Kuanzia sasa hivi ni marufuku kwa kampuni hizo kuendelea kununua pamba kwenye mkoa huu, najua walipewa vibali lakini ni kimakosa, Amcos ambazo zilipewa pesa, kuanzia sasa sizitishe kununua na pesa zirejeshwe kwenye kampuni hiyo,” ameongeza Kafulila.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali haitawavumilia watu wote ambao wapo kwa ajili ya kuwahujumu wakulima au kukwamisha jitihada za serikali za kuboresha zao hilo.
Alisema kuwa, hatua nyingine kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa watu wote ambao walihusika katika uhujumu wa mbegu hizo, ikiwemo wale ambao walisababisha mbegu hizo zichukuliwe badala ya kwenda kwa wakulima.
“Wapo watu ambao walichepusha hizo mbegu, nao hatua dhidi yao zitachukuliwa, uchunguzi utafanyika kwa wahusika wote kuanzia Bodi ya pamba,” amesema Kafulila.
DIRAMAKINI Blog imewatafuta viongozi wa kampuni hizo, ambapo Mkurugenzi wa Chisano Peter Bahini amekiri kuwa mbegu hizo zilikamatiwa kwake lakini hakuhusika katika uhujumu wa mbegu hizo.
“Ni kweli mbegu zilikamatiwa kwangu, lakini wamiliki wa hizo mbegu walikuja tu kupima mzigo wao, hivyo mimi sihusiki…ninachokiomba haki itendeke na niruhusiwe kununua pamba,” amesema Bahini.
Naye Mkurugenzi wa Birchard Arshard amesema kuwa bado wao kama kampuni hawajapata barua rasmi ya zuio hilo, pindi watakapoletewa wataweza kuzungumzia jambo hilo “ Kwa sasa hauwezi kusema chochote,” amesema Arshard.
Tags
Habari