Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema kuwa amezuia malipo kwa kampuni ya ukandarasi CHICCO ambayo inajenga barabara ya Mwigumbi – Maswa km 50 kwa kiwango cha lami kutokana na kujengwa chini ya kiwango.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila akizungumza na wafanyakazi wa Mkoa huo leo ofisini kwake.
Kafulila amefikia maamuzi hayo ikiwa imepita wiki moja tangu afanye ziara kukagua ujenzi wa Barabara hiyo na kukuta eneo kubwa la barabara hilo likiwa limeharibika kwa kiwango kikubwa.
Mkandarasi hiyo kutoka China anajenga Barabara hiyo kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 60, huku ikiwa imeanza kuharibika na kujaa mashino kabla haijafunguliwa.
Akizungumza leo kwenye kikao na wafanyabishara ambao walitoa malalamiko juu ya ubovu wa miundombinu ya barabara mkoani humo, Kafulila amesema kuwa tayari ameanza kufanyia kazi changamoto hiyo.
Amesema kuwa katika hatua za mwanzo, amezuia malipo kwa mkandarasi huyo mpaka pale atakapofanya marekebisho kwenye barabara hiyo maeneo yote ambayo yameharibika.
"Hatuwezi kumlipa mkandarasi kiasi kikubwa cha pesa, lakini barabara inaanza kuharibika kwa kiasi kikubwa kabla haijafunguliwa, na tutafanya uchunguzi wa miradi yote iliyopo chini ya TANROADS pamoja na TARURA,”amesema Kafulila.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amesema ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa mikataba 31 ya TANROADS mkoani humo, ambayo wameitoa kwa wakandarasi kutengeneza barabara katika mwaka huu wa fedha 2020/21.
Amesema kuwa, kuna uwezekano wa Barabara hizo kujengwa chini ya kiwango chanzo chake kikawa ni mikataba hiyo, ambapo ameagiza mikataba hiyo 31 yenye thamani ya sh.Bilioni 17 kuchunguzwa kwani fedha nyingi zimeletwa mkoani Simiyu.
“Baada ya kujionea hali ya barabara hiyo, mbali na kuagiza mkandarasi asilipwe ili afanye marekebisho, lakini nimeagiza mikataba yote ichunguzwe,” ameongeza Kafulila.