KALEMANI: EPUKA UTAPELI,LIPIA UMEME TANESCO

Dkt.Medard Kalemani ambaye ni Waziri wa Nishati amewaomba wananchi kufanya malipo yao ya kuunganishiwa umeme kwenye ofisi za Tanesco na kuepuka kulipa kwa watu ambao hawahusiki na kutoa huduma hiyo ili kuepuka usumbufu na kutapeliwa, anaripoti ROBERT KALOKOLA (Diramakini Blog) Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akibonyeza kitufe kuwasha umeme katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Chato.(picha na Robert Kalokola).

Waziri Kalemani amesema, wananchi wanaohitaji kulipia umeme ni lazima kufanya malipo hayo kwa utaratibu wa shirika na inapotea changamoto yoyote kama kuchelewa kuunganishiwa na nyingine mwananchi aonane na uongozi hasa meneja wa ngazi husika ili kuepuka usumbufu.

Ametoa wito huo katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Chato mkoani Geita alipokuwa anawasha rasmi umeme katika kijiji hicho katika Jimbo la Chato ambalo yeye ni mbunge pia.

Mheshimiwa Waziri Kalemani amesema, malalamiko mengi kuhusu wateja kuombwa rushwa au kutapeliwa yakifuatiliwa unakuta wakilalamikiwa siyo wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).


Pia amewaomba wananchi wasitoe fedha kwa vibarua na vishoka badala yake wajenge tabia ya kuwasilisha malalamiko yao kwa mameneja ili yaweze kutatuliwa.

Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Mtakuja wamesema, huduma ya umeme kufika katika kijiji hicho inafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwao.

Henry Makoye (43) mkazi wa kijiji hicho amesema, umeme utawasaidia kufanya shughuli za uchomeleaji kwa kutengeneza milango ya vyuma ambayo huduma hiyo ilikuwa inapatikana mbali kabla umeme kufika.

Amefafanua kuwa, huduma hiyo ilikuwa inapatikana Chato Mjini kwa kuwa ndipo umeme wa uhakika ulikuwa unapatikana pamoja na vijana wanaojua kuchomelea milango na madirisha.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akionyesha kifaa maalum cha kutumika kusambaza umeme kwenye nyumba kwa gharama ndogo bila kutumia nyaya nyingi. (Picha na Robert Kalokola).

Aidha, amesema ajira zitakuwepo kwa vijana kwa kujiajiri kwenye miradi mbalimbali kama kusaga nafaka,saluni za kunyolea nywele, kuchomelea na mengine mengi.

Naye Maria Sengerema (48) ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Mtakuja amesema kuwa, kuunganishiwa umeme kijijini hapo kumesaidia wanawake kutotembea umbali mrefu kwenda kusaga nafaka.

Amefafanua kuwa, kabla ya kuunganishiwa umeme walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya kusaga nafasi kwa ajili ya kupata unga.

Ameeleza kuwa, mashine zilizokuwa zinatumika kusaga zilikuwa za kutumia mafuta na zilikuwa mbali na huduma yake ya kusaga taratibu.

Baada ya umeme kuwafikia,Maria amesema baadhi ya wananchi wenye uwezo kiuchumi wamesogeza mashine za kutumia umeme kijijini hapo na huduma ya mashine za umeme zinafanyika kwa haraka zaidi.

Pamoja na kuwasha umeme rasmi katika kijiji hicho, Waziri Kalemani amewataka wananchi kulipia umeme ili waweze kuunganishiwa kwa sababu serikali imeshusha bei hadi 27,000 kwa vijijini na mjini.

Aidha, amesema nguzo za umeme kwa sasa zinatolewa bure kwa mwananchi na haziuzwi kama zamani.

Waziri Kalemani alikuwa kwenye ziara katika Jimbo la Chato ambapo mbali na kuwasha umeme katika kijiji cha Mtakuja ,pia alikabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo cha Afya Bwina na kufanya kikao cha ndani pamoja na watumishi wa Chama cha Ushirika cha Chato (CCU) ambayo kinamiliki kiwanda cha kuchambua pamba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news